Taifa Stars ilipigana vita bila ya silaha

Stars yajipa mtihani mzito Cameroon

Muktasari:

  • Kuna wakati tulikuwa tukiamini kuwa Tanzania haiwezi kuingia katika vita na China kwa sababu ikitaka kufanya hivyo, taifa hilo la Asia litaamuru wananchi wake waje Afrika Masharina kusimama kuizunguka nchi kwa kuwa ni wengi.

Kuna wakati tulikuwa tukiamini kuwa Tanzania haiwezi kuingia katika vita na China kwa sababu ikitaka kufanya hivyo, taifa hilo la Asia litaamuru wananchi wake waje Afrika Masharina kusimama kuizunguka nchi kwa kuwa ni wengi.

Kwa uwingi huo tutashindwa kupigana nao kwa kuwa watakuwa wako katika kila mpaka na bado wana jeshi.

Hizo zilikuwa akili za kitoto lakini zilizojengwa katika kuaminisha kuwa wingi unaweza kuwa silaha tosha katika vita.

Viko vitu vingi vingine vinavyoweza kuisaidia nchi vitani; kama mbinu za medani na silaha za kisasa.

Cha msingi ni kwamba ni lazima uwe na cha ziada kumzidi mwingine ili uweze kushinda vita au mashindano mengine yoyote.

Jana usiku tumeshuhudia timu yetu ya taifa ya soka, Taifa Stars ikilala kwa mabao 2-0 mbele ya Zambia katika mechi yake ya kwanza ya fainali za MIchuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) yanayofanyika nchini Cameroon.

Kipigo hicho kiliifanya Tanzania kuwa ya kwanza kupoteza mchezo kwa zaidi ya bao moja, ingawa baadaye usiku sifa hiyo ikahamia kwa Namibia iliyochapswa mabao 3-0 na Guinea, timu nyingine mbili za kundi letu.

Kocha Etienne Ndayiragije aliamua kujaribisha takriban wachezaji watano wapya katika mechi hiyo dhidi ya Zambia, ambayo licha ya kuwa juu katika orodha ya ubora wa Fifa, haionyeshi kuwa na kikosi kikali.

Charles Manyama, Carlos Protus, Baraka Majogolo, Lucas Kikoti, Yusuf Mhilu na Ayoub Lyanga walipewa nafasi ya kuanza katika mechi hiyo, huku Lyanga na Majogolo pekee wakiwa wamejaribiwa katika mechi dhidi ya Congo DR.

Hao walishirikiana na Aishi Manula, Bakari Mwanyeto, Shomari Kapombe, Feisal Salum na Ditram Nchimbi kuunda kikosi kilichoanza dhidi ya wazoefu Zambia.

Ingawa haikuonekana tofauti kubwa katika kipindi cha kwanza, ni dhahiri uzoefu uliamua mchezo katika kipindi cha pili wakati krosi mbili kutoka kushoto zilipozaa penati na bao la pili lililofungwa kiufundi.

Kawaida beki mmoja wa pembeni hutakiwa kuwa wa mwisho wakati mpira unapotoka upande mwingine na ndivyo alivyofanya Kapombe katika bao la kwanza. Alifika mbele ya lango haraka kudhibiti Mzambia asiunganishe wavuni krosi, lakini bahati mbaya mpira ukamgonga mkononi na kusababisha penati iliyozaa bao, licha ya Manula kujinyoosha kuifuata.

Bao la pili pia lilitokana na krosi iliyotoka kushoto. Baada ya Wazambia kugongeana pasi fupifupi upande wa kushoto, hatimaye Collins Sikombe aliburuziwa mpira kuelekea mstari wa mwisho.

Wakati Sikombe akifikiria afanye nini, Emmanuel Chibula, aliyekuwa nyuma ya Kapombe, alitoroka na kwenda mbele ya lango akiwa takriban miguu 12 na ndipo Sikombe akamuona na kumpiga krosi ya kimo cha mbuzi aliyeiunganisha moja kwa moja wavuni.

Ni dhahiri winga wa kulia alitakiwa awe ameona utoro huo wa Chibula na kwenda kumghasi, lakini takriban macho ya wachezaji wetu wote yalielekea kule mpira ulikokuwa na si kwa wachezaji waliokuwa katika sehemu hatari.

Ni rahisi kusema mabao hayo yalitokana na matukio na si mikakati ya Wazambia, lakini iweje yatokee mbele ya goli? Kuna kitu Wazambia walituzidi.

Haikueleweka sababu za kocha kuwaacha benchi wazoefu kama Said Ndemla, ambaye angeweza kusukuma mbele mashambulizi na kuiunganisha timu vizuri, Deus Kaseke, Dilunga na Farid Mussa, ambao anawafahamu na ameshawajaribu, achilia mbali akina Aboubakar Salum na Mzamiru, ambao uwezo wao hauna shaka.

Kwa kipindi cha mwaka mmoja alichokaa na Stars, wakati huu wa fainali angekuwa ameshapata kikosi na si kuendelea kujaribu kama anavyofanya sasa katika hii vita ya Cameroon.

Na ukijiuliza maswali hayo, yanakuja mengine mengi; kwanini hakumuita Tshabalala, Metacha Mnata, Frank Domayo na wengine.

Pia yatakuja maswali, hivi mechi zilizopita zilikuwaje tangu Ndayiragije apewe timu. Mwishoni utaonekana una tatizo naye na si kwamba kuna tatizo katika timu.

Timu iliruhusu Wazambia wachezee mpira katika nafasi kubwa iliyokuwa ikiachwa, kama ilivyokuwa katika mechi na DRC, ambao walipata nafasi kubwa katikati ya uwanja kutembeza mpira walivyotaka.

Stars ilipokwenda kushambulia, haikuwa rahisi kujua inatumia njia gani (scientificity), na matokeo yake unaona mpira umeshafika na hivyo hakuna uwiano mzuri wa wachezaji mbele ya goli, achilia mbali katikati na nyuma iwapo mpira unapotea.

Mara kadhaa wachezaji walipambana kupokonya mpira lakini walipoupata hawakuonekana wanajua wautumieje na hawakuonekana wanajua nguvu yao iko wapi ili waitumie vizuri; kutumia nguvu na kasi ya Ditram Nchimbi? kutumia ustadi wa kikoti kutoa pasi za mwisho? Kutumia stadi za Lyanga kumlisha Nchimbi? Au kuwatuliza Wazambia kwa kumiliki mpira kwa muda mrefu?

Mpira tulipoupata tuliupeleka mbele, ambako ulipokonywa na kurudishwa tena kwetu kwa kasi, huku washambuliaji wao wakiwa na uwezo wa kuwahi mipira ya kichwa na kuiendeleza mbele au kurudisha kwa viungo ili waanzishe mashambulizi ya uhakika.

Mambo hayo mengi yanategemea uzoefu ambao Ndayiragije aliamua kuupumzisha.

Silaha yetu kwa Wazambia bila ya kujali ubora wao Fifa, ilikuwa ni uzoefu wa wachezaji tuliowaita-- tena wengine wameitwa baada ya kukaa nje ya kikosi kwa miaka kadhaa.

Hatuwezi kwenda vitani bila ya kujua nguvu yetu iko wapi au tukaenda vitani na nguvu yetu, lakini tukaipumzisha badala ya kuitumia.


Imeandikwa na Na Angetile Osiah