Tembo wawa tishio Chemba

Tembo wawa tishio Chemba

Muktasari:

  • Wakazi wa Vijiji vya Itolwa na Jangalo wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma wamedai kuishi kwa hofu kutokana na kujeruhiwa na tembo.

Dodoma. Wakazi wa Vijiji vya Itolwa na Jangalo wilayani Chemba Mkoa wa Dodoma wamedai kuishi kwa hofu kutokana na kujeruhiwa na tembo.

Wakizungumza na Mwananchi juzi, wakazi hao walisema mbali na kujeruhiwa, pia tembo wanakula mazao shambani.

Kuanzia Juni mosi hadi sasa zaidi ya matukio 10 ya kujeruhiwa na tembo yamejitokeza katika vijiji hivyo.

Juma Ndwata, mkazi wa Jangalo alisema tembo hao walifika katika shamba lake na kuwadhuru watu wanne waliokuwa shambani.

Alisema walitoa taarifa Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini wanaona kimya hadi sasa.

“Giza likiingia kila mmoja ana wasiwasi, anajua nini kitatokea maana tembo wanapenda mbaazi, sasa huku kwetu ni shida sana,” alisema Ndwata.

Alisema katika eneo la Ipala kumekuwa na matukio zaidi kwa kuwa kila siku lazima tembo wafike na kujeruhi watu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlongia Kata ya Mlongia, Juma Sambala alikiri kuwapo kwa matukio hayo, akisema watu wawili wamejeruhiwa, mmoja amelazwa katika Kituo cha Afya cha Hamai na mwingine Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.

Mwenyekiti huyo aliwataja waliojeruhiwa ni Masasi Augustino ambaye yupo Hamai na Mzee Jombe aliyelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kondoa.

Ofisa Wanyamapori Wilaya ya Chemba, Ahmed Kimolo alisema tayari wameshafika katika vijiji hivyo na kuwaondoa tembo hao wanaotoka katika Pori la Akiba la Mkungunero.

Alisema pia tembo hao wanatoka katika Hifadhi ya Tarangire na hiyo imekuwa ni njia yao.

Matukio ya tembo kujeruhi wananchi na kuharibu mazao yamekuwa yakiripotiwa mara kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini, huku waathirika wakisema wamekuwa wakipata hasara.