Tanzania yatajwa kushirikisha jamii uhifadhi

Muktasari:

  • Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zinatekeleza dhana ya ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi wa kivitendo kwa kutoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kusimamia rasilimali za wanyamaporiArusha. Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zinatekeleza dhana ya ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi wa kivitendo kwa kutoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika kusimamia rasilimali za wanyamapori

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Septemba 23, 2022 na Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii, Juma Mkomi  wakati akifungua warsha ya kupitia na kuthibitisha mkakati wa usimamizi na uendeshaji wa maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs)  iliyofanyika jijini Arusha.

Amesisitiza kuwa WMAs ni kinga (buffer) muhimu kwa maeneo ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu.

Mkomi amesema bila WMAs changamoto za kiuhifadhi zitaathiri moja kwa moja Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Hifadhi ya Ngorongoro na Mapori Tengefu

Kutokana na umuhimu huo, Mkomi ametoa wito kwa  wadau wa Uhifadhi nchini kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuendeleza WMAs ili kuziwezesha kujisimamia na kujiendesha.

Ameongeza kuwa kupitia ushirikishwaji huo jamii zimekuwa zikinufaika na matunda yatokanayo na shughuli za uhifadhi katika maeneo yao kwa kujiletea maendeleo na huduma za kijamii ikiwamo shule na zahanati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya  Wanyamapori, Dk Maurus Msuha amesema toka kuanzishwa kwa dhana ya WMAs jamii imekuwa ikishiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori hali inayopelekea ulinzi kuwa madhubuti

Amesema kufuatia hali hiyo  maeneo ya WMAs yamekuwa ya kuvutia shughuli mbalimbali za uwekezaji  kwa ajili ya utalii wa picha, uwindaji wa kitalii na uwekezaji kwa ajili ya hewa ya ukaa

Akizungumzia manufaa ya ushirikishwaji huo, Dk Msuha amesema katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2021 jumla ya jumuiya 15 zenya mikataba ya uwekezaji katika uwindaji wa kitalii zimeweza kukusanya jumla ya Sh4.91 bilioni ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ufadhili wa wanafunzi kusoma katika vyuo vikuu.