Siku, dakika za mwisho kabla ya Ben Saanane kutoweka

Mkuu wa Idara ya Sera na Utafiti Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Ben Saanane.Picha na Maktaba.

Muktasari:

  • Zikiwa zimesalia siku zisizozidi 30 kabla ya kutumia mwaka mmoja tangu Ben Saanane atoweke, maswali kuhusu sehemu alipo hayajakoma na wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba aliulizwa kuhusu kada huyo wa Chadema. Gazeti la Mwananchi linaangalia matukio kadhaa yaliyoambatana na kutoweka kwake.

Siku chache kabla ya kupotea katika mazingira yasiyoelezeka, kada wa Chadema, Ben Saanane alifanya mambo mengi kama mawasiliano yake binafsi na pia ya chama chake.

Hata hivyo, kati ya mawasiliano hakuna kilichosaidia kung’amua ni katika mazingira gani mwanasiasa huyo kijana alipotea na yuko wapi hivi sasa; hai au amekufa.

Novemba 14 mwaka jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa Ben kuonekaka ofisi za makao makuu ya Chadema yaliyopo Mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni ambako alitumia muda wake mwingi.

Siku hiyo alisaini kitabu cha mahudhurio ya watumishi wa ofisi hiyo na kufanya shughuli zake za kichama. Hiyo ikawa siku ya mwisho kwa Wanachadema kumuona.

Ben alikuwa msaidizi wa karibu wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akimsaidia kufanya tafiti na uchambuzi katika masuala ya siasa na uchumi.

Siku alipotoweka, vikao vya Bunge vilikuwa vikiendelea mjini Dodoma, na ni katika kipindi hicho hicho Taifa lilitangaziwa kifo cha aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta.

Wakati hayo yakitokea, Ben hakuwa Dodoma na bosi wake lakini aliwasiliana na Mbowe kwa kumtumia ujumbe mfupi wa simu kumpa pole kwa msiba mkubwa wa kitaifa. Hii ikawa mara yake ya mwisho kuwasiliana na Mbowe.

Ingawa kwa wanachadema, Novemba 14 ilikuwa siku ya mwisho kuonana naye, kwa majirani zake na watu wengine walikuwa na siku moja zaidi. Siku iliyofuata, yaani Novemba 15, Ben aliamkia nyumbani kwake Mabibo jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya ufuatiliaji wa mawasiliano yake ya simu inaonesha kuwa Ben alitoka Mabibo asubuhi na kwenda au kupelekwa maeneo ya mikocheni ambako alitumia muda mrefu sana huko.

Mawasiliano yanaonyesha baada ya kutumia masaa kadhaa eneo la Mikocheni, alirudi ama kurudishwa eneo la Mabibo jioni. Alikuwa na nani na akifanya nini ni swali ambalo si ndugu zake wala vyombo vya usalama wameweza kulijibu.

Ufuatiliaji wa mawasiliano yake unaonyesha pia kuwa siku hiyo hiyo jioni simu yake ilitumika kutoa Sh50, 000 kwa wakala wa M-Pesa aliye eneo la Mburahati. Hiki kilikuwa kitendo cha mwisho kufanywa na Ben kupitia simu yake ya mkononi. Tangu hapo utambuzi wa simu yake ukapotea kabisa katika mtandao.

“Tumejaribu kufuatilia inaonekana wamei-block (wameizuia) ile simu,” alisema John Mrema, ambaye ni mkurugenzi wa uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema.

“Mtu anayeweza kufanya hivyo si mtu wa kawaida. Tulikuwa tunatumia njia mbalimbali kutafuta taarifa za Ben, sasa huwezi tena kum-trace (kumpata).

“To be frank (kusema kweli) ukitafuta namba ya Bern Saanane, ukiingiza kwenye system (mfumo) yao, unatakiwa uwe na password (nywila). Na ni simu hiyo tu sio simu zote zina password. So inaonekana ni mtu mmoja tu ndio anaweza kuaccess details (kuziona taarifa) za simu ya Ben.

