Tanapa yafunga kipande cha njia Mlima Kilimanjaro
Muktasari:
- Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na kusababisha maporomoko ya mawe na miamba ya barafu, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), limefunga kipande cha njia cha ‘Arrow Glacier’ ambacho hutumika na baadhi ya wageni wanaopanda mlima huo kupitia njia ya Machame, Lemosho, Londorosi na Umbwe.
Moshi. Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), limefunga kipande cha njia cha ‘Arrow Glacier’ ambacho hutumika na baadhi ya wageni wanaopanda Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Machame, Lemosho, Londorosi na Umbwe.
Taarifa za kufungwa kwa njia hizo, zimetolewa na Ofisa Uhifadhi Mwandamizi Kitengo cha Mawasiliano Tanapa, Catherine Mbena, huku ikieleza inatokana mvua zinazoendelea kunyesha katika mlima huo na kusababisha maporomoko ya mawe na miamba ya barafu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kusitisha matumizi ya kipande hicho, itatumika njia ya kawaida ya kutokea Baranco kelekea Karanga hadi kufika kileleni, hadi hapo mvua zitakapokoma na ukaguzi kufanyika, ili kujiridhisha kuwa njia hiyo ni salama.
"Ukaguzi uliofanywa na timu ya wataalamu wa Tanapa ikishirikiana na watalaamu wa taasisi ya NOLS (National outdoor leadership school), wenye uzoefu katika masuala ya usalama wa milimani, umeonyesha hali imezidi kuwa mbaya kwani maporomoko ya mawe, miamba ya barafu na utelezi yameongezeka na si salama kwa watumiaji." imeeleza taarifa hiyo.
Kipande cha 'Arrow Glaciers' kinaanzia karibu na kituo cha Baranco katika eneo la 'Lava tower' na kinapita kwenye kasoko (crater) kuelekea kileleni ambapo wageni hupendelea kupita eneo hilo kwa ajili ya kuona mandhari nzuri ya mlima na pia ni rahisi kufika kileleni.
Januari 19, mwaka huu, Kitongoni cha Marukeni, kilichopo Kata ya Machame Kaskazini na Kijiji cha Lyamungo Kati, Wilaya ya Hai, mkoani hapa vilikumbwa na mvua ya mawe ya barafu iliyoambatana na upepo mkali.
Imeelezwa kuwa athari zilizotokana na mvua hiyo, ni kuangushwa kwa migomba zaidi ya ekari 20, kahawa na parachichi, huku nyumba zaidi ya 15 zikiharibiwa kutokana na kuangukiwa na miti mikubwa.