Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takataka zinapogeuzwa fursa mijini

Muktasari:

Wakati Watanzania wakiungana na watu wengine duniani kuadhimisha siku ya mazingira duniani, mbali na tatizo la ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, kwa Tanzania lipo tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira.

Mkaa ni gharama, tumia nishati mbadala.’ Hiyo ni kauli mbiu ya mwaka huu katika ya Siku ya Mazingira duniani ambayo kilele chake ni leo Juni 5.

Wakati Watanzania wakiungana na watu wengine duniani kuadhimisha siku ya mazingira duniani, mbali na tatizo la ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa, kwa Tanzania lipo tatizo kubwa la uchafuzi wa mazingira.

Mazingira yanachafuliwa kutokana na utupwaji ovyo wa takatala za kila aina huku hali ikiwa mbaya zaidi katika jiji la Dar es Salaam, jiji lenye watu zaidi ya milioni tano huku wakishindwa kabisa kuwa na ustaarabu katika uhifadhi wa takataka.

Hali ikoje Dar es Salaam.?

Ofisa Afya, Mazingira wa Jiji la Dar es Salaam, Enezael Ayo anasema kwamba kwa siku moja mkoa wa Dar es Salaam unazalisha tani 4,600 za takataka.

“Kutokana na kiasi kikubwa cha taka kinachozalishwa na jiji hili, halmashauri ya jiji iliamua kuhamasisha vikundi vya vijana na wanawake zaidi ya 10, kuingia katika biashara ya kutengeneza mkaa unaotokana na takataka, lengo likiwa kupunguza idadi ya takataka tunazopeleka katika dampo la Pugu Kinyamwezi,” anasema Ayo.

Anasema halmashauri ya jiji ilitoa Sh100 milioni kwa ajili ya kununua mashine na kuzikabidhi kwa vikundi hivyo ili kutengeneza nishati mbadala ya mkaa inayotokana na taka.

Hata hivyo hadi sasa bado mradi huo haujaweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mkuu wa Idara ya Usafi Manispaa ya Temeke, Ally Hatibu anasema kwa siku tani 1400 za taka, huzalishwa katika manispaa hiyo.

“Kati ya tani 1400 tunazozalisha kwa siku katika Manispaa ya Temeke, ni tani 875 pekee ndio tunazipeleka katika dampo la Pugu Kinyamwezi” anasema Hatibu akimaanisha kwamba zaidi ya tani 500 hazijulikani zinapoishia.

Anasema moja ya mikakati ya manispaa hiyo ni kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya namna bora ya kutunza mazingira.

“Mkakati mwingine ni kuwapata wahandisi wenye uwezo na vifaa vya kuzolea taka ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati” anabainisha.

Kwa upande wake, Ofisa Afya Hospitali ya Rufaa Temeke, Juhudi Nyambuka anasema jamii haina budi kuzingatia sheria na kufuata taratibu za utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuepuka milipuko ya magonjwa.

Sheria ya mazingira inasemaje?

Hatibu anafafanua kuwa mtu akichafua mazingira anatakiwa kupigwa faini ya Sh 50,000 au kifungo kisichopungua miezi 12 na hii ni kwa mujibu wa sheria ambayo imetungwa na halmashauri.

“Lakini sheria iliyotungwa na Bunge mwaka jana, inasema kuwa mtu akichafua mazingira kwa kutupa taka ovyo anatakiwa apigwe faini kuanzia Sh 200,000 hadi milioni moja au kifungo cha miaka miwili jela,” anafafanua Hatibu.

Pia, Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 (Environmental Management Act) inaelekeza kuwa, kwa yeyote anayechafua mazingira, atatakiwa kulipa faini kuanzia Sh1 milioni hadi 50milioni.

Kauli ya Waziri Mkuu

Akizindua maadhimisho ya Wiki ya Mazingira, Mei 31, mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema haoni sababu kwa wananchi kuendelea kutumia mkaa wa kuni ambao una gharama kubwa, wakati kuna nishati mbadala ambayo bei yake ni nafuu.

Majaliwa anabainisha kuwa ni wakati kwa wakazi wa Dar es Salaam kubadilika na kuachana na matumizi ya mkaa, kwani kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.

Takataka ni mradi

Wakati wakazi Dar es Salaam wakilia na tatizo la takataka, kijana Mohamed Msangi takataka kwake takataka ni fursa, ameanzisha mradi wa kuzoa taka nyumba kwa nyumba na kisha kwenda kuzichakata kwa ajili ya kutengeneza mbolea na nishati mbadala.

“Ajira hazitafutwi bali zinatengenezwa na ili ufanikiwe inabidi uiheshimu kazi yako ndipo itakupa kipato na kupata mafanikio hata kama kazi hiyo ina muonekano wa tofauti mbele ya jamii,” anasema Msangi (30).

Msangi ameamua kubadili maisha yake, baada ya kuchukua mkopo wa Sh 17 milioni kutoka Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) na kuanzisha mradi wa kuzoa taka katika kata tatu za Manispaa ya Morogoro, ambazo ni Boma, Kilakala na Kichangani zenye mitaa zaidi ya 10. “Mwanzo ilikuwa ngumu kueleweka kwa jamii lakini kwa sasa wametuelewa kwa kuwa tunatoa huduma bora na ya kisasa,” anasema Msangi ambaye kwa sasa anamiliki kampuni ya uzoaji taka ya Mwale Cleaner, iliyopo Kilakala, Morogoro.

