Tanesco yaanza majaribio ya smart mita
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Martin Mwambene akizungumzia utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo
Muktasari:
- Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) limeeleza utekelezaji wa majukumu yake huku ikianisha mipango yake ya kuwezesha wateja kufanya malipo ya umeme na kuingia katika mita moja kwa moja kama utaratibu inavyofanyika kwenye ving’amuzi.
Dodoma. Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) limesema liko katika majaribio ya mita za umeme ambazo mteja ataweza kulipia na kuingia kwenye mita husika moja kwa moja kama inavyofanyika kwenye ving’amuzi.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Februari 22,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja wa shirika hilo, Martine Mwambene wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo.
Amesemwa waliahidi kuwa Agosti mwaka jana wawe na smart mita ambazo zinamwezesha mteja kununua na kuingiza umeme moja kwa moja kama ilivyo kwenye king’amuzi.
“Mchakato wa programu hii unaendelea kilichotokea ni hizi mita zinagharama na wakianza kuzifunga bila kuangalia wanaweza kupeleka mzigo mkubwa wa gharama kwa mwananchi,” amesema.
Amesema wanaangalia teknolojia iliyobeba vitu vingi na gharama ambayo itaweza kuhimilika kwa mteja.
Amesema kuna majaribio yanaendelea kufanyika ya baadhi ya mita na itakayokuwa bora zaidi ndio itakayotumika.
Aidha, Mwambene amesema wao hawauzi umeme na kuwa wanachouza wao ni huduma wanazozitoa.
“Yapo mazingira ambayo mteja amekuwa akigharamia nguzo zaidi ya sita, sheria inaruhusu namna ya kumfidia na anafidiwa kupitia wateja watakaounganishwa katika eneo hilo. Lakini inatumika zaidi katika miradi,” amesema.
Amesema kwenye mteja kugharamia nguzo tatu ni gharama za kawaida ambazo ziko katika utaratibu wao wa malipo.