Prime
Simulizi maisha ya mwalimu Yufresh ilivyojaa matumaini, mikasa

Hayo ni maneno ya Yusuph Ibrahim (32), mwalimu wa shule ya msingi Kisuma iliyopo Kata ya Nyaminyusi, halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Vijijini, mkoani Kigoma.
Kama kuna watu wanatambua umuhimu wa taasisi ya familia, basi Yusuph atakuwa miongoni mwao, kwa kuwa anaamini kila kinachoendelea kwenye maisha yake kwa sasa ni sababu ya msingi imara wa upendo uliojengwa ndani ya familia yake.
Wakati ndoa nyingi kwa sasa zikiwa kwenye migogoro na kila uchwao tunasikia taarifa za wenza kuuana, Yusuph kwake mambo ni tofauti, akieleza kuwa mwenza wake ndiye anayemfanya kuwa imara na furaha na kumuondolea kumbukumbu za ulemavu ambao hakuwa nao hapo awali.
Mwalimu huyu amejizolea umaarufu mkubwa mitandaoni kutokana na namna yake ya kujichanganya na wanafunzi, akicheza na kuimba nao kwa furaha ilhali anatumia magongo kwa sababu ya ulemavu alionao.
Si kwamba anacheza na watoto bila sababu, mwalimu huyo anafanya hivyo kama sehemu ya kampeni yake ya kutokomeza utoro na alianza kwenye shule yake, kabla ya kuanza kupata mialiko ya kwenda kwenye shule za jirani na hatimaye katika wilaya nzima ya Kasulu Vijijini.
Yusuph, ambaye kwa wengi anajulikana kama mwalimu Yufresh, alikatwa mguu mwaka 2021 baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na uvimbe kwenye goti na kusababisha mambo yake mengi kwenda kombo.
“Sikuwahi kuwa na tatizo lolote kabla, mfumo wangu wa kufundisha unahusisha kucheza na watoto kama ambavyo naonekana sasa, hata wakati huo nikiwa mzima na miguu yangu miwili nilikuwa navutiwa zaidi ninapocheza na wanafunzi wangu, hilo limekuwa likisaidia wawe karibu na mimi na waelewe masomo ninayofundisha.
“Siku moja nikiwa shuleni nakumbuka ilikuwa mwaka 2017, kama kawaida nacheza na wanafunzi nikapata maumivu makali kwenye mguu, ikabidi nisitishe kucheza, yale maumivu yaliendelea kwa muda mrefu hadi nilipokuja kugunduliwa kuwa nina uvimbe mkubwa kwenye goti”.
Wakati huo alikuwa akifundisha kwenye shule binafsi jijini Dar es Salaam, mwajiri wake alimsaidia kupata matibabu ya awali lakini haikufua dafu, uvimbe ukazidi kumea na kumea, uwezo wake kwenye kazi ukapungua, ikafika muda akalazimika kukaa nyumbani.
Hali hiyo ya ugonjwa iliyodumu kwa takribani miaka minne iligharimu ajira yake, akajikuta amepoteza kazi akabaki nyumbani akijiuguza.
Baada ya muda alipata nafuu na akaitwa kufundisha katika shule nyingine ya binafsi mkoani Mbeya, akiwa huko ugonjwa ukamrudia tena na akatakiwa kufanyiwa upasuaji ili kuondoa uvimbe huo ambao ulianza kuharibu mifupa yake ya goti.
Si kwamba mguu wake ulikuwa umefikia hatua ya kukatwa, alitakiwa kulipia Sh4 milioni ili aondolewe uvimbe huo ambao awali ulitolewa kwa upasuaji mkubwa, kutokana na hali ya maisha yake akaona hawezi kumudu kiasi hicho cha fedha ilhali hana uhakika na uvimbe huo kuondoka moja kwa moja, hivyo akaamua ni heri akatwe.
“Nilifikiria namna mke wangu anavyohangaika na mimi, akinionesha kila aina ya kujali kwa mateso ninayopitia kutokana na maumivu makali niliyokuwa nayapata, maana ilikuwa ni lazima nimeze dawa kila siku, nikamwambia ni heri nikatwe huo mguu.