Anafafanua kuwa tangu aanzishe mradi huo mwaka 2016 hadi sasa zaidi ya wateja 500 wamefikiwa na huduma hiyo.

“Vijana wenzangu tusitegemee kuajiriwa, tujiajiri, kuthubutu na kujiamini ndio kufanikiwa, ukianguka unainuka na kuendelea na safari,” anasema Msangi.

“Nilivyomaliza kidato cha sita, mwaka 2012 katika Sekondari ya New Castrol nchini Uganda, nilirudi Tanzania na matokeo yalivyotoka nilitakiwa kuendelea lakini sababu za kiuchumi zilinifanya nishindwe kujiunga na elimu ya juu, hivyo nikaamua kujiingiza katika biashara ya kuuza nguo na baadaye mboga ambazo zote hazikunilipa,” anasema Msangi.

Anasema baada ya kuachana na uuzaji nguo, mboga na matunda, alianza kutengeneza mbolea kupitia taka, lakini soko la mbolea kwa kipindi hicho halikuwa zuri, ndipo alipokuja na mbinu mpya ya uzoaji taka nyumba kwa nyumba.

Msangi anasema hadi kuanzisha huduma hiyo chanzo chake ni kukithiri kwa ugonjwa wa kipindupindu siku za nyuma kutokana na mrundikano wa takataka katika maeneo hayo.

“Baada ya kuona ugonjwa wa kipindupindu umekuwa tatizo katika maeneo tunayoishi, niliona nifanye utafiti mdogo tu ambao nilibaini kuwa tatizo kubwa ni takatakata zinazorundikana maeneo mengi,” anasema Msangi ambaye mafunzo ya uzoaji taka alijifunza nchini Zimbabwe.

“Niligundu kuwa asilimia 70 ya magonjwa ambayo binadamu anaugua yanazalishwa kupitia takataka na hii ndio sababu niliamua kuanzisha mradi huo wa kuzoa taka katika kata hizo” anabainisha.

Anafafanua kwamba wakati anaanza mradi alianza na mtaji wa Sh20 milioni lakini kwa sasa ana mtaji wa zaidi ya Sh 60milioni.

“ Wakati naanza huduma hii, nilikuwa na bajaji tatu na pikipiki, lakini kwa sasa nina gari moja aina ya Fuso kwa ajili ya kuzolea takataka, bajaji zaidi ya nne na pikipiki ambazo zimewekewa mifuko maalum ya taka na nimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 10,” anasema Msangi na kuongeza:

“Sikuvutiwa na mtu yeyote hapa nchini kuanzisha mradi huu, bali nilivutiwa na kampuni moja ya Uingereza iitwayo West Management, ambayo inatoa huduma ya uzoaji taka nyumba kwa nyumba, nikaona kwa nini na mimi nisifanye hivi,” anabainisha Msangi, ambaye kampuni yake inajiendesha yenyewe na sasa ina mtaji wa zaidi ya Sh60 milioni kutoka Sh 20milioni.

Anavyotoa huduma

Juliana Joseph anayefanya kazi katika kampuni ya Mwale Cleaner, anasema mteja anayejiunga na huduma hiyo anapaswa kujaza fomu ambayo itakuwa na anuani yake na kuingizwa katika mfumo wa kampuni hiyo.

Anasema baada ya mteja kujaza fomu, anatakiwa kulipia huduma hiyo kwa Sh6,000 kwa mwezi ambapo, kampuni hiyo inapita kwa wateja hao mara tatu kwa wiki kwa ajili ya kuzoa taka.

“Pia tunafuatili wateja wetu kujua kama wanaridhika na huduma hii na pale kwenye changamoto, mteja anakuwa na namba za viongozi wetu, anaweza kupiga muda wote na kusaidiwa,” anasema Juliana.

Malengo na mikakati yao

Juliana anaeleza kuwa moja ya mikakati yao ni kuzalisha fursa za ajira kwa vijana 1,000 ifikapo mwaka 2020 na kuongeza idadi ya wateja kutoka 500 hadi kufikia 5,000 ifikapo mwaka 2025.

Anasema lengo la kampuni hiyo ni kutoa huduma bora ya kufanya usafi wa mazingira kwa kuzoa taka majumbani, kwenye kampuni na taasisi mbalimbali ili kulinda mazingira na kulinda jamii zinazowazunguka, lakini pia.

“Ndoto yangu ni kuwekeza katika maeneo ambayo yamekuwa na tatizo sugu la takataka na kuendelea kutoa huduma ya uzoaji taka katika maeneo yote ya mkoa wa Morogoro na Tanzania,” anasema Msangi.

Anasema wapo mbioni kuingia mkataba na kampuni moja ya nchini Zimbabwe ili kuboresha huduma hiyo na wanatarajia kusaini mkataba wenye thamani ya Sh 280 milioni.

“Tupo katika mchakato wa kutafuta eneo kubwa kwa ajili ya kuchakata takataka tunazokusanya ili ziwe mbolea na nishati mbadala ya kupikia,” anaeleza Msangi.