Simulizi binti aliyebakwa na wanaume wawili na kuambukizwa Ukimwi

Sunday April 04 2021
Simulizi pc
By Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Mtoto wa kike wa miaka 15 ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Temeke jinsi alivyobakwa na mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi.

Kitendo hicho kinadaiwa kufanywa Juni 25, 2020 katika maeneo ya Kijichi, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam na mwanafunzi wa IFM, Godbless Eneriko.

Mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari (jina linahifadhiwa) alidai wakati akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Anna Mpessa, huku akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Cecilia Mkonongo.

Binti huyo alidai kuwa wakati akisoma shule alikuwa akiishi na baba yake eneo la Tabata na inapofika kipindi cha likizo alikuwa akienda kuishi na mama yake mzazi Kijichi kwa sababu wawili hao walishatengana.

Alisema walipofunga shule Desemba, 2019, wakati huo akiwa kidato cha kwanza, alikwenda Kijichi kwa mama yake na akiwa huko siku moja mshtakiwa alipiga simu ya nyumbani kwao ambayo aliipokea na mtu huyo kujitambulisha kuwa yeye ni jirani yao.

“Huyu mshtakiwa alikuwa na mazoea ya kuja nyumbani kumfuata kaka Frank.

Advertisement

“Aliponipigia simu nilipokea na kumuuliza wewe ni nani akanijibu ni jirani yako Godbless na nilimuuliza namba hii kakupa nani akaniambia ‘tuliza hasira mrembo’,”alidai mtoto huyo.

Alidai Desemba 25, 2019 walikutana na mshtakiwa huyo na kumwambia waende nyumba ya kulala wageni na walipoingia ndani mtoto huyo alihoji kwa nini amempeleka maeneo hayo yanayotumika kufanyia mapenzi, ndipo mshtakiwa akamweleza hawezi kufanya chochote isipokuwa ana maongezi naye.

Alidai mshtakiwa alimweleza kuwa kama hamwamini ashike funguo wa mlango wa chumba walichokuwamo na kwenda kukaa kwenye stuli na kumueleza anampenda na anataka wawe wapenzi.

“Siku hiyo hatukufanya chochote. Baada ya maongezi mshtakiwa alinipa Sh 22,000 ambazo kati ya hizo Sh 2,000 niliitumia kupanda bodaboda kuelekea Tabata nilipokuwa nikiishi na baba na Sh 20,000 nilinunulia simu aina ya Tecno ambayo niliitumia kuwasiliana na mshtakiwa,” alidai binti huyo.

Alidai Machi, 2020 shule zilifungwa kutokana na ugonjwa wa corona, ndipo aliamua kwenda kwa mama yake Kijichi.

Alidai ilipofika Juni 25, 2020 shule zilifunguliwa mama yake alimweleza aende kwa baba yake kwa ajili ya kuendelea na masomo, lakini mtoto huyo alikataa na mama yake alimchapa, akakasirika na kutoroka nyumbani ambapo alimpigia simu mshtakiwa ambaye alimwelekeza wakutane kwenye baa ya Kibeta iliyopo Kijichi.

“Nilipofika alininunulia chipsi mayai na bia moja aina ya Savanah, kabla ya siku hii kukutana mshtakiwa alikuwa ananipigia simu na kunieleza amenivumilia sana anataka kufanya mapenzi na mimi,” alidai.

Alisema baada ya kumaliza Savanah moja mshtakiwa alimchukua na kumpeleka kwenye chumba kilichopo karibu na baa hiyo ambapo ndani kulikuwa sabufa (redio), pazia, kitanda na zulia.

“Wakati huo sabufa ilikuwa imewashwa na ilikuwa inawaka taa za rangi ya bluu ndipo mshtakiwa huyo alinivua nguo na kuanza kunibaka na kunisababishia maumivu makali, baada ya kumaliza alinitoa nje ya chumba na kunieleza nimsubiri hapo katika benchi anarudi,” alidai.

Alidai kuwa ilikuwa ni usiku mshtakiwa aliingia ndani ya baa na kumletea Savanah nyingine mbili na kumueleza aendelee kunywa anakuja akaondoka, lakini hakurudi hadi baa na maduka jirani yote yakafungwa.

“Wakati nikiwa nimekaa peke yangu akaja kijana aliyejitambulisha kwa jina la Zungu ambaye na yeye ana kesi ya kunibaka mimi kwa hakimu mwingine. Aliniuliza ‘Hapa unamsubiri nani?’ Nikamjibu namsubiri Godbless yupo ndani ya baa ya Kibeta akaniambia hawezi kuja kwa kuwa baa imefungwa na hakuna mtu.

“Akaniambia niende naye nyumbani kwake nikalale, nikakataa, akanihakikishia hatanifanya kitu kibaya, mimi nitalala katika godoro na yeye atalala chini, tulipofika kweli nililala kitandani na Zungu akalala chini ila cha kushangaza nilipoamka asubuhi nilijikuta sina nguo na pembeni alikuwa kijana huyo amelala huku naye akiwa hana nguo na nilipoangalia sehemu za siri nilikuwa zimeingiliwa,” alidai.

Alidai Zungu alimuomba msamaha na kutaka kumlipa Sh 30,000 lakini alizikataa. Alidai wakiwa njiani kuelekea kituoni Zungu alikutana na dada aliyemtaja kwa jina moja la Zulfa wakasalimiana huku wakitaniana, ambapo baadaye alimuomba dada huyo aishi naye kwa sababu hakuwa na pa kuishi, alimchukua na kwenda kuishi naye Mbagala

“Wakati naishi na Zulfa nilimtafuta Godbless nikampata na tukaendelea na mahusiano bila ya Zulfa kujua,” alidai mtoto huyo.

Alidai Agosti 30, 2020 Zulfa alimweleza kodi imeisha na hana uwezo wa kulipa hivyo anarudi nyumbani kwao Kijichi, ikabidi waende wote, mama yake akapata taarifa na kwenda kumchukua.

Baada ya kurudi nyumbani alimwelezea yote aliyopitia, ndipo mama yake alienda kutoa taarifa polisi akapewa Fomu ya Polisi ya Matibabu (PF3). Baada ya kuchukuliwa fomu hiyo alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke kwa ajili ya vipimo ambavyo vilionesha ameingiliwa na kwamba alikuwa na maambukizi ya Ukimwi.

“Naendelea kunywa dawa za kurefusha maisha nachukulia Hospitali ya Temeke na mara ya mwisho nilichukuwa Machi 3 mwaka huu,” alidai mtoto huyo.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 27, mwaka huu.

Advertisement