Sindano za ganzi zinavyoua wanasoka

Muktasari:
Mwananchi imeongea na wachezaji, madaktari wa timu na viongozi ambao wameeleza jinsi walivyoshuhudia au kufanyiwa au kusikia vitendo hivyo, ambao baadhi wanajuta kuweka rehani afya zao.
Dar es Salaam. Ni kawaida kusikia mchezaji ambaye yuko katikati ya kipindi cha kung’ara, akapata jeraha na baadaye kuonekana mara chache uwanjani kabla ya kupotea kabisa.
Baadhi wanaweza kuwa walipata jeraha kubwa na hawakulitibu vizuri na wengine kutoshughulikia vizuri matibabu baada ya kutibiwa na hivyo kutopona vizuri na kusababisha mchezaji atundike daruga.
Hii hufanyika kwa kulazimishwa na uongozi kuchoma sindano za kutuliza maumivu au za ganzi (anaesthetic) na hivyo kuweza kucheza, kumbe ndio anajiharibia maisha yake ya soka.
Mwananchi imeongea na wachezaji, madaktari wa timu na viongozi ambao wameeleza jinsi walivyoshuhudia au kufanyiwa au kusikia vitendo hivyo, ambao baadhi wanajuta kuweka rehani afya zao.
“Mara nyingi mambo haya hufanyika katika mechi ambazo zina upinzani mkali,” alisema nahodha wa zamani wa Simba, Seleman Matola.
Matola anasema endapo timu inakuwa na idadi kubwa ya majeruhi, hasa wachezaji tegemeo, klabu huamua kutumia sindano ya ganzi.
“Imewahi kunitokea,” alisema.
“Nilichoma sindano katika mechi tatu tofauti, zote za Yanga na Simba ili nicheze, lakini kilichonikuta baadaye sitakaa nisahau.”
Kocha huyo wa Lipuli ya Iringa na ambaye aliwahi kuchezea Supersport ya Afrika Kusini, anasema haikuwa mara hizo zote tatu hakuchomwa sindano kwa hiari yake, bali alilazimishwa kutokana na umuhimu wake katika timu na kama kiongozi ndani na nje ya uwanja, hivyo hakuweza kukataa.
“Nililazimishwa haikuwa kwa mapenzi yangu. Nilikuwa naumwa goti wakati nikiwa miongoni mwa wachezaji tegemeo. Kuna daktari anaitwa Mashaka yuko Arabuni ndiye alinichoma,” anakumbuka Matola.
Matola anasema anajuta kukubali kutumia sindano hizo.
“Nikiwa Afrika Kusini niliumia kifundo cha mguu katika mechi ya kwanza. Daktari aliyenitibu alisema baada ya wiki mbili nitakuwa sawa, lakini nikawa bado naumwa,” alisema.
Anasema daktari alipata hofu, hivyo alishauri uongozi umpeleke kwake kwa vipimo zaidi ndipo ikagundulika alikuwa na jeraha ambalo halikutibiwa vizuri kutokana na kutumia sindano ya ganzi.
Wakati wachezaji wengi wanachoma ganzi kutuliza maumivu ya majeraha ya miguuni, nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay anajuta kutumia sindano hiyo kwa jeraha la kichwani wakati akiichezea CDA ya Dodoma katika mechi dhidi ya Lipuli.
“Najuta kwanini nilifanya vile,” anakumbuka. “Lakini wachezaji wetu wanapaswa kuwa waangalifu na kuepuka mambo hayo. Katika timu zetu, haya yapo. Enzi zile nacheza Yanga yalikuwepo.”
Anasema alichoma sindano hiyo baada ya kupasuka kichwani na kushonwa nyuzi kadhaa na kuendelea na mchezo, lakini anasema baada ya mechi “nilipata maumivu makali”.
‘Sijui kama siku hizi yapo’
Pia kiungo wa zamani wa Pan Africans, Mohamed “Adolph” Rishard anaona kama vitendo hivyo vimepungua.
“Zamani mambo hayo yalikuwa yakifanyika, siku hizi sijui,” alisema Adolph.
“Lakini athari yake ni kubwa (kwa sababu) mchezaji anazidi kuumia. Wachezaji wanaokubali kupigwa sindano maisha yao kisoka yanakuwa mafupi mno.”
Madaktari walivyohusika
Nao madaktari hulazimika kuhakikisha wachezaji muhimu wanashiriki katika mechi muhimu, kama Nassor Matuzya anavyokumbuka jinsi alivyowachoma sindano za ganzi, Haruna Niyonzima na Hamisi Kiiza mwaka 2012.
“Wote walikuwa wanaumwa na vyombo vya habari viliripoti kuwa hawangewezi kucheza mechi dhidi ya Coastal Union halafu baadaye na Mgambo (zote za Tanga),” anasema Matuzya.
“Kiiza alikuwa anaumwa ankle (kifundo cha mguu), Niyonzima alikuwa na jipu puani. Lakini vyote vilidhibitiwa na walicheza na ndiyo walitupa ushindi wa bao 1-0, pasi ya Niyonzima akafunga Kiiza,” anasema Matuzya.
Lakini anasema mchezaji hapigwi ganzi bali huchomwa sindano ya kuzuia maumivu na kitendo hicho kinafanywa na daktari mwenye taaluma ya michezo.
“Ganzi lazima umsimamie ili ikiisha umuongeze. Sindano ya kupunguza maumivu unamchoma ili kumuondolea maumivu kwa muda fulani,” anasema.
Hata hivyo, Dk Albert Urimali (maumivu, usingizi na majeraha) wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), anasema tatizo linaweza kuwa kubwa kwa mchezaji aliyechoma sindano hiyo kama ameumia misuli au vikamba vya jointi.
“Kwa mchezaji aliyeumia ankle inakuwa na mambo mengi,” alisema Dk Urimali.
“Unaweza kukuta amekata vikambakamba vinavyoshikilia jointi iweze kupumua. Kama tatizo ni hilo inaweza kumsababishia madhara baadaye.”