Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania ina uhaba wa wataalamu dawa za usingizi, ganzi 1,200

Rais wa Chama cha Wataalamu wa Dawa za Usingizi na Ganzi Tanzania (Sata), Dk Edwin Lugazia akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.

Muktasari:

  • Takwimu zinaonyesha madaktari bingwa wa dawa za usingizi na ganzi nchini, wapo 85 pekee ambapo ili kutatua changamoto hiyo, nchi inahitaji wataalamu kama hao 1,200 ili kuendana na viwango vya kimataifa vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dar es Salaam. Chama cha wataalamu wa dawa za usingizi na ganzi Tanzania (Sata) kimesema licha ya Serikali kuweka miundombinu ya kutosha katika sekta hiyo, bado kuna chagamoto ya upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi.

Mpaka sasa nchi ina madaktari bingwa wa dawa za usingizi na ganzi 85 pekee, licha ya kuwa na vituo vya afya vya umma 9,610.

Akizungumza jijini Dar es Salaam na Mwananchi,  Jumapili Mei 12, 2024 Rais wa Sata, Dk Edwin Lugazia amesema kuna wataalamu bingwa 85 pekee nchi nzima ambao wanahudumu katika vituo mbalimbali vya umma na binafsi, ili kutatua tatizo hilo wanahitajika 1,200.

Amesema Serikali ya awamu ya sita imeweka miundombinu ya usingizi salama ikiwemo mashine za kutosha pamoja na vitendea kazi na dawa za kutosha, lakini bado nchi inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na watoa huduma wenye weledi wa kutosha.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, wamekuwa wakiendelea kujengeana uwezo katika aina tofauti za upasuaji ikiwa ni pamoja na namna ya kutoa usingizi salama pamoja na kuwahudumia mahututi wanaohitaji dawa za usingizi.

"Kwa sasa vituo vingi vimeongezwa, tunahitaji kukimbizana kufundisha watoa huduma ambao wataweza kutoa huduma hizi kila mahali,” amesema.

Aidha amesema kupitia mkutano wao wa mwaka unaojumuisha washiriki 250, wataweza kujadiliana na kupata mafunzo kwa vitendo na nadharia na kubadilishana mawazo.

"Mkutano huu umekuwa ukifanyika kila mwaka kwa wanataaluma kwa lengo la kujadiliana na kubadilisha uzoefu, sambamba na mafunzo tofauti tofauti pamoja na kujengeana uwezo katika ngazi ya chini mpaka ya juu hadi ya kimataifa,” amesema Dk Lugazia.

Pia amesema kupitia mkutano huo, wanajadiliana changamoto wanazokumbana nazo pamoja na zile zinazolikabili Taifa, katika huduma za kutoa dawa za usingizi na wagonjwa mahututi na kutafuta mbinu mbadala za kukabilina nazo.

Kwa upande wake Katibu wa Sata, Dk John Kweyamba amesema madaktari bingwa ambao wamekuwa wakiingia katika chama hicho, hupata fursa mbalimbali zilizolenga kuwajenga zaidi.

"Wataalamu hawa wanapojiunga na chama chetu wanapata fursa ya kwenda kujiendeleza katika nchi mbalimbali, tulizo na uhusiano nazo kama chama na kuiwezesha nchi kupata wataalamu wabobezi zaidi.”

Hata hivyo amesema licha ya kuwepo kwa changamoto wamekuwa wakizifanyia kazi. “Tunakiri zipo lakini kwa sasa zimepungua kutokana na madaktari bingwa nchini kuongezeka. Tumekuwa tukiwajengea uwezo wengi mikoani hasa wauguzi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi," ameeleza.

Aidha amesema chama hicho kimekuwa kikishirikiana na Serikali katika kupunguza changamoto hizo.

Katika hatua nyingine ametoa wito kwa wataalamu kuzidi kuungana kwa pamoja, ili kujenga Taifa lenye wataalamu bora na kutengeneza afya bora kwa wananchi.