TPA yaeleza umuhimu bandari ya Bagamoyo

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa

Muktasari:

Bandari ya Bagamoyo inayotarajiwa kujengwa ni muhimu kama Tanzania inataka kujenga uwezo kabla mahitaji hayajaongezeka, mamlaka ya bandari ilisema jana na kuondoa hofu kwamba mradi huo unaweza kuathiri bandari zilizopo.

Dar es Salaam. Bandari ya Bagamoyo inayotarajiwa kujengwa ni muhimu kama Tanzania inataka kujenga uwezo kabla mahitaji hayajaongezeka, mamlaka ya bandari ilisema jana na kuondoa hofu kwamba mradi huo unaweza kuathiri bandari zilizopo.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa aliwaambia wahariri jana kuwa kutokana na umuhimu wa kuwa na bandari inayoweza kuhudumia ipasavyo meli kubwa ambazo haziwezi kuhudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam, waliamua kuendelea na mradi huo licha ya kuwaondoa wawekezaji waliokuwa wakifanya mazungumzo na Serikali siku za nyuma.

“Kwa kweli, hatuzungumzii tena kuhusu mradi mpana wa dola 10 bilioni kwa sababu baadhi ya watu watakuwa wakiuliza pesa hizi zote zitatoka wapi. Tunazungumzia tu kipengele cha maendeleo ya bandari kwa ajili ya mradi mkubwa wa kanda maalumu ya kiuchumi ya Bagamoyo,” alisema na kuongeza:

“Tunaweza hata kuamua kuanza na gati moja au gati mbili. Kama Serikali, hatuwezi kukaa tu kwa sababu bado hatujapata wawekezaji wa kushirikiana nao”.

Alisema lengo lilikuwa ni kuendeleza bandari za Tanzania kwa kuiga jinsi bandari za Singapore na Jebel Ali katika Falme za Kiarabu zilivyokuwa zikisaidia shughuli za kiuchumi na kupunguza bei kwa watumiaji wa mwisho.

Mwaka 2013, Serikali ilitia saini mkataba na Kampuni ya China Merchants Holdings International (CMHI) na Mfuko Mkuu wa Hifadhi wa Taifa wa Oman kujenga bandari kama sehemu ya Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (BSEZ).

Mpango wa kujenga BSEZ ulianza mwaka 2004 kama sehemu ya mpango wa Tanzania wa mwaka 2020 ambao ulitaka kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda huu na ambayo ilikadiriwa kuwa mradi mzima ungegharimu dola 10 bilioni (takribani Sh23 trilioni).

Hata hivyo, uongozi wa awamu ya tano wa hayati John Magufuli ulitupilia mbali mradi huo ukisema ulikuwa wa kinyonyaji na usiofaa.

Lakini alipozungumza na wafanyabiashara Juni mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema uongozi wake umeanza upya mazungumzo ya kufufua mradi huo. Sambamba na hilo, Mbossa alisema jana kuwa kutokana na kutarajia kupanda kwa mizigo, TPA haikuwa na la kufanya zaidi ya kuanza maandalizi ya utekelezaji wa miradi ya bandari ya Bagamoyo (Pwani), Chongoleani (Tanga) na Kisiwa-Mgao (Mtwara).

Alisema Serikali imefanya maboresho kadhaa katika bandari zake ambazo zimesababisha kuongezeka kwa uhudumiaji wa mizigo katika bandari zote kuu. Kwa mfano, uwezo wa kuhudumia mizigo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara unakadiriwa kufikia tani milioni 27.5 katika mwaka wa fedha 2024/25.

Hata hivyo, TPA inatarajia kuwa bandari zake zitapokea tani milioni 26.1 za shehena ya mizigo katika mwaka wa fedha 2024/25.

“Hii ina maana kwamba kiasi cha mizigo tunachotarajia kupokea kitakuwa asilimia 94.9 ya uwezo wa bandari zetu,” alisema.

Kwa Bagamoyo, lengo litakuwa ni kuwa na bandari yenye kina kirefu zaidi inayoweza kuhudumia meli zinazohitaji kina cha zaidi ya mita 17, ili kukalia. Kinyume chake, Bandari ya Dar es Salaam ina kina cha takribani mita 14.5.