Simbachawene atoa siku 14 kituo cha polisi kuhamishwa

Thursday March 04 2021
simbachawene
By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene ametoa wiki mbili kituo cha polisi kihamishiwe katika mji mdogo wa Mtera ili wananchi zaidi ya 10,000 wanaoishi kata hiyo waweze kupata huduma kwa ukaribu.


Kuhamishwa kwa kituo hicho kutawafanya wananchi hao kuondokana na adha ya kutembea zaidi ya kilomita tano kwenda kituo cha polisi kilichopo eneo la Mtera Camp.


Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji huo wa Mtera, Simbachawene amesema baada ya kukikagua kituo hicho amebaini kipo porini kama wananchi wanavyosema na kwamba kuna umuhimu kituo hicho kuhamishwa.


Advertisement

“Kazi ya Jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zao, kituo kipo porini na uhalifu mwingi unatokea barabarani, wahamiaji haramu polisi wenyewe wanawakamatia hapa barabarani, wezi, wahalifu, wapiga dili na majambazi wote wanakamatiwa huku wanakoishi watu.”


“Kituo kipo mbali kabisa porini kwa sababu kilikuwa ni kambi waliorithi wakati wa ujenzi wa kituo cha Mtera zamani wakawekwa kule na polisi wakabaki kule,” amesema Simbachawene.


Amesema uwepo wa kituo hicho katika eneo hilo pia ni hatari kwa usalama wao kutokana na kile alichobainisha kuwa nguvu ya polisi ni wananchi kwa sababu jeshi hilo ni la usalama wa raia na endapo polisi wakizidiwa wanawaomba wananchi wawasaidie.


 “Hivi wakivamiwa kule watasaidiwa na nani, si mtakuta wamekufa wote, na wenyewe wapo wangapi watano, sijui sita, kule ni porini. Kimsingi busara zote zinataka tufikirie upya, kituo kile kinatakiwa kihame kije huku barabarani, uamuzi wangu ni kwamba kituo kile cha polisi ndani ya siku kumi na nne kiwe kimehamia hapa barabarani,” amesema Simbachawene


Baada ya mkutano wa hadhara, Simbachawene alikubaliana na viongozi wa kata hiyo kuyachukua majengo yaliyokuwa zahanati ya zamani ya Mtera yatumike kwa ajili ya kituo cha polisi pamoja na zahanati hiyo ilitumike kwa ajili ya makazi ya mkuu wa kituo hicho.

Advertisement