“Sikutegemea mwitikio wake katika hili, kwa upendo na unyenyekevu mkubwa akaniambia kama umeamua hivyo hakuna shida Mungu atatuongoza na maisha yataendelea, niliumia umaskini unasababisha nipoteze kiungo changu lakini imani aliyoonesha mke wangu ikanipa ujasiri,” anasema Yusuph.
Kauli hiyo ya mkewe ilimpa faraja ya hali ya juu na hakutaka kupoteza muda, akaweka saini kwenye fomu za kuruhusu akatwe mguu huo mkewe akiwa shahidi.
Aliingia kwenye chumba cha upasuaji akiwa hajui nini hatima ya maisha ya familia yake, lakini maneno ya faraja na matumaini aliyokuwa akipata kutoka kwa mkewe yalimfanya apige moyo konde.
Hata mara baada ya kukamilika upasuaji, Yusuph anasema mkewe aliendelea kuwa naye bega kwa bega, aliongeza upendo na unyenyekevu maradufu.
“Kama binadamu kuna wakati unaweza ukawa unafikiria mambo hasi, mke wangu hakunipa hiyo nafasi, yani hadi sasa sijaona tofauti yoyote kana kwamba hakuna kitu ambacho kimetokea kwenye maisha yangu. Nakumbuka tu mtoto wangu alikuwa akiniuliza maswali sasa baba itakuwaje, utafundishaje, nikawa namjibu nitafundisha tu maana nimeshaona watu wenye ulemavu na maisha yao yanaendelea kama kawaida.
“Nimepitia kukatishwa tamaa na watu wangu wa karibu, wengi waliamini baada ya kukatwa mguu ualimu ndio basi na wapo ambao walikuwa wanajaribu kumshawishi mke wangu aniache, lakini hakuyapa nafasi maneno yao hadi sasa familia yetu ina furaha mno”.
Furaha ya Yusuph inathibitishwa na mkewe, Rosina Maro, mwenyewe anakiri kuwa upendo na ujasiri aliomuonesha mumewe ndiyo unamfanya awe na furaha licha ya kupata ulemavu katika safari ya maisha yake.
Rozina ambaye alifunga ndoa na Yusuph miezi miwili kabla ya mwalimu huyo kukatwa mguu, anasema upendo, amani na mshikamano ndiyo nguzo inayowafanya waendelee kuwa na furaha, licha ya changamoto waliyopitia muda mfupi baada ya kuingia rasmi kwenye ndoa.
Anasema msingi imara walioujenga wakati wa maisha waliyoishi katika miaka zaidi ya mitano ya uhusiano kabla ya ndoa yalimfanya ausikilize zaidi moyo wakati wa kipindi kigumu cha mume wake kukatwa mguu.
“Ni kweli tumepitia kipindi kigumu cha kuhangaika na huo mguu, hata siku aliponiambia kwamba anataka akatwe nilijawa na ujasiri wa kumkubalia nikiamini ndiyo tiba ambayo anastahili kupata. Kibinadamu hofu lazima iwepo kwamba maisha yatakuwaje, lakini hilo halikunirudisha nyuma.
“Kama niliishia naye kwa upendo na furaha wakati akiwa mzima na miguu yake miwili kwa nini nibadilike baada ya mwenzangu kupata changamoto? Moyo wangu uliniambia kwamba huyo ndiye mwanaume ambaye Mungu amekupa hivyo napaswa kuendelea kuwa naye kwenye shida na raha,” anasema.
Kuhusu anachokifanya mumewe na kumpa umaarufu mitandaoni, Rozina anasema hana tatizo nacho kwa kuwa ni kitu ambacho anaona kinampa furaha na siku zote amekuwa akimuunga mkono kwa kuwa anafurahi kumuona mume wake akifurahi.
Amani na faraja anayopata nyumbani ndiyo ikamfanya Yusuph kuyakubali maisha yake mapya kwa haraka na kuwa mbunifu katika kazi yake. Mara baada ya kukatwa mguu hakutaka kuacha kazi yake, akatafuta msaada wa mguu bandia uliomwezesha kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
“Mguu nilikatwa nikiwa kwenye shule moja ya binafsi kule Mbeya, kwa bahati nilipata mguu wa bandia, maisha mapya yakaanza, sikuwahi kujutia wala kumlalamikia Mungu kwa sababu niliamini ana kusudi lake na hivyo ndivyo ilivyokuwa, mwaka uliofuata nikapata ajira serikalini.”
