Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TPHPA kufanya utafiti wadudu walioshambulia mazao ya wakulima Mbozi

Kaimu Meneja Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Nyanda za Juu Kusini (aliyevaa fulana nyeupe) Emmanuel Mausa akizungumza kwenye moja ya shamba la mkulima wilayani Mbozi.

Muktasari:

Kaimu Meneja wa TPHPA Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Mausa akizungumza leo Jumatatu Aprili 22, 2024 amesema wamefika Kijiji cha Ikomela wilayani Mbozi  kwa lengo la kuchukua sampuli ya mdudu

Songwe. Baada ya kubainika uwepo wa wadudu wanaoharibu na kushambulia mazao katika Kijiji cha Ikomela wilayani Mbozi, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti Viuatilifu Tanzania (TPHPA) wamefika kufanya utafiti.

Kaimu Meneja wa TPHPA Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Mausa akizungumza leo Jumatatu Aprili 22, 2024 amesema wamefika kijijini hapo kwa lengo la kuchukua sampuli ya mdudu huyo ambaye watamuingiza maabara kwa uchunguzi zaidi na kupata suluhisho la nini cha kufanya.

Mwananchi wiki iliyopita iliripoti juu ya mashamba ya wakulima kuathiriwa na mdudu huyo aliyetajwa kwa jina la Garden white Grubs.

"Tumekuja kuangalia ukubwa wa tatizo na ni  kweli wadudu wapo, tumechukua sampuli ili tukafanye utafiti na kujua ni aina gani ya lava anayezaliwa eneo hili,” amesema Mausa.

Amesema wakishatambua aina ya mdudu huyo, itawarahisishia kutambua viuatilifu vitakavyomuangamiza na wataviainisha ili kuwajulisha wananchi wa maeneo yaliyoathirika.

"Kutokana na changamoto ya wadudu kushambulia mizizi ya mazao na hatimaye kunyauka, tukishamaliza tafiti tutawaletea viuatilifu vya aina mbili ambavyo ni viuatilifu vya mfumo ambavyo hupuliziwa mapema kabla ya mvua kuanza kunyesha, hiki huteketeza mayai, na viuatilifu vingine tutakavyovileta kwa wakulima ni vya mguso,” amesema.

Mausa amesema viuatilifu hivi hupuliziwa kwenye mmea na mdudu akitaka kula majani au mizizi yake hufa,” amesema.

Ofisa Kilimo Wilaya ya Mbozi, George Nipwapwacha amesema kutokana na kilio cha wakulima wa Kijiji cha Ikomela na vijiji jirani ndani ya Kata ya Kilimampimbi na Ihanda, watafanya pia tathimini kwenye maeneo hayo  ili kupata takwimu sahihi za maeneo yaliyoathiriwa.

Rubeni Msomba  ambaye ni miongoni mwa wakulima ambao mashamba yao ya kahawa yameshambuliwa,  amesema amefarijika baada ya kutembelewa na watalaamu kutoka TPHPA.

“Tunawaomba watalaamu watuletee haraka majibu ya wadudu hawa ili na sisi tuanze kuzalisha kwa faida, huu ni mwaka wa nne tunasumbuliwa na wadudu hawa,” amesema Ruben.

Mkulima Onesmo Kabungo amesema wadudu hao  wamewasumbua kwa muda mrefu sasa licha ya kutoa taarifa za mara kwa mara kwa wataalamu wa kilimo, lakini safari hii ndiyo kilio chao kimesikika.

Hata hivyo, wakulima hao wameiomba TPHPA kuwaletea majibu mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa kilimo wa 2024/25.