Tahadhari uwekezaji sarafu mtandao

Muktasari:

Kumekuwa na wimbi kubwa la watu kutaka kuwekeza kwenye sarafu mtandao (cryptocurrency), ikiaminika kwamba ni njia rahisi ya kutajirika kwa haraka.

By Yusuph Kileo

Kumekuwa na wimbi kubwa la watu kutaka kuwekeza kwenye sarafu mtandao (cryptocurrency), ikiaminika kwamba ni njia rahisi ya kutajirika kwa haraka.

Wakati huo huo wahalifu mtandao nao hawako nyuma; wamekuwa wakiiandama kwa kasi miundombinu yake na na hata wawekezaji wa sarafu hiyo.

Kwa mujibu wa serikali ya kenya, mwishoni mwa 2021, Wakenya walipoteza zaidi ya dola 100 milioni kutokana na utapeli kwenye sarafu mtandao.

Nchini Afrika kusini, Juni mwaka jana wawekezaji wa sarafu mtandao kwenye moja ya kampuni inayojishughulisha na sarafu hiyo, walipoteza zaidi ya dola bilioni 3.6.

Wanye nia ya kuwekeza kwenye sarafu mtandao ni muhimu wakajua hatari inayozunguka sarafu hiyo na namna bora za kujilinda na hatari hizo.

Matapeli hawa wana njia mbalimbali za kutapeli ikiwamo kutumia tovuti feki. Huunda tovuti ghushi ya biashara ya sarafu mtandao au matoleo ghushi ya pochi rasmi za sarafu mtandao.

Tovuti hizi ghushi huwa na majina sawa na wakati mwingine tofauti kidogo na tovuti wanazojaribu kuiga kwa madhumuni ya kuiba taarifa za watakaoingiza taarifa zao kwa malengo ya kufanya biashara ya sarafu mtandao au kufanya wizi wa moja kwa moja ambapo tovuti husika itakuruhusu kutoa kiasi kidogo cha pesa.

Njia nyingine ni kutumia programu tumishi feki/ ghushi, zinazoweza kupatikana Google Play na Apple App Store. Ingawa programu hizi mara tu zinapogundulika huondolewa, hiyo haimaanishi kwamba programu tumishi hizo hazija waletea watumiaji athari. Maelfu ya watu wamepakua programu ghushi za sarafu mtandao.

Kupandisha na kuiangusha sarafu mtandao: Hii inahusisha moja ya sarafu mtandao au tokeni kuchagizwa kwa kufanyiwa uhamasisho na matapeli mtandao kupitia barua pepe au mitandao ya kijamii. Lengo likiwa kuwafanya wafanyabiashara kukimbilia kununua sarafu husika, ili kuiongezea thamani sarafu hiyo.

Mara tu baada ya kufanikiwa kuipandisha bei, matapeli hao mtandao wanauza mali zao, jambo ambalo husababisha kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya sarafu husika. Hili linaweza kutokea ndani ya dakika.

Pia wanaweza kughushi kupitia watu mashuhuri: Matapeli wakati mwingine hujifanya au kudai uidhinishaji kutoka kwa watu mashuhuri ili kuwavutia walengwa.

Ulaghai huu unaweza kuwa wa kisasa zaidi, ukihusisha tovuti na vipeperushi vya kuvutia ambavyo vinaonekana kuonyesha kuidhinishwa au kupewa sapoti na watu mashuhuri kwenye biashara ya sarafu mtandao wakiwamo matajiri wa dunia.

Utapeli kupitia zawadi (Give away scams): Matapeli mtandao hutumia njia ya kuwahadaa wawekezaji wa sarafu mtandao kwa kuwaambia watakapowekeza wanaweza kupata mara mbili ya walichokiwekeza na mara nyingi hutumia akaunti zinazoweza kuonekana kuwa ni rasmi, jambo litakalowafaya wafanya biashara wa sarafu mtandao kuwekeza kwa kasi wakitegemea faida ya haraka.

Kuna viashiria mbalimbali unavyoweza kutumia kugundua uhalifu huu, ikiwamo kuaminishwa kuwa ukiwekeza utapata faida tu na si vinginevyo. Ikumbukwe kwenye biashara kuna kupata na kukosa pia. Nenda na uhalisia huu, tilia shaka taarifa ya kufaidika pekee.

Kiashiria kingine ni andiko kuhusiana na sarafu mtandao husika kukosekana au kuwa na mashaka, Kila sarafu mtandao huambatana na andiko linalohusiana na sarafu hiyo. Pale inapotokea taarifa sahihi kukosekana, ni kiashiria kingine kuwa sarafu mtandao hiyo ina walakini.

Kutopatikana kwa majina ya timu ya washiriki wa sarafu husika. Ni muhimu kujua ni kina nani wako nyuma ya sarafu husika. Ikiwa huwezi kujua ni nani anayeendesha sarafu hiyo, kuwa mwangalifu.

Unajilindaje? Lazima ulinde mkoba wako wa sarafu mtandao, Ili kuwekeza katika sarafu mtandao, unahitaji pochi (mkoba) uliyo na funguo binafsi (private key). Ikiwa kampuni itakutaka uzitoe funguo zako ili kushiriki katika fursa ya uwekezaji, kuna uwezekano mkubwa kuwa ni ulaghai. Weka faragha funguo za mkoba wako.

Angazia kwa umakini programu tumishi ya mkoba wako wa sarafu, inashauriwa mwekezaji au mfanya biashara wa sarafu mtandao kwa mara ya kwanza unapoanza kufanya biashara, kutuma kiasi kidogo tu cha fedha ili kuthibitisha uhalali wa programu tumishi.

Ikiwa unasasisha (updating) programu yako ya pochi na ukaona hali ya kutilia shaka, sitisha programu hiyo.

Aidha, tunashauri watumiaji kuwekeza kwenye vitu wanavyovielewa. Hakikisha unafanya uchunguzi wa kina na kujiridhisha kuhusiana na sarafu unayotaka kuwekeza.

Yusuph Kileo ni mtaalamu bobezi wa mifumo ya usalama mitandaoni. 0746626167 Blog: http://ykileo.blogspot.com/ykileo.blogspot.com/>