Simulizi ya safari ya maisha waliofunga ndoa uzeeni (2)

Muktasari:
- Jana tulianza simulizi ya wanandoa Dk Christian Kiwia na Christina Teemba, namna walivyofikia uamuzi wa kufunga ndoa na safari ya maisha ambayo kila mmoja amepitia. Endelea...
Dar es Salaam. Jana tulianza simulizi ya wanandoa Dk Christian Kiwia na Christina Teemba, namna walivyofikia uamuzi wa kufunga ndoa na safari ya maisha ambayo kila mmoja amepitia. Endelea...
Unaweza kujiuliza kwa nini wawili hawa wasifunge ndoa ya kimyakimya kama wafanyavyo watu wazima wengi.
Kwa mujibu wa Dk Kiwia, hawakuona sababu ya kufanya hivyo, kwa kuwa hakukuwa na kitu cha kuficha. Ni vema dunia nzima ikafahamu kuwa amepata mwenza.
“Alipofariki mke wangu kila mtu alijua, ibada yake iliongozwa na Askofu Mkuu wa TAG, maaskofu na wachungaji wengi walikuja kwenye mazishi. Sasa iweje ninapopata mke iwe siri?
“Hakuna cha siri na bahati nzuri tumekutana na mwenzangu wote tunapenda kuchangamana na watu wa hali zote. Hatubagui tajiri wala maskini,” anasema.
Kutokana na hilo, hata sherehe ya harusi yao haikuwa na kadi ya mwaliko wala mchango, ilifanyika eneo la wazi nje ya kanisa, ili kila aliyetaka kushiriki afanye hivyo bila kikwazo. Kama taratibu za kanisa zinavyoelekeza baada ya wawili hao kukubaliana walikwenda kupima afya zao na kujikuta wako salama na kuingia hatua mpya zaidi.
“Sikutaka kuruka hatua yoyote, tulipima afya zetu kuhakikisha tuko safi, ndipo tulipoanza taratibu za kwenda kwenye jamii, kupeleka posa, tukakaa kikao cha mahari na hatimaye tukaingia rasmi kwenye uchumba na nilimvalisha pete ya uchumba,” anasema Dk Kiwia.
Maisha yake na mkewe wa kwanza
Dk Kiwia anasema ndoa yake ya kwanza iliyodumu kwa miaka 48 ilikuwa na furaha kutokana na mwanamke ambaye Mungu alimpatia kabla ya kuamua tofauti.
“Niliishi na mke wangu kwa miaka 48 na miezi saba kabla ya Mungu kumtwaa. Rachel Kiwia alikuwa mwanamke mwaminifu na mtiifu.
“Naweza kusema alikuwa jasiri, maana kuishi na Dk Kiwia unaweza kupewa shahada, ‘am tough’, wakati nasoma nilitamani kuwa jaji, ila roho mtakatifu akanipeleka kwenye kumtumikia Mungu,” anasema na kuongeza:
“Mama yule alikuwa na moyo wa kumcha Mungu, hana kelele. Ukimwambia kitu hakijamuingia ananyamaza kimya. Tumefanya huduma pamoja katika maeneo mengi nchini.”
Huduma ya neno la Mungu kwa wawili hao haikuishia nchini, walizuru mataifa mbalimbali kuhubiri na hatimaye kuweka makazi nchini Marekani. Huko walijenga nyumba, walinunua shamba na maisha ya kuhubiri injili yakaendelea, huku Dk Kiwia akifundisha wachungaji katika vyuo mbalimbali.
“Tulihubiri injili katika majimbo 11 ya Marekani na tulikwenda pamoja mataifa 10, huku mimi nikisafiri katika mataifa 14 kote huko ni kufanya huduma ya Mungu,” anaeleza.
Anasema pamoja na kuwekeza huko bado alichagua Tanzania ndio sehemu angemzika mkewe baada ya kufikwa na umauti kutokana na kuugua kwa muda mrefu.
Safari ya ndoa kati ya Dk Kiwia na Rachel ikahitimishwa Agosti 3, mwaka jana na ikawa pigo kwa mchungaji huyo kupata msiba akiwa peke yake ughaibuni. Dk Kiwia anasema haikuwa rahisi kwake kutokana na gharama za kusafirisha mwili, lakini kutokana na mapenzi aliyokuwa nayo kwa mkewe akapiga moyo konde na kuwa tayari kwa lolote.
“Ukipata msiba ughaibuni hususani Marekani ni kitu kigumu, kwanza hata majirani hawana taarifa, utalia mwenyewe hakuna huo utamaduni. Pili gharama za kusafirisha ni kubwa si chini ya Sh30 milioni ila nikasema lazima hili lifanikiwe na kwa msaada wa Mungu nikafanikisha kumzika mke wangu nyumbani Moshi,” anasema.
