Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi watakiwa kuulinda Mlima Kilimanjaro

Mwenyekiti wa UVCCM Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, Yuvenal Shirima.

Muktasari:

  • Wananchi wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutumia kipindi hiki cha mvua kupanda miti kwa wingi katika maeneo ya wazi, kuzunguka vyanzo vya maji na maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro.

Moshi. Wananchi wa Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wametakiwa kutumia kipindi hiki cha mvua kupanda miti kwa wingi katika maeneo ya wazi, kuzunguka vyanzo vya maji na maeneo ya kuzunguka mlima Kilimanjaro, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zimekuwa tishio nchini na duniani kote.

Rai hiyo imetolewa leo ijumaa April 7, 2023 na mwenyekiti wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi vijijini, Yuvenal Shirima ambapo amesema bado zinahitajika jitihada za makusudi za kupanda miti, ili kuilinda barafu iliyopo katika mlima Kilimanjaro.

Shirima amesema athari za mabadiliko ya tabianchi ni nyingi ikiwemo kupungua kwa mvua na kipindi kirefu cha ukame na kwamba ili kuweza kukabiliana na athari hizo, kila mwananchi anapaswa kupanda miti katika maeneo wanayoishi, maeneo ya wazi na kuzunguka vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuitunza.

Aidha amesema ni jukumu la kila mmoja kushiriki kupanda miti kwa wingi katika kipindi hiki cha mvua za masika, ili kuongeza barafu katika mlima kilimanjaro na  kuhakikisha mazingira yanapendeza na hali ya hewa inakuwa nzuri.

"Hakuna ambaye haoni mabadiliko haya ya tabianchi kwa sasa, kila mmoja ameshuhudia, naomba tuchukue hatua wote za kukabiliana nayo ikiwemo kupanda miti, kulinda na kutunza vyanzo vya maji na kuepuka uharibifu wowote wa mazingira na misitu".

Ameongeza kuwa "Tumeendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti katika naeneo mbalimbali ikiwemo maeneo ya kuzinguka mlima Kilimanjaro ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutunza barafu ya mlima Kilimanjaro. Lakini pia tukipanda miti kwa wingi tutawezesha hali ya hewa kuwa nzuri"

"Pia tuombe vyama vyote vya siasa, tushirikiane kuhamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi, kwani jambo la maendeleo halina chama, na katika jambo la maendeleo tuungane kwa umoja wetu, kulitekeleza kwa nguvu".

Akizungumza Naima Shaaban mkazi wa Moshi, amesema bado elimu yautunzaji wa mazingira, inahitajika katika jamii, ili kuchochea kasi ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini.

"Kumekuwepo na kasi ya ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira hadi kwenye misitu, na katika kukomesha hili, tunahitajika kutolewa kwa elimu kwa wananchi na kuwekwa kwa sheria kali za kuwabana wale watakaobainika kuharibu mazingira" amesema Naima