Takukuru yachunguza watumishi wanaotoza fedha wajawazito

Muktasari:

Watumishi wanaochunguzwa ni kutoka baadhi ya zahanati mkoani Tabora baada ya kulalamikiwa na wajawazito kuwalipisha kuanzia Sh45,000 hadi Sh90,000  ili wapate huduma.

Tabora. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tabora inawachunguza watumishi wa baadhi ya zahanati mkoani humo wanaodaiwa kuwalipisha wajawazito wanaokwenda kujifungua ili wapate huduma.

Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo amesema watumishi hao wamelalamikiwa kuwatoza wajawazito kuanzia Sh45,000 hadi Sh90,000 ili wapate huduma ya kujifungua kwa upasuaji.

“Wamewalalamikia wahudumu katika baadhi ya zahanati kuwatoza kiasi hicho cha fedha ili wapate huduma ya upasuaji,”amesema

Chaulo ambaye amekataa kutaja idadi ya watumishi wanaochunguzwa pamoja na zahanati wanazofanyia kazi ili kutovuruga uchunguzi, amesema watakapoukamilisha watatoa taarifa kamili.

Ameeleza kuwa kuna Wilaya mbili ambazo zahanati zake ndio zinaongoza kulalamikiwa na kuwa huenda idadi ya wajawazito wanaolalamika ikaongezeka kutokana na mwamko walionao wananchi na wajawazito.

Akizungumzia malalamiko yaliyopokelewa katika kipindi cha Julai hadi Septemba , 2023 amesema wamepokea malalamiko 74 ambapo malalamiko 48 yalihusu rushwa na 26 hayakuwa na viashiria vya rushwa.

Alisema malalamiko 23 yasiyohusu rushwa watoa taarifa wameshauriwa njia bora ya kutatua malalamiko hayo na 3 yalihamishwa idara zingine ili kupatiwa ufumbuzi.

Chaulo amezitaja sekta zilizolalamikiwa na idadi yake kwenye mabano kuwa ni  Tamisemi (51), Afya na Mahakama (7 kila sekta), Polisi (5) na Ardhi (4).

Baadhi ya wakazi katika Manispaa ya Tabora wamesema pamoja na jitihada za Serikali kutoa elimu kuhusu huduma pasipo malipo kwa wajawazito bado utekelezaji umekuwa haufuatwi kikamilifu.

"Mimi nilienda kujifungua katika zahanati ambayo nilitakiwa kutoa fedha Sh30,000 kwa ajili ya gloves" amesema Mwanaidi Athuman mkazi wa Mtaa wa Rehani Manispaa ya Tabora.

Naye Lucy Kandoro mkazi wa Mtaa wa Nyembo kata ya Ipuli amesema wajawazito kuombwa chochote bado ipo ingawa kwa sasa inaangaliwa hali ya mtu.