TMDA yachunguza madhara ya aliyechomwa sindano, kuungua vidole

Muktasari:

  • Kufuatia madai ya mwananchi aliyelalamika kupitia mitandao ya kijamii kuugua vidole baada ya kuchomwa sindano ya mkono kwenye duka la dawa muhimu, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imeanza uchunguzi wa tukio hilo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imesema, inafanya uchunguzi wa tukio la mwananchi aliyedai kuchomwa sindano katika duka la dawa muhimu na kuungua vidole vya mkono wa kushoto.

 Tukio hilo lilisambaa kwenye mitandao ya kijamii Mei 8, 2023 ambapo Ester Mkombozi alionekana kwenye picha mjongeo akidai vidole vyake vya mkono wa kushoto vimeungua baada ya kuchomwa sindano katika duka la dawa alilolitaja kwa jina la El-Shadai Medics lililopo Kata ya Ngulelo jijini Arusha.

Kupitia video hiyo, jana Mei 11, 2023 TMDA kwenye taarifa iliyotolewa kwa umma ilieleza kwamba, baada ya kuiona video hiyo ilifuatilia na kumpata Easter na tayari wameanza kufanya uchunguzi wa kina wa tukio hilo na itatoa taarifa kamili.

"TMDA ilifanya ufuatiliaji wa haraka wa taarifa hizo kwa kushirikiana na ofisi ya  Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Baraza la Famasi na Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru  na kufanikiwa kuonana na Ester akiwa Hospitali ya Mount Meru," imeeleza taarifa hiyo. 

Kutokana na uchunguzi unaoendelea, TMDA imewataka wananchi kuwa watulivu na taarifa kamili itatolewa kuhusu tukio hilo.