Sita wafariki kwa kugongwa na gari, 16 wakijeruhiwa

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya akionyesha gari iliyowagonga wakimbiaji wa kikundi cha Adden Palace Hotel na kusababisha vifo vya watu sita huku 16 wakijeruhiwa. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Dereva wa gari iliyosababisha vifo vya watu sita na wengine 12 kujeruhiwa wakifanya mazoezi katika barabara ya Lumala wilayani Ilemela mkoani Mwanza ametokomea kusikojulikana huku polisi wakianzisha msako.

Mwanza. Watu sita wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kugongwa na gari dogo aina ya Toyota Hilux eneo la Shule ya Msingi Lumala wilayani Ilemela mkoani Mwanza walipokuwa wanafanya mazoezi pembezoni mwa barabara.

Aajali hiyo imetokea leo Jumamosi Juni 22, 2023 ambapo dereva huyo anayedaiwa kutokea nyuma yao alisababisha maafa hayo kisha kutokomea kusikojulikana.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema kikundi kinachoundwa na wafanyakazi wa Hoteli ya Adden Palace, wateja na majirani wa hoteli hiyo ndio waliopata ajali wakati wakifanya mazoezi.

Msuya amesema Jeshi hilo limeanza msako wa dereva huyo aiyetelekeza gari hilo kwenye kituo cha mafuta baada ya kusababisha ajali hiyo.

Amewataja waliofariki kuwa ni Makorongo Manyanda, Peter Fredrick, Shedrack Safari, Selestine Safari, Hamis Wariri na Aman Matinde.

Amesema majeruhi 12 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure huku wanne wakipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa uangalizi maalum.

Miili ya marehemu ipo katika Hospitali ya Mkoa Sekou Toure huku taratibu za kuikabidhi kwa ndugu zikiendelea kuratibiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza.

“Nitoe pole kwa familia waliopoteza wapendwa wao na tuendelee kuwaweka kwenye maombi majeruhi wote wapate uponyaji wa haraka na waruhusiwe warudi nyumbani kuendelea na majukukumu yao,” imesema taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala.