Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanesco yatenga Sh500 milioni kuondoa ukatikaji umeme Morogoro

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Morogoro baada ya kuzindua uwekaji nguzo 900 za zege.Lilian Lucas.

Muktasari:

  • Shirika la Umeme Tanesco, ofisi ya Morogoro imeanza maboresho ya miundombinu ya umeme kwa kuondoa nguzo zilizochakaa na kuweka nguzo za zege hatua itakayosaidia kupunguza adha ya kukatika umeme kunakotokea mara kwa mara kwa wakazi wa maeneo ya Turiani na Msamvu

Morogoro. Katika kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa umeme mara kwa mara, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Morogoro limeanza kuboresha miundombinu ya huduma hiyo kwa kuondoa nguzo za miti na kuweka za zege.

Maboresho hayo ya nguzo zaidi ya 900 kwa awamu tatu zitawekwa kwenye laini ya Turiani- Kibati – Dakawa kwenda hadi maeneo ya Msamvu na kukamilika kwake kutaleta unafuu wa huduma hiyo kwa wananchi na wafanyabiashara wa Turiani Wilaya ya Mvomero.

Akizungumzia wakati wa uzinduzi uwekaji wa nguzo hizo Turiani leo, Jumanne Januari 2, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli amesema wilaya hiyo imekuwa na changamoto ya kukatika kwa umeme jambo linalokwamisha shughuli za maendeleo.

“Mwaka jana mlitoa kilio kikubwa cha umeme kusumbua katika tarafa hii ya Turiani, kiasi kwamba imekuwa ikipunguza uzalishaji wa uchumi, lakini leo tunaona nguvu zimeelekezwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme,” amesema

Amesema mradi huo una thamani ya zaidi ya Sh500 milioni na utaondoa nguzo zilizochoka na kuweka mpya huku akieleza timu ya vijana wataalamu imeshafika kwa ajili ya kuanza kufanya kazi kwa siku 40.

Nguli amewataka wananchi na wafanyabishara wa maeneo hayo kuwa wavumilivu katika kipindi cha kukosekana kwa huduma hiyo ikiwa na kuchukua tahadhari pindi watakapoona nyaya chini.

Akizungumzia matengenezo hayo, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Fadhili Chilombe amesema Turiani ni laini inayosumbua na kuongoza kwa tatizo la umeme kimkoa kwa sababu ya ukubwa na urefu wa laini.

“Maboresho ya awamu ya kwanza yatakamilika ndani ya siku sita itahusisha ubadilishaji wa nguzo 250 na uwekaji wa konekta kwenye makutano yote kwenye eneo litakaloguswa na kazi hiyo itaanzia Turiani mpaka mpakani mwa Tanga na Morogoro,” amesema nakuongeza

“Matumaini yetu tukishakamilisha hiyo kazi kwenye hicho kipande hatutegemei kupata tatizo lolote, awamu ya pili itaanzia hapa Turiani hadi Dumila mpaka Kikunde itahusisha ubadilishaji nguzo 220 na kuweka konekta 1,350,” amesema.

Meneja huyo amesema awamu ya tatu itaanzia Dumila mpaka Msamvu mahali ambapo umeme unatoka na kwa ujumla kazi hiyo itagharimu zaidi ya Sh500 milioni lengo ni kuona maeneo hayo ya Turiani na baadhi ya maeneo ya mjini umeme utatulia kabisa.

Amesema baada ya kukamilika kwa laini hiyo, Tanesco itaanza kazi kwenye laini inayotoka Msamvu kwenda Kilosa, jumla ya vikundi 12 vyenye watu 15 kila kikundi ili kufanya kazi kwa ufanisi.

“Morogoro ya sasa haiko hivyo, tumejipanga na tumeona sio sawa kuendelea na ule utaratibu wa miaka yote kuwa kuanza kazi leo na kumaliza baada ya miezi sita, lengo letu ni kuhakikisha mpaka kufika mwezi wa sita mwaka huu 2024 matatizo ya umeme yote ndani ya mkoa,” amesema.

Pia amesema, uchunguzi walioufanya na uzoefu walionao unaonyesha kwamba laini zenye shida ndani ya Morogoro ni Turiani, Kilosa, Mikumi na Kilombero na wamejipanga kuzifanyia kazi.

Mwenyekti wa wafanyabishara Turiani, Erondy Malekia amesema, wao kama wakazi na wafanyabiashara wa eneo la Turiani wamekuwa na tatizo la kukatika kwa umeme kwa muda mrefu.

Malekia amesema, kuletwa kwa nguzo za zege kutasaidia kumaliza tatizo la umeme lililopo kwa sasa huku akipongeza serikali kwa kuwafikiria.

Naye mkazi wa Turiani, Eliufoo Urasa amesema uamuzi wa Tanesco kuweka nguzo zisizoungua moto utakuwa mkombozi kwao kwa kuwa kwenye maeneo hayo watu wamekuwa wakichoma ambao pia huathiri nguzo.