Tanroads yataja chanzo maji kupita juu ya daraja jijini Mwanza

New Content Item (1)
Maji yakiwa yametwama katikati ya barabara inayoingia kwenye maduka ya soko la Mkuyuni jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

Wakazi wa jijini Mwanza wanaotumia barabara ya Kenyatta inayotoka Mwanza mjini na kupita Kata za Mkuyuni, Butimba, Nyegezi, Mkolani na Buhongwa wamelazimika kusimama kwenye foleni zaidi ya masaa matatu baada ya  mto kufurika kisha maji kuanza kupita juu ya daraja la Mkuyuni.

Mwanza. Wakati watumiaji wa barabara ya Kenyatta jijini Mwanza wakilazimika kutumia zaidi ya masaa mawili kwenye foleni baada ya maji kujaa hadi kupita juu ya daraja la Mto Mkuyuni, Wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza imetaja tabia ya watu kutupa taka taka kwenye mto huo ndiyo chanzo cha maji hayo kujaa.

Mto huo umefurika maji leo Machi 24, 2023 baada ya mvua iliyoanza kunyesha Saa tisa usiku wa kuamkia leo na kukatika Saa tatu asubuhi ikiwaacha watumiaji wa barabara hasa eneo la mkuyuni kusubiri maji yapungue ndiyo wavuke kuendelea na shuguli zao.

Maji hayo yaliyokuwa yakitoka kwenye mto huo na kusambaa hadi barabarani pia yameingia hadi kwenye soko la nafaka la Mkuyuni na kuwaacha wafanyabiashara wakilia kutokana na hasara waliyoipata.

Barabarani pia kulikuwa na vuta nikuvute kati ya madereva kila mmoja akitaka kuwahi safari anayoelekea hivyo kulazimisha kupita magari mengine na kusababisha  msongamano wa magari hasa kwa upande wa magari yanayotoka  mjini kati kuelekea maeneo ya Nyegezi, Malimbe na Buhongwa kuongezeka.

Akiwa kwenye daladala inayofanya safari kati ya Igoma na Nyashishi, Mkazi wa Machinjioni Raila Said amesema amefika eneo hilo tangu Saa 4 asubuhi akielekea stendi ya mabasi nyegezi kwa ajili ya safari ya kwenda Geita lakini hadi Saa sita daladala yao ilikuwa bado kwenye foleni.

“Kilichonisaidia sijakata tiketi naenda kukatia huko huko stendi laasivyo leo ningeachwa na basi kwa sababu nilipanga kuondoka na basi la Saa 7 mchana,”amesema

Mfanyabiashara wa Soko la Mkuyuni aliyejitambulisha kwa jina moja la Mbulu amesema licha ya soko hilo kuwa kero kipindi cha mvua kutokana matope kujaa lakini leo imekuwa kero na kilio kwao baada ya maji kuingia hadi maeneo wanayohifadhia matunda.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mwanza, Ambrose Pascal amesema Serikali inampango wa kuijenga barabara hiyo kwa njia nne ambao utahusisha na daraja hilo.

Ambrose amesema chanzo cha maji kujaa katika mto huo kisha kupita juu ya daraja hilo kinasababishwa na taka taka zinazokusanywa na maji kutoka kwenye makazi ya watu ambazo huziba njia ya maji.

“Kisa cha kujaa maji mara kwa mara na kuleta mafuriko ni takataka zinazosababisha kuziba na taka taka hizo zinasababishwa na wananchi kutupa ovyo na mvua zinaponyesha zinasomba na kusababisha maji kujaa darajani na kuziba,”amesema

Amesema tayari wametoa taarifa kwenye vikao vya Wilaya ya Nyamagana ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kutupa taka ovyo.

“Kwa hiyo matokeo ya wananchi kutupa taka ovyo ndo hayo yanapelekea maji kuziba na kusababisha mafuriko katika daraja letu,”amesema Ambrose