Takukuru yamkabidhi shamba mjane wa Profesa Doriye

Tuesday April 13 2021
mjane pc
By Joseph Lyimo

Babati. Mjane wa aliyekuwa katibu mkuu ofisi ya rais, mipango na uwekezaji, Profesa Joshua Doriye aliyedhulumiwa shamba na viongozi wa kijiji cha Getanuwas wilayani Hanang’ mkoani Manyara amerejeshewa shamba hilo na Takukuru.


Akizungumza jana Jumatatu Aprili 12, 2021 mjini Babati mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Makungu amesema mjane huyo alitaka kudhulumiwa shamba hilo na mwenyekiti wa kijiji hicho,  Adam Mwanga.

Makungu amesema Profesa Doriye katika uhai wake kama ilivyo kwa watanzania wengine alikuwa na haki ya kumiliki mali ikiwa ni haki ya kikatiba iliyoainishwa chini ya ibara ya 24 (1) (2) katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomeka pamoja na madhumuni ya kutungwa kwa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Amesema kati ya mali alizofanikiwa kumiliki wakati wa uhai wake ni shamba lililopo kijiji cha Getanuwas wilayani Hanang’ mkoani Manyara.

Amesema mwaka 2019 mjane huyo wakati akishughulikia mirathi, Mwangu kwa kushirikiana na watu wengine waliokuwa na nia ovu ya kutwaa shamba hilo,  walikataa kutambua umiliki wa ardhi katika kijiji hicho  na  kukwamisha ufungaji wa shauri la mirathi namba 47/2019 uliokuwa ukiendelea mahakama ya mwanzo Kawe.

Advertisement

Amesema uchunguzi wao umebaini Profesa Doriye alipewa shamba hilo na Serikali ya kijiji cha Getanuwas tangu mwaka 1978 na umiliki wake haukuwahi kuangaliwa na mtu yeyote katika kipindi chochote na nyaraka zote kuhusu umiliki zipo na viongozi wa wakati huo wamethibitisha pasipo shaka umiliki wa shamba hilo.

Amebainisha kuwa shamba hilo pamoja na nyaraka walikabidhi rasmi kwa mjane ili aweze kuendelea na utaratibu wa kufunga mirathi hiyo katika mahakama ya mwanzo Kawe.

Amesema wanaendelea kuchukua hatua kwa wachache ambao kwa tamaa zao wanagombea nafasi za kisiasa zikiwemo uenyekiti wa mtaa na vijiji kwa nia ovu ya kwenda kupora mali za wananchi zilizopatikana kwa njia halali.

Advertisement