Tanroads kuwatumia wataalamu, makandarasi wa ndani
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta.
Muktasari:
- Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umesema, matumizi ya maudhui ya ndani katika sekta ya ujenzi itaongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini nchini.
Dar es Salaam. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) umesema matumizi ya maudhui ya ndani katika sekta ya ujenzi itaongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini nchini.
Maudhui ya ndani yanarejelea matumizi ya makampuni ya ndani, wataalamu binafsi, nyenzo zinazopatikana nchini na utaalamu katika kuendeleza miradi ya ujenzi.
“Kutengeneza fursa kwa wananchi wa eneo husika kujipatia kipato kupitia kuajiriwa ni miongoni mwa njia za kupunguza umaskini.
"Mchakato wa kujenga, kuendesha na kutunza miundombinu unatoa fursa kubwa kwa ajili ya kutengeneza ajira na kuna maelewano mapana miongoni mwa Watanzania katika kuongeza fursa hizi,” amesema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mohamed Besta katika mahojiano na Mwananchi.
Besta alisema kutegemea kampuni za kigeni kubuni na kutengeneza vifaa si jambo endelevu, kwani utaalamu unaweza kukoma pindi ujenzi unapokamilika.
Tanroads inasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 36,760.29 ikiwa na jukumu la kuboresha barabara ikiwemo kwenye viwanja vya ndege.
Mwongozo wa Kitaifa wa Maudhui ya Sekta Mbalimbali za Mitaa uliotolewa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (2019) umebainisha kuwa sekta ya ujenzi inayopewa kipaumbele katika kuendesha ajenda ya maudhui ya ndani nchini.
Baadhi ya hatua zinazochukuliwa na serikali kukuza maudhui ya ndani katika sekta ya ujenzi na sekta nyinginezo ni pamoja na kutunga sheria na kanuni zinazohitaji kampuni za ujenzi kuweka kipaumbele cha maudhui ya ndani katika miradi yao, kujenga uwezo wa wataalam wa ndani, kuhimiza kampuni za ndani ya ujenzi na huduma kushindana katika miradi ya miundombinu ya ukubwa na ugumu mbalimbali, na kukuza ubia kati ya kampuni za ndani na nje ya nchi.
Bodi ya Makandarasi (CRB) pia ina utaratibu wa kufadhili kupitia Mfuko wa Msaada wa Makandarasi (CAF), ambao unalenga kuwawezesha wakandarasi wa ndani kupata miradi zaidi.
Hazina hiyo ilidhamini miradi 236 yenye thamani ya jumla ya Sh129.95 bilioni mwaka wa 2022 ili kusaidia makandarasi kwa malipo ya awali ya jumla ya Sh14.78 bilioni, kulingana na bodi hiyo.
Jambo ambalo limesaidia hivi majuzi makandarasi wa ndani na washauri kushinda zabuni za serikali za umma ni kuzingatia upya, uwazi, na usaidizi katika mchakato wa ununuzi.
Kulingana na tovuti ya Statistica, sekta ya ujenzi ilichangia Sh15 trilioni kwenye pato la Taifa kutoka robo ya kwanza hadi ya tatu ya 2021. Mwaka 2020, thamani ya sekta hiyo katika uchumi ilifikia Sh19.4 trilioni ikiwa ni kiwango cha juu zaidi tangu 2015.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zinaonyesha kuwa pato la Taifa la Tanzania limeongezeka hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 85.42 (Sh200 trilioni) kwa mwaka huu 2023 kutoka Dola za Marekani bilioni 69.9 (Sh163.5 trilioni) mwaka 2021.