Taso yaiomba Serikali kuwarejeshea majengo, mabanda

Moja ya jengo ambalo liliikuwa likisimamiwa na Chama cha Wakulima Tanzania(TASO) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliyojengwa kwenye viwanja vya maonyesho ya wakulima vya John Mwakangale jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

Chama cha Wakulima Tanzania (Taso) kimeiomba Serikali kurejesha umiliki wa majengo na mabanda ya maonyesho ya wakulima Nanenane katika viwanja  vya John Mwakangale jijini Mbeya baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani  kuwarejeshea  usajili uliofutwa  tangu mwaka 2017.

Mbeya. Chama cha Wakulima Tanzania (Taso) kimeiomba Serikali kurejesha umiliki wa majengo na mabanda ya maonyesho ya wakulima Nanenane katika viwanja  vya John Mwakangale jijini Mbeya baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani  kuwarejeshea  usajili uliofutwa  tangu mwaka 2017.

Akizungumza na Mwananchi   leo Jumapili Machi 20, 2022 Katibu wa Taso, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ramadhani Kiboko amesema awali Serikali iliwafutiwa usajili na maonyesho hayo kusimamia na Serikali za mikoa kutokana na kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa Taso ngazi za juu kuonyesha ukaidi



Kiboko ameeleza sababu za kuomba kurekeshewa umiliki wa mabanda na kushirikishwa kuendelea kusimamia maonyesho ya  Nanenane  kuwa ni  kuendeleza kutoa elimu ya kisera kwa wakulima katika sekta ya uvuvi, ufugaji na kilimo ambayo wameikosa tangu mwaka 2017 .

''Uwepo wa  Chama cha Wakulima Tanzania (Taso) Nyanda za Juu Kusini ni kuwaunganisha  kupata elimu ya uzalishaji na ufugaji, kikubwa tunashukuru Wizara kwa kurejesha  usajili kwani kwa kipindi chote baada ya kufutiwa tumeyumba na kupoteza mwelekeo jambo lililokuwa likisababisha wanachama kukata tamaa '' amesema.

Mwenyekiti wa Taso Kanda ya Nyanda za Juu,  Crispin Mtono, amesema kuwa wamepigania kurejeshwa usajili  lakini cha kushangaza bado mali za  chama yakiwepo majengo  zinashikiliwa na Serikali na sasa wanasubiri taarifa za  Wizara  ili  warejeshewe mali na kushiriki katika maonyesho ya wakulima Nanenane Kanda.

''Suala la mali ni kama limekwisha ni kwa kuwa tumefuatilia tumeelezwa watalizungumza kwenye vikao vya maandalizi ya Nanenane mwaka huu na kutuhakikishia kuwa yatakuwepo kwa sasa tunasubiri maelekezo ya Serikali''amesema.

Mwanachama wa Taso, Fatma Ismail amesema wanaishukuru Serikali kwa uamuzi sahihi wa kuwarejeshea usajili kwani itakuwa chachu ya kuendelea kuwakutanisha wakulima na kubadilishana uzoefu wa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.