Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi usiyoijua kuhusu huduma ya ganzi wakati wa upasuaji nchini

Mtaalamu wa tiba ya usinginzi na kuondoa maumivu, Balozi Mpoki Ulisubisya (kulia) akimweleza Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile kuhusu mashine mpya ya tiba ya usingizi wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).

Na Mpigapicha maalumu

Muktasari:

  • Kama Rais wa Chama cha Waanaesthesia wa Tanzania (Sata) na mwanadiplomasia, aliungana na jumuiya ya Muhas na viongozi wa juu serikalini kuzindua maabara hiyo iliyofadhiliwa na kampuni ya teknolojia ya Marekani ya Gradian Health Systems kwa lengo la kuimarisha utaalamu wa anaesthesia nchini.

Dar es Salaam. Dk Mpoki Ulisubisya ni kati ya madaktari wa kwanza kupata elimu ya utaalamu wa kuweka ganzi kabla ya operesheni (anaesthesia), ambaye kwa miaka kadhaa ameshuhudia kupanda na kushuka kwa fani hiyo nchini.

Kabla ya kutoa mhadhara mbele ya wataalamu wa afya hivi karibuni jijini Dar es Salaam, kuhusu anaesthesia, wataalamu hao walitulia kimya kusubiri hotuba yake. Ungeweza hata kusikia sauti ya pini inayodondoka.

Akitumia uzoefu wake wa kuhutubia mbele ya hadhara, alizungumza kwa msisitizo akisema, “habari hii lazima isimuliwe…” huku akifafanua kwa undani kuhusu takwimu za kushtua kuhusu vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Dk Ulisubisya alieleza jinsi vifo hivyo vinavyohusiana na hali ya utoaji huduma ya anaesthesia, hasa alipokuwa akilinganisha na hali ilivyo kwa Afrika na duniani kwa jumla.

Mtaalamu huyo alizungumza katika siku ambayo Tanzania ilikuwa ikizindua maabara ya kwanza ya mafunzo ya anaesthesia, tukio lililofanyika Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Muhas).

Kama Rais wa Chama cha Waanaesthesia wa Tanzania (Sata) na mwanadiplomasia, aliungana na jumuiya ya Muhas na viongozi wa juu serikalini kuzindua maabara hiyo iliyofadhiliwa na kampuni ya teknolojia ya Marekani ya Gradian Health Systems kwa lengo la kuimarisha utaalamu wa anaesthesia nchini.

Ndani ya chumba cha upasuaji

Dk Ulisubisya alikumbusha kisa chenye sintofahamu akiwa chumba cha upasuaji katika hospitali kijijini ambako kwa miaka kadhaa, wataalamu wa afya hawakuwahi kuona dawa muhimu ya kuondoa maumivu inayojulikana kama pethidine.

Katika hospitali hiyo, uamuzi juu ya tiba gani itumike hata katika michakato migumu kama upasuaji zinategema uwepo au kutokuwepo kwa dawa, na si viwango.

Akiwa mtaalamu aliyesafiri muda mwingi, Dk Ulisubisya anakumbuka siku ambayo alipelekwa kwenye kituo cha afya kilichopo Kusini mwa Tanzania, safari ambayo ilimuonyesha jinsi huduma ya anaesthesia ilivyo nchini.

“Nilipata nafasi ya kusafiri kwa ndege ya Amref kwenda Nachingwea,” anasema. “Nilikuwa na rafiki yangu naye mtaalamu. Tulipofika tuliangalia wagonjwa na kuamua wanaofaa kufanyiwa upasuaji.

“Nikiwa nimeshafanya kazi katika Hospitali ya Taifa, nilitarajia angalau huduma za msingi zingekuwepo, kwa hiyo wakati wa operesheni niligundua mgonjwa alihitaji dawa ya kutuliza maumivu (pethidine), kwa sababu wakati huo nyama zilikuwa zinakatwa na kungekuwa na maumivu makali.”

Anasema, “nilimwambia mpasuaji, tusubiri kwanza hizo dawa ziletwe. Nusu saa ilipita bila kuletwa dawa hiyo, hakukuwa na pethidine hadi baada ya dakika 45. Nikagundua kuwa tulikuwa na muda mfupi kwani tulitakiwa turudi tena tulikotoka kwa ndege.”

