Suluhisho la jinsi mbili

Muktasari:
- Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imesema imeanza kufanya uchunguzi kwa watu waliozaliwa na jinsi mbili ili kujua upande wenye nguvu na iwapo mtu huyo ni mwanamume au mwanamke.
- Hiyo ni kutokana na kile kilichobainishwa kuwa baadhi ya watu wanaozaliwa katika hali hiyo hawajijui ni jinsi ipi yenye nguvu na wengine hujificha bila kutafuta msaada.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, imesema imeanza kufanya uchunguzi kwa watu waliozaliwa na jinsi mbili ili kujua upande wenye nguvu na iwapo mtu huyo ni mwanamume au mwanamke.
Hiyo ni kutokana na kile kilichobainishwa kuwa baadhi ya watu wanaozaliwa katika hali hiyo hawajijui ni jinsi ipi yenye nguvu na wengine hujificha bila kutafuta msaada.
Pia, maabara hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa vinasaba kwa wagonjwa wa figo na ndugu wanaotaka kuwapa figo zao ili wafanyiwe upandikizaji.
Hayo yalisemwa na Daniel Ndiyo, mkurugenzi wa huduma za udhibiti wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, alipozungumza na Mwananchi katika Maonyesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Ndiyo alisema watoto wanaozaliwa na jinsi mbili wapo mitaani, lakini wanafichwa huku akibainisha kuwa wazazi sasa hawapaswi kufanya hivyo, kwa kuwa Ofisi ya Mkemia mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na madaktari wanafanya uchunguzi kuthibitisha ni jinsi ipi inayotawala kati ya ile ya kiume na kike.
“Tukifanya uchunguzi wa kimaabara, tunaweza kutambua huyu ni mwanamke au ni mwanamume, jinsi ambayo haitakiwi kuwepo tunashauri madaktari wamfanyie upasuaji.
“Tukishamfanyia upasuaji ataendelea na maisha yake kama kawaida, anaondokana na maisha ya kujificha na yale ya kutotambulika kuwa yeye ni mwanamke au mwanamume,” alisema Ndiyo.
Alisema tofauti na zamani, angalau hivi sasa watu wanajitokeza na kuelezea hali walizonazo watoto wao baada ya kuzaliwa na hivyo amewataka wengine wajitokeze zaidi.
Mifano iliyopo
Ingawa Ndiyo hakutaja mifano wala idadi ya watu waliojitokeza kwa upimaji, ipo mifano kadhaa iliyowahi kuripotiwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani na masaibu waliyokumbana nayo wahusika.
Miongoni mwao ni Sidney Etemesi, raia wa Kenya aliyezaliwa akiwa na viungo vya uzazi aina mbili, uume na uke aliyeripotiwa na Shirika la Utangazali la Uingereza BBC Juni mwaka jana.
Kwa mujibu wa habari hizo zilizochapishwa katika tovuti ya BBC, Sidney anasema maumbile yake yamekuwa changamoto kubwa katika uhusiano wake na watu wengine katika jamii na ameishi kwa kukejeliwa, japo si hali ya kujitakia.
Ingawa mwili wa Sidney umebeba viungo vya uzazi aina mbili, kwa kumwangalia, bila kujua hali yake ya kuzaliwa nayo, ungemfananisha na mtu mwingine yeyote.
Kwa mujibu wa habari hiyo, yeye huishi kama mwanamume ingawa kwa kiasi mwonekano wake wa sura unaegemea upande wa wanawake.
Hali hiyo ndiyo humchanganya Sidney anapopambana na nafsi yake na kujaribu kujitambulisha kwa wengine.
“Kila siku ya maisha yangu, ninapoingia kwenye bafu nikijitazama maumbile yangu ya kuwa na uke na uume katika mwili mmoja huwa najihisi mnyonge na mwenye hofu kuu. Ila sina la kufanya,” anasema Sydney.
Maisha ya utotoni
Sidney alizaliwa akitambulika kama msichana na wazazi wake wakampa jina Beatrice. Kwa kuwa hali yake ya maumbile ilikuwa ni siri iliyokuwa imefichwa sana na wazazi wake, naye hakuwa na ufahamu kuwa alikuwa tofauti na watoto wengine na wala hakuwa na ufahamu kuwa katika maumbile ya kawaida huwa binadamu anabeba aina moja tu ya viungo vya uzazi.
Lakini siku zilivyozidi kusonga, alianza kujihisi ndani yake kwamba anavutiwa na tabia za kiume. Alianza kujitambulisha kama mtoto wa kiume na kutaka kucheza na wavulana, na hapo ndipo matatizo kati yake na wazazi yalipoanza.
Wao hawakumuunga mkono, wala hawakutaka kusikia chochote kuhusu hisia zake, waliamini alikuwa binti.
Lakini alipotimiza umri wa miaka 13, mwili wake ulianza kubadilika kama watoto wengine, na mabadiliko yake yalianza kufanana na yale ya kiume hadi akatengwa na hatimaye kufukuzwa nyumbani.
Baadaye alibadili jina na kuitwa Sidney badala ya Beatrice.