Tari yabaini maharage yenye virutubisho muhimu kwa lishe
Muonekano wa shamba la mbegu mpya ya maharage aina ya TARIBEAN6 yenye uwezo wa kuongeza nguvu za kiume baada ya kufanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)
Muktasari:
- Mbegu hiyo imeanza kutumika rasmi mwaka 2024 baada ya mafanikio ya tafiti ya uzalishaji wa maharage ya Jesca mwaka 1997 ambayo yalileta tija na fursa ya kiuchumi kwa wakulima.
Mbeya. Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) imesema mbegu mpya ya maharage aina ya Taribean 6 ina kiwango kikubwa cha protini pamoja na madini ya chuma na zinki, virutubisho vinavyochangia kuboresha lishe na afya ya walaji, hususan wanawake wajawazito na watoto.
Mbegu hiyo ilianza kutumika rasmi mwaka 2024 baada ya kukamilika kwa utafiti, ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio ya maharage aina ya Jesca yaliyofanyiwa utafiti mwaka 1997.
Mtafiti Mwandamizi wa Kitengo cha Maharage wa Tari-Uyole, Reinfrid Maganga amesema taasisi hiyo imeongeza uzalishaji wa mbegu za Jesca na Taribean 6 kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya wakulima na watumiaji.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Julai 9, 2026, Maganga amesema uzalishaji wa mbegu umeongezeka kutoka tani mbili msimu uliopita hadi tani nne, msimu huu.
Amesema utafiti uliofanywa na Tari unaonyesha aina hizo za maharage zina kiwango kikubwa cha protini, madini ya chuma na zinki, ambavyo ni muhimu katika kuboresha lishe na afya.
Maganga amesema, Tari inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha wananchi wanapata maharage yenye ubora wa lishe.
Mikakati ya Tari
"Tunaendelea kuwafikia wananchi na wakulima kwa elimu kuhusu faida za maharage haya. Yana protini nyingi pamoja na madini ya chuma na zinki ambavyo ni muhimu kwa afya na lishe," amesema.
Tofauti ya Jesca na Taribean 6
Amefafanua kuwa maharage ya Jesca yalitokana na utafiti uliofanyika mwaka 1997, wakati Taribean 6 ilianza kutumika mwaka 2024 baada ya kufanyiwa maboresho yaliyolenga kuongeza tija ya uzalishaji na uwezo wa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema aina zote mbili zina kiwango kikubwa cha protini, madini ya chuma na zinki, lakini Taribean 6 imeboreshwa zaidi ili kutoa mavuno mengi na kustahimili mazingira mbalimbali ya uzalishaji.
Maganga amewashauri wananchi, hususan wazazi, kujumuisha maharage hayo katika mlo wa familia ili kuboresha lishe, huku akiwataka wakulima kutumia mbegu bora na kupima afya ya udongo ili kuongeza uzalishaji.
Wafanyabiashara wazungumzia mahitaji
Mfanyabiashara wa maharage ya jumla na rejareja, Ndimiake Francis amesema maharage ya Jesca yanaendelea kuwa na soko kubwa kutokana na mahitaji ya walaji.
"Kwa wastani nauza maharage yenye thamani ya kati ya Sh200,000 na Sh300,000 kwa siku. Bei yake ni kubwa kuliko mengine na wakati mwingine huadimika kutokana na mahitaji kuwa makubwa," amesema.
Naye Sebastian Joseph amesema alianza kutumia maharage ya Jesca baada ya kuyafahamu kupitia Maonyesho ya Nanenane mwaka 2020.
"Awali nilidhani ni hadithi, lakini baada ya kuyatumia niliona tofauti kwa uzoefu wangu binafsi, ndiyo maana nimeendelea kuyatumia," amesema.