Simulizi madai kujeruhiwa na bastola

Friday May 20 2022
Simuluzi pc
By Berdina Majinge

Iringa. Wakati Jeshi la Polisi Mkoani Iringa likimshikilia Mkurugenzi wa Shule ya Sun Academy, Nguvu Chengula (50) kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi Alifan Mkwawa (35) kwa kutumia kitako cha bastola baada ya kufika shuleni hapo kuomba uhamisho wa mtoto wake, mkewe, Prisca Kimaro amesimulia ilivyokuwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Allan Bukumbi tukio hilo lilitokea juzi shuleni hapo, mtaa wa Mawelewele Kata ya Mwangata Manispaa ya Iringa.

Bukumbi alisema mtuhumiwa Chengula akiwa ofisini kwake alimshambulia Alifan Mkwawa, maarufu kama Wilbert, mjasiriamali mkazi wa Isakalilo kwa kutumia kitako cha bastola aina ya Canik 55 anayoimiliki kihalali na kumjeruhi kichwani.

Simulizi pcc

“Mlalamikaji alijeruhiwa wakati alipokuwa ameenda na mwenza wake, Prisca Kimaro kwa nia ya kuomba uhamisho wa mtoto wao Leonard Wilbert Mkwawa (6) mwanafunzi wa darasa la pili shuleni hapo,” alisema.


Advertisement

Ilivyokuwa...

Akisimulia ilivyokuwa, Prisca ambaye ni mke wa mhanga na mzazi wa Leonard Mkwawa alisema awali yeye ndiye alifika shuleni hapo kwa ajili ya kuomba uhamisho kabla ya mumewe.

Aliamua kumhamisha mwanaye baada ya kile alichokieleza kuwa, shule zilipofunguliwa Aprili 2022 mtoto wao alilazimika kutembea kwa miguu kutoka shuleni hapo hadi nyumbani kwao Isakalilo kutokana na wazazi kutofanya malipo ya usafiri wa shule (school bus).

Alisema hilo liliwafanya kukwazika na kuamua kudai uhamisho, lakini alipofika shuleni hapo kujua utaratibu ndipo usumbufu ulianza.

“Nilipokwenda niliambiwa nimuone mhasibu, akaniambia kama nataka kumhamisha mtoto natakiwa nilipie ada ya Aprili ambayo ni Sh75,000, hivyo nikija tena nilete hiyo pesa, picha ndogo (passport) mbili na Sh2,000 ya kadi ya uhamisho,” anasimulia Prisca.

Alisema kwa wakati huo hakuwa na pesa hivyo alirudi nyumbani na Jumatatu wiki hii alirudi tena baada ya kupata alivyoagizwa.

“Nilivyofika shuleni nilikwenda kumuona mhasibu nikalipia ili nipewe uhamisho, lakini alikuja Mkuu wa shule na kumuelekeza mhasibu kuwa kuna utaratibu mpya ambao Mkurugenzi wa shule ameuanzisha, ambao mzazi anapaswa kulipa hela zaidi ya aliyoambiwa,” alisema na kuongeza:

“Lakini nililipa ile pesa, nikapewa risiti nikaambiwa niende kumuona mkuu wa shule, baada ya kufika kwake aliniambia amenyang’anywa jukumu hilo na sasa linashughulikiwa na mkurugenzi mwenyewe, natakiwa nikamuone na kuna utaratibu mpya ameuanzisha.

Alisema alipofika kwa mkurugenzi wa shule ambaye ni Nguvu Chengula alimpatia risiti, lakini alimuambia bado anadaiwa huku akielezwa utaratibu mpya unaomtaka alipie ada hadi ya Juni.

Alieleza kuwa hilo lilimfanya kuhoji, kwa nini alipie ada ya miezi mitatu ambayo mtoto hatokuwapo shuleni? Lakini alijibiwa kuwa ni utaratibu na baada ya kutoridhika na majibu alihoji tena kuwa hawaoni kufanya hivyo ni kutomtendea haki.

“Alinijibu siwezi kumpangia kwa sababu yeye ndiyo mmiliki wa shule na utaratibu huo hauwezi kubadilika.

“Baada ya malumbano hayo mama wa mtoto alisema hawezi kukubali aonewe na kuomba arudishiwe pesa yake aliyotoa kwa ajili ya malipo ya Aprili ambayo pia ameilipa bure, kwani tayari mtoto anasoma shule nyingine.

Lakini Mkurugenzi huyo alisema pesa haiwezi kurudishwa, kwani imeshaingia kwenye mfumo na uhamisho haupo, huku akiita mlinzi na kuamuru amuondoe kwa nguvu.

“Baada ya mlinzi kufika alinipiga na kuninyanyua kwa nguvu na kunitupa nje ya ofisi, tena mbele ya wanafunzi, nikampigia mume wangu kumueleza kilichotokea, alifika shuleni bila kuchelewa.”


Dada wa Mkwawa atoa neno

Dada wa Mkwawa, Shauri Mkwawa alisema familia yake imesikitishwa na kitendo hicho, huku akieleza kuwa kuhamisha mtoto ni haki yake.

“Mdogo wangu hajawahi kuwa na ugomvi na mkurugenzi wala mwalimu yeyote pale shuleni, lakini tumeshangaa uhamisho umeleta fujo hadi kufikia kumpiga ndugu yetu hadi kumuumiza kiasi kile, inashangaza.

“Haieleweki kama alikusudia au ni bahati mbaya, lakini mpaka mtu anafikia hatua ya kutafuta silaha na kumpiga nayo mtu labda alijiandaa kufanya hivyo,” alisema Shauri.

Mtuhumiwa huyo amekamatwa pamoja na kielelezo cha bastola ambayo imehifadhiwa kituoni, upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Advertisement