TCC yapongeza Serikali kuweka mazingira ya biashara

Muktasari:
- TCC Plc yaipongeza Serikali kwa kuweka mazingira ya kuaminika na rafiki katika masuala ya biashara, huku wakiweka rekodi ya mauzo ya mwaka 2022.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Tanzania Cigarette Public Limited TCC Plc, Takashi Araki ameipongeza serikali kwa kuweka mazingira ya kuaminika na rafiki katika biashara ya tumbaku.
Araki ameyaeleza hayo katika taarifa yake wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa na wadau wa kampuni hiyo, jijini hapa, akisema anafarijika kuona motisha inayotolewa na serikali kwa matumizi ya tumbaku inayopatikana nchini na kuelezea juhudi zao katika kutunza mazingira.
“Tumefanya juhudi nyingi za kulinda mazingira, kufanya kazi kwa uwajibikaji, na kuhakikisha utawala bora, ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika miradi ya nishati ya jua, maji na usimamizi wa taka,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TCC Plc Paul Makanza amesema amefarijika kuona kampuni imeweka rekodi ya mauzo ya mwaka 2022, kutokana na mbinu za kina na mkakati zilizowekwa pamoja na ushirikiano thabiti ndani ya kampuni.
“Kumekuwa na ukuaji imara ambao umepelekea mtiririko thabiti wa fedha za uendeshaji na ongezeko la thamani ya wanahisa kwa mwaka wa tatu mfululizo,” amesema.
Ameongeza kwa kusema “Kwa upande wa matokeo yao ya fedha, anafuraha kuripoti kwamba faida yao kabla ya kodi (PBT) kwa mwaka iliongezeka kwa asilimia 23.7 ambayo ni sawa na Sh106.8 bilioni ikilinganishwa na Sh86.3 bilioni za mwaka 2021.
Amesema ingawa kodi ya mapato iliongezeka kwa asilimia 40.2 kutokana na marekebisho ya kodi ya mapato ya miaka ya awali, faida baada ya kodi (PAT) bado ilionyesha ongezeko kubwa la asilimia 16.2 hadi kufikia Sh 69.2 bilioni kutoka Sh59.6 bilioni mwaka wa 2021.
Ameeleza kwamba ukuaji huo wa faida ulichangiwa na ufanisi sahihi wa kiutendaji na usimamizi mzuri wa gharama.
Hata hivyo kulingana na taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji na Meneja Mkuu, kiasi cha ndani kilifikia bilioni 5.7 katika kipindi hicho, ambacho ilikuwa ni ongezeko la asilimia 10 kutoka 2021.
Tanzania Cigarette Public Limited Company (TCC Plc) ni kampuni ya sigara nchini Tanzania ambayo inatengeneza, kusambaza, na kuuza sigara chini ya chapa zifuatazo: Camel, Winston, Winston Club, Embassy, Portsman, Sweet Menthol, na Crescent & Star.
Ilianzishwa mwaka 1961 kama East African Tobacco, ilitaifishwa mwaka 1975 na baadaye kubinafsishwa wakati serikali ilipouza sehemu yake ya udhibiti.