Ajira hiyo ikamlazimu kuhama kutoka Mbeya hadi Kigoma katika halmashauri ya Kasulu vijijini, mke wake akaendelea kumpa moyo na wote wakakubaliana aripoti kwenye kituo hicho alichopangiwa.
“Nilipofika halmashauri nikiwa nimevaa mguu wa bandia, hakuna aliyejua kama ni mlemavu, hivyo nikapangiwa shule moja iko milimani, ikabidi nizungumze na anayepanga na nilipomuonesha mguu wangu ikabidi anibadilishie na kunipangia shule ambayo angalau ina mazingira rafiki.
“Nilipata mapokezi mazuri katika shule niliyopangiwa kuanzia kwa walimu hadi wanafunzi, lakini katika siku chache nilizoanza kazi nikabaini kuna tatizo kubwa la utoro, watoto wengi wanakacha masomo na kushinda mashambani”.
Hali hiyo haikumpendeza Yusuph, akamshirikisha mkewe kwamba anatamani kuona mabadiliko na kwa haraka akafikiria kuanza kutengeneza ukaribu na wanafunzi ili kuwaondoa hofu waliyonayo dhidi ya shule na walimu kwa ujumla.
Anasema, “Kama ilivyo kawaida yake mke wangu nilipomshirikisha akaniunga mkono na kuniambia ni kitu kizuri, tukakubaliana iwe kampeni ya kutokomeza utoro, nikaanzisha mchakamchaka na vipindi vya nyimbo za hamasa kwa wanafunzi, hasa tunapokuwa mstarini. Watoto wakaanza kuvutiwa na shule wakiamini kupata burudani hiyo ni lazima uwe unakuja shuleni, taratibu mahudhurio yakaanza kuongezeka.”
Habari zikavuma, shule jirani zikavutiwa na anachofanya mwalimu huyu, akaanza kualikwa kwenda kuwachangamsha wanafunzi wa shule nyingine na hapo ndipo jina la Yusuph likashika hatamu katika halmashari ya Kasulu vijijini, sasa kila anakopita anafahamika kama mwalimu Yufresh.
Kampeni yake haikuishia kwenye kuimba na kucheza na wanafunzi, alianza kutafuta mahitaji muhimu, ikiwemo viatu, madaftari na sare za shule kwa watoto wanaotoka kwenye familia duni ili kuwapa hamasa ya kwenda shuleni.
“Ninachokifanya huwa kinawavutia watu wengi wanaoniona mtandaoni, wapo wanaoguswa na kunitumia pesa, sasa kila nikiangalia kuna watoto wenye uhitaji huwa naishia kuzitumia pesa hizo kujaribu kupunguza changamoto zao. Mfano huwa nina utaratibu wa kununua mashati, nashona kaptura na sketi halafu nikienda kwenye shule nauliza kama kuna wanafunzi ambao wanaenda shuleni bila kuwa na sare nawapatia.
Huku ni kijijini, hakuna mwamko wa elimu, sasa ikitokea kuna mtoto ana nia ya kusoma lakini hana mahitaji muhimu kwa nini tusimsaidie huyu ili apate elimu, hivyo ndivyo nafanya, nashukuru kuna watu wengi wanaguswa kwa namna moja au nyingine kunishika mkono,” anasema.
Palipo na mafanikio hapakosi changamoto, hata Yusuph naye yapo magumu anayokutana nayo, mojawapo ni maumivu makali anayopata wakati akicheza na watoto kwa msaada wa magongo.
"Kucheza na magongo napata maumivu, kwa sasa nahitaji mguu bandia, niliowahi kuwa nao haunifai tena, kwani umenisababishia vidonda, daktari wangu ameniambia ule ulikuwa wa awali, hivyo nahitaji ambao teknolojia yake iko juu kidogo, nasikia gharama yake ni kati ya Sh5 milioni hadi Sh6 milioni.
"Changamoto nyingine niliyonayo ni kukosa usafiri, nalazimika kutumia bodaboda kufika katika hizo shule ambazo naenda kueneza kampeni ya kutokomeza utoro, kuna siku nilianguka kwenye pikipiki. Natamani ningepata angalau bajaji inisaidie kutoka eneo moja kwenda lingine".