“Nilimwambia mpasuaji (anamtaja jina), tafadhali endelea na upasuaji, akitumia Ketamine, kisha operesheni ikakamilika. Hapakuwa na pethidine.

“Saa nne baadaye, ndipo mtu mmoja anakuja kuniambia kwamba, unajua, kusema kweli, ni miaka sita tangu tuione dawa uliyoiomba.”

“Sasa huwa mnafanyaje?” aliuliza Dk Ulisubisya na alijibiwa, “huwa tunawapa wagonjwa dawa ya diazepam.”

Akiwa amebaki na mshangao, alisema, “sikuwahi kujifunza katika mafunzo ya anaesthesia kuwa diazepam inafaa “kwenye huduma za upasuaji lakini kwa mazingira yale, ndivyo ilivyotokea, suala la mafunzo ya kitaalamu bado kuna safari ndefu.”

Lakini, kwa ushauri wake, njia bora ya kuhakikisha huduma za afya ni bora, ni kuwa na mambo muhimu matatu--miundombinu, vifaa vya afya na wafanyakazi wa afya.

“Ninachotaka kusema hapa ni kwamba hakuna mfumo ulio imara bila kuwa na mipango inayotekelezeka ili kuhakikisha mfumo mzima unafanikiwa. Ndiyo maana tunasema wataalamu ni lazima wafundishwe vizuri na vya kutosha,” alisema.

Dk Ulisubisya anasema hali hiyo inahusishwa na kiwango kikubwa cha vifo vya kina mama wajawazito na watoto, kulingana na utafiti na ushahidi wa utendaji ambao yeye aliuona akiwa kiongozi wa Wizara ya Afya.

Kutokana na idadi kubwa ya watu na changamoto za kijiografia pamoja na kutokuwepo kwa huduma za msingi za afya, Kanda ya Ziwa imekuwa ikitajwa kuongoza katika vifo vya akina mama wajawazito kuliko sehemu nyingine za nchi.

“Nilikuwa pia na nafasi ya kutembelea Kanda ya Ziwa. Tulikuwa tunafikiria kuanzisha vituo vya afya vya dharura, kwa hiyo kazi yangu ilikuwa ni kutathimi mkoa wa Kagera, hivyo nilikwenda Bukoba,” alisema.

“(Baada ya kufika) nilimuuliza mganga mkuu wa wilaya kama kulikuwa na kituo kinachotoa huduma hiyo ya dharur, naye alijibu akisema hakuna, bora uende Ndolage, wanacho kimoja.”

“Kwa hiyo tuliendesha gari hadi Kamachumu (Bukoba). Tukiwa hapo, niliomba kwenda chumba cha uangalizi maalum (ICU) na nikapelekwa kwenye chumba kilichotajwa kwa kazi hiyo. “Unajua niliona nini pale? Wagonjwa watano mtambo wa oxygen na sehemu tatu za kutolea zikiwa zimegawanywa kwa wagonjwa watatu na unaona mgonjwa mmoja akitosheka na oxygen, mtambo unapelekwa kwa mgonjwa mwingine,” anasema.

Hali ikoje Tanzania

Dk Ulisubisya anasema tatizo hilo ni changamoto kwa kinamama wakati wa kujifungua.

“(Hata hivyo), kwa sababu ya jitihada mbalimbali, idadi ya wanawake wanaofariki nchini inaweza kupungua…hii ni kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na wanaume na wanawake katika fani hii walioamua kubeba mzigo huu kuhakikisha huduma bora zinatolewa,” anasema.

“Nilipokuwa nafanya kazi Wizara ya Afya nilifuatilia (vifo vya wanawake). Tukajiuliza wanawake wangapi wanaofariki kutokana na hali ya vituo vya afya kila mwezi na kila wiki? Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kutaja idadi kamili lakini tunapoteza wanawake kila mwezi nchini.”

“Nina uhakika kuwa jitihada zinazofanywa na Serikali zimewezesha kuboresha vituo vya afya, kwa hiyo idadi itapungua.”