Sintofahamu hekta 10,000 alizotoa Magufuli Kasulu
Kasulu. Sintofahamu imeibuka kati ya wananchi wa vijiji vya Kagerankanda na Mvinza katika Wilaya ya Kasulu na Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kuhusu umiliki wa sehemu ya hekta zaidi ya 10,000 ya ardhi iliyomegwa na Serikali kutoka msitu wa Makere Kusini kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Wakati wananchi wa vijiji hivyo vinavyounda Kata ya Kagerankana wakidai haki ya kumiliki ardhi yote ya msitu iliyomegwa mwaka 2017 kwa amri ya aliyekuwa Rais John Magufuli, uongozi wa Halmashauri ya Kasulu na TFS unaungana kupinga madai hayo.
Wakiwasilisha kilio chao mbele ya Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyefika Kijiji cha Kagerankanda katika ziara yake ya kuimarisha chama hicho, baadhi ya wananchi waliushutumu uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kujimilikisha isivyo halali zaidi ya hekta 5,300 zilizopaswa kugawanywa kwa wananchi baada ya kutolewa na Dk Magufuli.
“Sisi wananchi ndio tulipaza sauti kumlilia Rais Magufuli kuhusu kukosa maeneo ya kilimo na mifugo akaamua kutupatia hizo hekta zaidi ya 10,000, lakini uongozi wa halmshauri ukajitwalia zaidi ya nusu ya ardhi yote tuliyopaswa kumiliki,” alisema William Maganga.
Madai hayo pia yalitolewa na Alfred Nsanzugwako kutoka Kijiji cha Mvinza, akisema baadhi ya maeneo ambayo sasa wananchi wanakodishwa kwa malipo kati ya Sh20, 000 hadi Sh50,00 kwa ekari kwa msimu mmoja wa kilimo, yalikuwa yao ya asili na yakatwaliwa kwa shughuli za uhifadhi.
“Yaani TFS imechukua maeneo yetu ya asili na kuyageuza kuwa hifadhi, halafu inatukodishia tena kwa shughuli za kilimo kwa malipo ambayo hata stakabadhi hazitolewi. Huu ni uonevu kwa wananchi,” alisema Nsanzugwako.
Akiunga mkono madai hayo, Boniface Kabulanya alidai ametoa zaidi ya Sh200,000 kukodisha shamba ndani ya eneo la msitu huo tangu Julai 21, mwaka huu, lakini hadi sasa hajapatiwa eneo la kulima na akiuliza anatishiwa na Ofisa wa TFS aliyepokea fedha hizo.
“Fedha hizo nililipa kwa simu na nimehifadhi ujumbe wa kuthibitisha malipo hayo, hadi sasa nasubiri fomu niliyoahidiwa kupewa ili nijaze kabla ya kuonyeshwa eneo la kulima,” alisema Kabulanya.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kasulu Vijijini, Joseph Kasusura mbali na kukiri halmashauri kumiliki zaidi ya hekta 5,000 kati ya zaidi ya 10,000 zilizomegwa kutoka hifadhi hiyo ya msitu kwa amri ya Rais Magufuli, alisema:
“Eneo lile lilimilikishwa kwa halmashauri kisheria kwa ajili ya mipango ya halmashauri na sasa linatumika kwa shughuli za kilimo kwa watu kuomba na kuruhusiwa,” alisema Kasusura.
Hata hivyo, maelezo ya mkurugenzi huyo yanapingwa na wananchi waliodai wanaogawiwa ardhi hiyo ni wale wenye madaraka na walio na uwezo kifedha.
Walidai baadhi ya wanaopewa wanatoka nje ya Kasulu, huku wenyeji wa eneo hilo wenye shida ya ardhi wakikosa maeneo ya kulima.
Mhifadhi Mkuu wa mradi wa Shamba la miti la Makere Kusini, Deograsias Kavishe alisema tangu mwaka 2021, Serikali kupitia TFS ilianzisha mradi wa kilimo cha kupanda miti kwa kuwaruhusu wananchi kulima hifadhini kwa sharti la kupanda na kutunza miti.
“Eneo ambalo wananchi wanaruhusiwa kulima huku wakipanda na kulinda miti linamilikiwa kihalali na TFS kwa mujibu wa GN namba 718 ya mwaka 2018, inayoonyesha eneo la hifadhi ya msitu wa Makere Kusini iliyomegwa kwa ajili ya kilimo,” alisema Kavishe.
“Sheria ya msitu inaruhusu kilimo mseto na wananchi wanaolima ndani ya eneo la hifadhi hawatozwi fedha, isipokuwa wanapewa dhamana na wajibu wa kupanda na kutunza miti katika mashamba yao.”
Alisema dhana ya wananchi kuwa eneo la msitu wanaloruhusiwa kulima kwa mfumo wa kilimo mseto ni ardhi ya kijiji, si sahihi.
Bali alitoa rai kwa wenye nia ya kuomba mashamba wajitokeze watapatiwa kwa mujibu wa taratibu, ikiwemo kujaza fomu maalumu.
Kavishe alisema kutozwa fedha wanaokwenda kuomba ardhi ya kulima kama linafanyika ni kosa.
“Ofisi yangu inafuatilia kwa karibu madai ya hayo kwa sababu huku ni kukiuka sheria,” alisema Kavishe.
Kutokana na malalamiko hayo, Zitto ameitaka Serikali kupitia mamlaka husika na kutatua kero za wananchi, ikiwemo kuwashughulikia maofisa wa TFS wanaotuhumiwa kuchukua fedha kutoka kwa watu ili kuwakodisha mashamba ndani ya msitu wa Makere Kusini bila kuwapa risiti ya malipo.