Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SMZ yaeleza sababu kusitishwa kwa safari za ndege za Air France, KLM

Muktasari:

  • Mashirika ya ndege ya Air France na KLM yametangaza hivi karibuni kusitisha kwa muda safari zao za moja kwa moja kati ya Paris na Zanzibar kuanzia Machi 22 hadi Mei 25, 2025 na Machi hadi Oktoba 2025, mtawalia.

Arusha. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kusitishwa kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Air France na KLM haihusiani na sera ya bima, bali ni suala la kawaida ikiwa ni sehemu ya marekebisho ya msimu wa safari za utalii.

Hayo yamebainishwa Desemba 20, 2024 na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Zanzibar, Mudrik Ramadhani Soraga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.

Soraga ameyasema hayo zikiwa zimepita siku chache tangu Air France na KLM walipotangaza kusitisha kwa muda,  safari za moja kwa moja kati ya Paris na Zanzibar kuanzia Machi 22 hadi Mei 25, 2025.

KLM, shirika dada la Air France, nalo litasitisha safari zake kutoka Amsterdam kwenda Zanzibar kwa kipindi kirefu zaidi, kuanzia Machi hadi Oktoba 2025.

Waziri Soraga amesema kusitishwa kwa safari hizo ni jambo la kawaida katika marekebisho ya biashara ya utalii hasa ikizingatiwa msimu huo Zanzibar inatembelewa na idadi ndogo ya watalii kutoka nchi hizo.

“Sio kweli kwamba inahusiana na ada ya bima ya usafiri ya Dola za Marekani 44 kwa watalii, bali ni mambo ya kawaida ya marekebisho ya biashara ya safari za anga,” amesema Soraga.

Soraga amesema shirika la Air France bado linaendelea kutua Zanzibar kwa usafirishaji wa mizigo.

Hata hivyo, amesema wanaendelea kufungua masoko mapya ya utalii katika nchi maarufu dunia ikiwemo Poland, India, Korea na Indonesia ili kuhakikisha Zanzibar inatimiza malengo yake ya utalii kwa mwaka.

Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas Manji amewahakikishia wadau wa utalii kuwa itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua.

Pia, amewataka wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi zinazozagaa mitandaoni kuhusu sababu za kusitishwa kwa safari hizo.

“Kama Kuna mtu yeyote ana maoni kuhusu uboreshaji wa sekta yetu tunamkaribisha kujenga nyumba moja ya Zanzibar,” amesema.