Simiyu wazindua mfumo kutoa taarifa kimkoa

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda akizungumza katika hafla ya uzunduzi wa mfumo wa tehama wa Simiyu Info. Picha na Samirah Yusuph
Muktasari:
- Mkoa wa Simiyu umezindua mfumo wa tehama wa ‘Simiyu Info’ kwa lengo la kutoa taarifa wakati halisi mtandaoni, hali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Simiyu.
Bariadi. Mkoa wa Simiyu umezindua mfumo wa tehama wa ‘Simiyu Info’ kwa lengo la kutoa taarifa wakati halisi mtandaoni, hali ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Simiyu.
Mfumo huu utasaidia asasi za umma na binafsi ziweze kutazama na kuibua chachu za maendeleo ya mkoa kupitia mpango wa maendeleo wa malengo ya maendeleo endelevu.
Akitoa taarifa ya mfumo huo Kaimu Afisa Tehama wa Mkoa huo, Fredrick Mhagama amesema faida za mfumo huo kuwa utarahisisha utendaji kazi, mawasiliano ya haraka, utoaji na ukusaji na upatikanaji wa taarifa, pamoja na kupata taarifa ukiwa nje ya mkoa na urahisi wa kufanya maamuzi kwa viongozi.
"Utoaji wa elimu juu ya malengo endelevu ya kimataifa na malengo ya endelevu ya miaka mitano ya kitaifa kwa watumishi wa Idara za Afya, Elimu na maendeleo ya jamii na wadau wengine pamoja na ulinganishaji wa mahitaji ya watumiaji wa mfumo na malengo endelevu ya kimataifa na malengo ya endelevu ya miaka mitano ya kitaifa," amesema.
Ameongeza kuwa mfumo huo unaweza kufanya kazi kama ulivyotarajiwa kwa kuzingatia mahitaji ya watumiaji kupitia taarifa kutoka kwenye mfumo unaweza kubaini chanzo cha changamoto na kutafuta ufumbuzi wa kudumu na kuondoa kabisa tatizo.
Akiuelezea mfumo huo, muwakilishi wa Mkurugenzi wa Kitengo cha Tehama kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambao ndio wasanifu wa mfumo huo, Frank Msuya amesema kuwa mfumo huo ni endelevu na umezingatia usalama wa mitandao na utajumuisha sehemu mbili ambazo ni faragha na umma.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa huo, Dk Yahya Nawanda amesema sababu zilizosababisha kusanifiwa kwa mfumo huo ni pamoja na changamoto za gharama kubwa za uandaaji na ukusanyaji wa taarifa katika halmashauri sita za mkoa huo.
Ugumu wa kupatikana kwa wakati kwa takwimu kuhusu afya, maendeleo ya jamii na elimu, wataalamu na wadau wengine wa maendeleo kutumia muda mwingi kukusanya taarifa wakati wa kuendesha shughili zao za maendeleo.
Pamoja na uwepo kwa taarifa zinazotofautiana katika sekta tofauti kunakotokana na vyanzo vya taarifa kuwa vingi na vingine siyo sahihi na ugumu wa kupata kwa wakati vihatarishi au vidokezo vya hatari vinavyoweza kusaidia kuandaa mpango wa mwaka wa maendeleo na ufuatiliaji.
"Kutokana na changamoto hizo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na wadau wa Maendeleo imeamua kusanifu mfumo wa Ki-elektroniki kukusanya taarifa ambao unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu," amesema Nawanda