Tanzania yapewa mkopo wa Sh361 bilioni

Katibu mkuu wizara ya fedha na mipango,Emmanuel Tutuba akizungumza jijini Dodoma kwenye hafla ya utilianaji saini wa mkataba wa mkopo wa masharti nafuu na Shirika la Maendeleo la nchini Ufaransa (AFD) wenye thamani ya Sh361.71 bilioni kwa ajili ya mradi wa kuzalisha umeme wa jua. Picha na Jonathan Musa

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu na Shirika la Maendeleo la nchini Ufaransa (AFD) wa Sh361.71 bilioni kwa ajili ya mradi wa kuzalisha umeme wa jua.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu na Shirika la Maendeleo la nchini Ufaransa (AFD) wa Sh361.71 bilioni kwa ajili ya mradi wa kuzalisha umeme wa jua.

Mkataba huo umesainiwa leo Ijumaa Juni 11, 2021 na katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na mwakilishi wa AFD nchini,  Stephanie Mouen.

Tutuba amesema mradi huo ambao utatekelezwa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ni wa mwaka mmoja unatarajiwa kuanza Machi mwaka 2022 na kukamilika Machi mwaka 2023.

“Lengo la mradi huu ni kujenga mitambo ya kuzalisha umeme wa jua kiasi cha megawati 150 katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga. Mradi huu unatarajiwa kuwa na awamu mbili ambapo awamu ya kwanza utaweza kuzalisha megawati 50,”amesema.

Amesema pia sehemu ya fedha za mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) itatumika kuboresha gridi ya Taifa kuifanya kuwa ya kisasa kuweza kujumuisha umeme wa nishati jadidifu zenye muda maalum na kupunguza upotevu wa umeme.