Tanzania kujifunza China dawa ya ukosefu wa ajira

Muktasari:
- Serikali ya Tanzania imesema inajifunza kutoka mataifa yaliyoendelea kukabiliana na changamoto ya ajira, huku ikihakikisha vijana wanajitambua, wanabadilisha fikra pamoja na kutengeneza sera wezeshi na ushirikishwaji ili wazalishwe vijana bora ambao kimsingi ni taifa la kesho.
Dar es Salaam. Serikali imesema inaendelea kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo kujifunza kwa mataifa yaliyoendelea, namna ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana hapa nchini.
Imesema itahakikisha vijana wanajitambua, kuwabadilisha fikra tegemezi, kutengeneza sera wezeshi pamoja na ushirikishwaji ili wazalishwe vijana bora ambao kimsingi ni taifa la kesho.
Hayo, yamebainishwa leo Juni 5, 2024 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alipohudhuria kama mgeni rasmi katika mjadala uliowakutanisha vijana wa China-Tanzania Youth Dialogue uliofanyika katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).
Akielezea kuhusu kupunguza tatizo la ajira linaloikabili nchi, Katambi amesema Tanzania inajifunza kutoka China yenye watu wengi zaidi kiteknolojia, kutafuta fursa ya mitaji, kushirikiana kwenye elimu pamoja na kiuchumi.
"China na Tanzania zina uhusiano wa miaka 60 ya kirafiki, wenzetu wameendelea na wapo zaidi ya watu bilioni 1.3 hivyo tumejifunza na tunaendelea ili kuendelea kunufaika katika uhusiano na mataifa ya nje.
"Wao pia wamepitia changamoto hiyo, tunachojifunza walifanya nini hivyo tunaiga ili kumaliza tatizo hili ikiwemo kushirikiana katika masuala ya elimu ya vijana, kilimo, mifumo ya sayansi, uvuvi, mawasiliano ujenzi, usalama tuone wapi tunashirikiana vipi eneo gani tunasaidiana na wapi tunawaiga," amebainisha Katambi.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo ya kufanya mabadiliko katika sera na sheria, ili kutengeneza mazingira mazuri kwa Watanzania kunufaika na uhusiano wa kitamataifa tulionao.
"Tunahakikisha kijana anajitambua ana wajibu gani katika familia na Taifa kwa ujumla kwa kusikiliza mawazo yao pia kisha tunawaandaa kuwa bora, wasiokuwa wezi wala wanaokula rushwa," amesema Katambi.
Kwa upande wake, Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian amesema lazima vijana wawekwe mbele kwa faida ya kesho kama walivyofanya China.
"Katika maendeleo endelevu lazima wawekwe sehemu sahihi tuwatengenezee uwezo kwa kuwabadilisha kimawazo kwanza."
Katika kushirikiana, Balozi Mingjian amesema mwaka 2023, wanafunzi wa Kitanzania 160 walipata ufadhili wa masomo nchini China, huku akisema kuna vyuo vya China vinavyofundisha Kiswahili, hivyo kuhitaji walimu kutoka Tanzania.
Akitoa ushauri , amesema vijana lazima waishi kwa kusimamia ndoto zao, kujituma ili kuwa bora katika maisha ya kesho.
Wakizungumza vijana hao wamesema kitendo cha kuiga mataifa yaliyoendelea, kitaleta tija lakini kwa kubadilisha mfumo mzima wa ushirikishwaji na utoaji ajira kwa vijana hapa nchini.
"Lazima Serikali itilie mkazo kwetu tangu wadogo ili tunapokua tunajua mambo yako vipi ili tukikutana na ukosefu wa ajira tusishangae," amesema Malcom Mhama.
Kijana mwingine Khadija Abdi, amesema vijana lazima wajitume ili kuepuka vishawishi ambavyo ni sehemu ya changamoto wanazokutana nazo, ikiwemo kuacha maadili ya Kiafrika na kuiga ya nje.
Aidha, amesema lazima vijana wa Kitanzania wachape kazi kama walivyo Wachina.
"Pia, Serikali ikazie suala la rushwa kuwe na adhabu kali. Kuhusu kubadilisha fikra, serikali peke yake haiwezi ni mtu mwenyewe aanze kwa kujibadilisha," amesema Khadija.