Hata hivyo, Dk Kiwia anasema amekubaliana na kazi ya Mungu na kumhakikishia mkewe mpya kuwa hajachukua nafasi ya mtu, amekwenda kwake kwa kusudi maalumu la Mungu.
“Nakwambia mke wangu kwamba wewe hujachukua nafasi ya mtu, sijakuoa kama mbadala, aliyekuwepo alikuwepo kwa wakati na mpango wa Mungu tangu alipoanzia hadi alipoishia.
“Na wewe unapoanza na mimi unakuja si kwamba, unachukua nafasi ya mtu bali unakuja kwa wakati wako na mipango ya Mungu. Sitakulinganisha na aliyekuwepo na utabaki kuwa wa kipekee kwangu”.
Maisha mapya Tanzania
Kabla ya kupatwa na msiba, Dk Kiwia na mkewe walikuwa na mpango wa muda mrefu wa kurejea nchini, lengo likiwa kufundisha neno la Mungu na kuwaandaa wachungaji.
Kwa kutambua hilo mwaka 2015 wakaanza kurudisha nguvu Tanzania na mwaka 2017 Askofu Kiongozi wa TAG alimuomba aje kusimamia Kanisa la Pugu Kajiungeni, huku akiendelea kuhudumu kwa njia ya kufundisha.
“Nilirudi nchini lakini mke wangu akaendelea kubaki Marekani, nikawa nakwenda na kurudi, lakini hapa kanisani hawakuwahi kumuona mama mchungaji.
“Sasa ilivyotokea amefariki nikaona ugumu wa kuanza upya na ikizingatiwa shughuli za uchungaji ni muhimu kuwa na mama mchungaji, hapo ndipo wazo la kuoa lilipokuja,” anasimulia Dk Kiwia.
Kilichowaunganisha Dk Kiwia, Christina
Pamoja na kuguswa na stori ya Christina kuwa kanisani kwa miaka mingi bila kuolewa wala kuzaa, yapo mambo mawili yaliyowafanya wawili hawa waungane.
Kwanza safari zao za wokovu zilifanana, wote walipata changamoto kutoka kwa wazazi na familia baada ya kueleza kuwa wameokoka.
“Miaka hiyo ya 60 hadi 70 kule uchagani suala la ulokole halikuwepo. Ni uwe Mkatoliki au Mlutheri, tuliogeukia upande mwingine tulionekana tumekengeuka. Wazazi hawakutuelewa.
“Wote tulipata shida kwenye familia zetu, sasa baada ya kukaa chini na Christina na kunisimulia stori yake akanieleza kuwa wakati huo alipata faraja kutoka kwa msichana mwenzake aitwaye Belta,” anasema na kuongeza: “Na mimi baada ya kuokoka nilimshuhudia kijana mwenzangu akaokoka, yaani tunda langu la kwanza la kiroho aliiitwa Charles Moshi. Kilichonishangaza huyo Charles na Belta baadaye wakaja wakaoana, hadi sasa wapo wanandoa”.
Maisha ya Christina kabla ya ndoa
Bibi huyu alifanya kazi katika taasisi mbalimbali, lakini baada ya kuona hapati kile anachostahili akaamua kuacha kazi na kujikita kumuangalia mama yake, ambaye kwa sasa ni mgonjwa.
Wakati wote huo bado alikuwa muumini mwaminifu kanisani, ndipo mchungaji alipomuomba kufanya kazi kanisani upande wa kitengo cha fedha. Christina alikubali jukumu hilo na kulifanya kwa ufanisi mkubwa kiasi cha kulifanya kanisa kuwa miongoni mwa yaliyofanya makubwa mjini Moshi.
Hilo linamgusa mumewe: “Huyu mama ni mwaminifu, amefanya makubwa pale kanisani kwao wamejenga jengo la ghorofa nne, wakati yeye hana chochote. Ni kweli aliamua kumtumikia Mungu,” anasema Dk Kiwia. Christina anaeleza kuwa akili yake ilikuwa ni kwa mama yake na Mungu wake ndiyo maana hakuhangaika na kitu kingine wala kutamani kumiliki mali. “Kuna baadhi ya watu waliona kama nimechanganyikiwa ila mimi nilikuwa na amani kwa kuwa niko ndani ya Yesu. Kwangu ilikuwa faraja kumhudumia mama yangu, ila kwa sasa jukumu hilo limebaki kwa wadogo zangu wengine”.
Mwananchi inawatakia heri katika maisha mapya na Mungu akawabariki.
Kwa maoni na ushauri kuhusu habari hii tuandikie kupitia 0658376444