“Kwa hiyo, inaonekana kuna mtu ambaye anacontroll (anadhibiti) hiyo system.”

Wakati ndugu wa karibu na viongozi wa Chadema wakitumia kila mbinu kujua aliko Ben, Desemba 24, siku moja kabla ya sikukuu ya Krismas mwaka jana, mtu asiyejulikana aliingia katika akaunti yake ya Facebook na kufuta baadhi ya maandishi yake yaliyokosoa viongozi wa juu serikalini.

“Huyu mtu aliingia kwenye akaunti ya Facebook ya Ben jioni na kufuta baadhi ya maandiko yake yoliyokuwa yanakosoa viongozi wa nchi.

“Sasa huyo aliyeweza kuwa na access (ruhusa ya kuingia), maana yake ni mtu aliyekuwa na password (nywila). Ni nani (huyo)?” anauliza Mrema.

“Ama alikuwa ni Ben mwenyewe na wakahakikisha anawapa password. Mashaka yetu yako hivyo.”

Kwa muda mrefu kabla ya kutoweka, Ben aliandika sana mawazo yake katika ukurasa wake wa Facebook, akichangia mijadala mingi ya kitaifa. Wakati mwingine aliwakosoa viongozi wakuu serikalini na wanasiasa.

“Ilifika mahali alipokea sms za vitisho zikimuonya kwa maneno kama ‘wewe endelea kuandika, kuna siku utajikuta uko mbele ya mamba peke yako’. Siku alipotushirikisha tulimwambia akaripoti polisi, na kweli alienda kuripoti. Sasa katikati ya sakata hilo ndio akapotea,” alisema Mrema.

“Sisi tuna shaka kwamba Ben alitekwa na watu wa usalama. Na tunasema hivyo kwa sababu moja kubwa, familia yake na sisi tumeomba polisi watuletee mawasiliano yake ya mwisho ya simu, wamekataa. Kwa sababu ingekuwa rahisi sana kujua aliwasiliana na nani mara ya mwisho na kuanza uchunguzi kuanzia hapo,” anasema Mrema.

Safari ya Afrika Kusini

Siku aliporipoti ofisi za makao makuu ya Chadema (Novemba 14, Ben aliaga baadhi ya watumishi wenzake kwamba alikuwa akijiandaa na safari ya Afrika Kusini kutetea tasnifu (thesis) yake ya Shahada ya Uzamivu (PHD) aliyokuwa akisoma.

Kwa zaidi ya miaka miwili kabla ya kutoweka, mwanaharakati huyo alikwenda Uholanzi mara kwa mara kwa ajili ya masomo yake hayo ya PHD. Mara tu baada ya tetesi za kutoweka kwake kuanza kusambaa, walioufahamu mpango wake huo hawakuwa na shaka kwani waliamini tayati angekuwa ameshaondoka kwenda Afrika Kusini.

Ilipofika Novemba 18, siku nne baada ya kuonekana makao makuu ya chadema, viongozi wa chama chake na ndugu zake walistuka baada ya familia yake kuanza kulalamika Ben haonekani nyumbani.

“Na sisi tukastuka, tukafanya jitihada za kuitafuta familia, tukakutana na dada yake, tukakutana na mdogo wake wakatuambia hajasafiri. Tukasema hapana, tukatumia network (mtandao) yetu kwenda uhamiaji lakini system za uhamiaji hazionyeshi kama amekwenda nje ya nchi. Kwa hiyo, tukajiridhisha kwamba hajaondoka nchini,” alisema Mrema.

“Tuliendelea kuwa na shaka tukasema ngoja twende Johannesburg, Afrika Kusini kujiridhisha endapo hajafika huko. Tulijiridhisha hajafika huko. Alikuwa ndani ya mipaka ya nchi na system ya uhamiaji imetuthibitishia.”

Habari hii ya kupotea kwa Ben Saanane itaendelea kesho.