SMZ yazindua mkakati kutokomeza maambukizi magonjwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua mkakati kabambe wa kitaifa wa kudhibiti na kutokomeza maambukizi ya virusi vya Ukimwi, homa ya ini B na kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mpango huo umezinduliwa leo Jumanne Novemba 22, 2022 na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi mjini Unguja chini ya udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS).
Akizungumza wakati wa kuzindua mpango huo, Mama Mariam katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amesema maradhi haya bado ni tishio kwa Zanzibar na yanapunguza nguvu kazi za nchi kwa kudhoofisha afya za vijana ambao ndio tegemezi katika uzalishaji wa rasilimali za nchi.
Amesema watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU wanauwezekano wa kufariki ama kulazwa hospitalini mara kwa mara.
“Pia, watoto wanaozaliwa na homa ya ini B wapo katika hatari ya kupata usugu wa maradhi hayo ambayo husababisha hatari kwa ini ikiwemo kusinyaa na kushindwa kufanya kazi na kupata saratani ya ini,” amesema
Amesema, wajawazito wenye maambukizi ya Kaswende nao huwa na uwezekano mkubwa mimba kuharibika, kuzaa mtoto ameshafariki au kuzaa mtoto njiti.
“Serikali kwa kushirkiana na wadau wa maendeleo imewekeza kwa miaka mingi kudhibiti maabukizi na kuwatibu watu wote wanaoishi na mardhi haya,” amesema
Ametumia fursa hiyo kuwataka wajawazito kujitahidi kufika kituo cha afya baada ya kujigundua kupata mimba ili wapimwe na kupatiwa matibabu mapema.
Naye Waziri wa Afya, Ahmed Mazrui amesema mafanikio licha ya kuwapo mafanikio ya kupunguza kasi ya maambukizi mapya lakini bado wananchi wanaambukizwa maradhi hayo na kusambaa kwa kasi.
Kwa mujibu wa Mazrui, miongoni mwa sababu kuendelea kuwapoa maambukizi hayo ni vishawishi mbalimbali, “tutachukua hatua baada ya kuzindua mpango huu nia ni kutyatokomeza ifikapo mwaka 2030.
Naye Mkurugenzi mkazi na Mwakilishi wa UNAIDS, Dk Martin Odiit amesema UNAIDS inatarajia kuwa sehemu ya hatua zinazofuata; utekelezaji wa mkakati na kufikia lengo kuu la kutokomeza magonjwa hayo matatu.