Sightsavers kushirikiana na Serikali kutokomeza upofu

Muktasari:
- Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo linalopambana na upofu na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Dk Caroline Harper alitoa ahadi hiyo juzi, alipozungumza na wakazi wa Mtaa wa Said Domo, Mlandizi ilipo kambi ya kliniki ya utoaji wa huduma ya urekebishaji wa vikope.
Kibaha. Shirika la kimataifa la Sightsavers litaendelea kushirikia na Tanzania bega kwa bega kuhakikisha hakuna tishio la upofu kwa wananchi wake, imeelezwa.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo linalopambana na upofu na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Dk Caroline Harper alitoa ahadi hiyo juzi, alipozungumza na wakazi wa Mtaa wa Said Domo, Mlandizi ilipo kambi ya kliniki ya utoaji wa huduma ya urekebishaji wa vikope.
Kambi hiyo inaendeshwa na Sightsavers ikishirikiana na Serikali kwa ajili ya kutoa huduma ya vikope, mradi unaolenga kutokomeza ugonjwa wa trakoma unaosababisha upofu.
“Nafurahia kuja Tanzania ikiwa mara yangu ya tatu. Nimejionea mwamko wenu wa kufanya uchunguzi wa macho, itabidi kuongeza fedha ili kuwasaidia Watanzania. Kama kuna wengine mnawajua (wenye matatizo ya macho) waambieni waje kufanya uchunguzi,” alisema Dk Harper.
Aliwaahidi wakazi hao kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watafanya kila liwezekanalo ili kutokomeza upofu.
Mratibu wa mradi huo, Mkoa wa Pwani, Angela Michael alisema kabla ya kukutana na watu wenye matatizo ya macho, wamekuwa wakitoa elimu kwa wahudumu wa afya vijijini namna ya kuwatambua wenye matatizo hayo.
Mmoja wa wanufaika na mradi huo, Asia Abdallah alilishukuru shirika hilo na Serikali kwa kutoa huduma hiyo ya macho ambayo ni tatizo kwa wananchi wengi.
“Sina cha kukupa mama (Dk Harper). Ila Mungu ndiyo atakulipa na uendelee na moyo huu kwa kuwasaidia Watanzania wengine wasiopata huduma hii,” alisema.
Daktari wa Macho wa Hospitali ya Bagamoyo, Francis Onesmo aliyekuwa miongoni mwa watoa huduma katika kliniki hiyo, alisema mazingira machafu hasa sehemu za ufugaji ni miongoni mwa sababu zinazochangia ugonjwa wa vikope.