Tembo wafungwa ving’amuzi Hifadhi ya Mkomanzi

Mkurugenzi wa utafiti na mafunzo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Dk Edward Kohi (aliyevaa miwani) akishirikiana na wataalamu wengine, kumfunga Tembo King'amuzi, ili kufuatilia mienendo ya wanyama hao na kuwadhibiti kutoka hifadhini kuvamia katika makazi ya watu na kusababisha uharibifu na Vifo. Picha na Florah Temba
Muktasari:
- Kifaa hicho kinafungwa kwa tembo jike ambaye ni kiongozi wa kundi na hivyo kusaidia kutambua mwenendo wa kundi husika linapoanza safari ya kutoka hifadhini kuelekea kwenye maeneo ya makazi na mashamba ya watu kufanya uharibifu.
Same. Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa kushirikiana na Shirika la Tanzanian Elephant Foundation (TEF) imeanza kufunga vifaa maalumu vya mawasiliano (ving'amuzi) kwa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ili kubaini mienendo yao, hatua ambayo itasaidia kupunguza migongano baina ya wanyama hao na binadamu.
Kifaa hicho kinafungwa kwa tembo jike ambaye ni kiongozi wa kundi na hivyo kusaidia kutambua mwenendo wa kundi husika linapoanza safari ya kutoka hifadhini kuelekea kwenye maeneo ya makazi na mashamba ya watu kufanya uharibifu.
Akizungumza wakati wa kufunga ving'amuzi hivyo kwa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Edward Kohi amesema mipango ya serikali ni kuhakikisha wanapunguza au kumaliza migongano baina ya wanyamapori na binafamu ambayo imekuwa tatizo kubwa katika maeneo ya kuzunguka maeneo ya hifadhi.
"Migongano ya wanyamapori hasa tembo na binadamu ni kilio kikubwa na mipango ni kuhakikisha tunaondoa au kupunguza migongano hiyo kwa kuwafunga tembo vifaa maalumu ambavyo vitatuwezesha kuwafuatilia na kuwadhibiti pindi wanapoondoka hifadhini," amesema.
"Kwa kuweka vifaa hivi itatusaidia kufahamu makundi ya tembo wanaoenda vijijini na yanapitia njia na maeneo yapi ili serikali na wananchi kujipanga kuwadhibiti na kuwarudisha hifadhini kwa haraka," amesema.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Emanuel Moirana amesema hatua hiyo italeta ufanisi mkubwa wa namna ya kukabiliana na migongano baina ya binadamu na Wanyamapori aina ya tembo ambao wamekuwa tishio kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo hususani Wilaya ya Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro na Lushoto mkoani Tanga ambako kuna kilio kikubwa.
"Tutafunga ving'amuzi nane katika Wilaya ya Same, Mwanga na Lushoto ambako ndiko kuna kilio kikubwa cha uvamizi wa tembo katika maeneo ya makazi ya wananchi na tutafunga makundi ya tembo yaliyoko pembeni mwa hifadhi na tembo walioko nje na lengo kubwa ni kuweza kubaini mienendo ya tembo na kuwafuatilia wanapoingia katika makazi ya wananchi ili kuwarudisha kabla hawajaleta madhara," amesema.
"Ni kweli kabisa kumekuwa na juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanyika katika kuwarudisha wanyama hawa lakini unapowafukuza au kuwarudisha usiku saa nyingine uhakika wa maeneo wanayoenda inakuwa siyo sawa, lakini kwa sasa vifaa hivi vitaongeza ufanisi kuhakikisha wanyama hawa wanarudishwa hifadhini na baadae pia tutaweza kuwafuatilia wanyama hawa wanapotoka hifadhini ili askari waweze kuchukua juhudi mahususi za kuwarudisha kabla hawajaenda maeneo ya wananchi," amesema.
"Hili limekuja muda mwafaka kwa sababu kwa sasa wananchi wanakaribia kuvuna sasa tukiongeza juhudi kipindi hiki tutasaidia kuokoa mazao ya wananchi ili kuweza kuvuna na kuondoa changamoto iliyokuwepo," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanian Elephant Foundation (TEF), Lameck Mkumburo amesema kwa kushirikiana na serikali watahakikisha wanatatua changamoto ya migogoro ya wananchi na wanyamapori ambayo imekuwa ikisababisha uharibifu wa mazao pamoja na kudhuru na hata vifo vya wananchi.
"Mradi huu unatekelezwa katika maeneo ya kuzunguka Hifadhi ya ya Taifa ya Mkomazi na unagharimu zaidi ya Sh100 milioni na kifaa hiki anafungwa tembo kiongozi katika kundi na tunaamini hili litawezesha kuwafuatilia tembo na kuwadhibiti kwa haraka kabla ya kuingia katika makazi ya wananchi na kuleta uharibifu," amesema.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Same, Abdillah Mnyambo amesema ufungaji wanyama hao vifaa vya mawasiliano vya kuwezesha kufuatilia mienendo yao ni faraja katika kuhakikisha tatizo la uvamizi wanyana hao katika makazi ya watu linamalizika.
"Hii ni faraja kwani uvamizi wa wanyama pori aina ya tembo kwa wananchi ni tatizo kubwa na kimekuwa kilio cha muda mrefu, sasa tunaamini kwa hatua hii wanaweza kuwadhibiti wanyama hawa na kumaliza tatizo hili la migongano ya Tembo na binadamu," amesema.