Simanjiro yatakiwa kuweka usalama wa chakula

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera akizungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo juu ya wakulima kuhifadhi mazao kupitia mpango wa stakabadhi ghalani. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Kutokana na ukame uliojitokeza kwa zaidi ya miaka mitatu, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wametakiwa kutunza mazao waliyonayo kwa ajili ya usalama wa chakula.

Simanjiro. Wananchi na viongozi wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, katika kuhakikisha wanapambana na njaa wametakiwa kuweka usalama wa chakula kwa kukitunza kilichopo kwani kwa zaidi ya miaka mitatu wamekumbwa na ukame.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera akizungumza na madiwani na watumishi wa halmashauri kwenye mafunzo ya stakabadhi ghalani amesema suala la usalama wa chakula ni muhimu.

Dk Serera amesema kutokana na elimu iliyotolewa na wataalam kutoka bodi ya usimamizi wa stakabadhi ghalani, itabadili mitazamo ya wakulima ili kuwakwepa walanguzi wa mazao.

“Simanjiro tujipange sasa kwa mazao ya kuhifadhi ghalani, iwe ni mahindi, maharagwe, vitunguu maji, alizeti au mengineyo, tukakae na wakulima na kujadili hili,” amesema Serera. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Samwel Gunza alisema suala la kuwepo na stakabadhi ghalani ni jambo muhimu kwa wakulima hivyo wanapaswa kutekeleza.

“Stakabadhi ghalani itawasaidia wakulima kwani kule Mtama mkoani Lindi nilikuwa mkurugenzi kabla sijahamia Simanjiro, walifanikiwa kuwaepuka walanguzi maarufu kama kang’omba,” amesema Gunza.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga alisema kuwepo na mizani katika minada kutasaidia tija kwa wafugaji na wakulima kwani watapima kwa uhakika.

“Mnapokuwa na mizani kwenye minada kutamnufaisha mfugaji kwani atatambua ng’ombe ana kilo ngapi na siyo kupima kwa macho na mkulima atabaini uzito wa mazao badala ya rumbesa,” amesema Kanunga.

Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Materi amesema suala la biashara kwa njia ya mtandao ni zuri kwani mkulima au mfugaji anaweza kuuza zao lake bila kuonana na mnunuzi.

“Japokuwa hilo litakuwa jambo geni hapa kwetu Simanjiro ila ni zuri kwani dunia imeenda kasi mno kwa kupitia mtandao mnaweza kufanya biashara bila kuonana,” amesema Materi.

Meneja mipango na uhamasishaji wa bodi ya usimamizi wa stakabadhi ghalani, Sura Ngatuni amesema hivi sasa walanguzi wanaingia shambani na kurubuni wakulima hivyo wanapaswa kupewa elimu ya stakabadhi ghalani ili wahifadhi mazao yao na kubakiza yakutumia.

“Mfano mtu anae lima gunia zake 100 anapaswa kujipanga kuwa ataweka ya chakula gunia ngapi za kula na familia na nyingine ahifadhi ghalani na kuepuka kurubuniwa na walanguzi,” amesema Ngatuni.