Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trafiki matatani kwa madai ya kudhalilisha Jeshi la Polisi

Muktasari:

  • Awali video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii leo Januari 15, 2025 ikiwaonyesha trafiki wawili, wa kike na wa kiume wakipokea vitu vilivyosadikiwa kuwa ni fedha.

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa daladala waliokuwa wamewakamata.

Taarifa ya kukamatwa kwa askari hao wa usalama barabarani (trafiki) zimetolewa leo ikiwa imepita miezi sita, tangu Mwananchi liliporipoti mfululizo wa habari kuhusu malalamiko ya madereva wa daladala kusumbuliwa na polisi kwa kuombwa fedha kila wanapokamatwa.

Kabla ya taarifa ya kukamatwa kwa askari hao, video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii leo Januari 15, 2025 ikiwaonyesha trafiki wawili, wa kike na wa kiume wakipokea vitu vinavyodhaniwa kuwa fedha kutoka kwa ama madereva au makondakta wa daladala zilizosimamishwa na kisha kuwaruhusu kuendelea na safari eneo la Vingunguti, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema wamewakamata polisi hao na wapo mahabusu.

Muliro amesema wamewakamata askari hao kwa kuwa wamefanya vitendo visivyo vya maadili ambavyo vinachafua taswira ya Jeshi la Polisi.

“Kwenye picha ile wanaonekana askari wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume, wakati wa kutekeleza majukumu yao wakifanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ya Jeshi la Polisi na kuchafua taswira ya jeshi na Serikali kwa ujumla.

“Askari hao tayari wamekamatwa, wapo mahabusu na hatua kali za kinidhamu za mashtaka ya kijeshi zimeanza kuchukuliwa kabla ya hatua nyingine za kisheria zitakazoamuliwa kuchukuliwa dhidi yao," amesema bila kuwataja majina askari hao.

Kamanda Muliro amesema jeshi hilo halitavumilia vitendo vyovyote vya kulidhalilisha au kwenda kinyume nalo.

Katika uchunguzi wa Mwananchi uliofanyika Julai 2024, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhan Ng’anzi alikiri kusikia malalamiko ya madereva na makondakta kuhusu vitendo vya kuombwa fedha, akisema jeshi hilo liko makini.

Hata hivyo, alisema kuna ugumu wa kupambana na vitendo hivyo unaosababishwa na kukosekana ushahidi wa moja kwa moja, ambao kimsingi ndiyo utakaomtia mtendaji hatiani.

“Inaonekana kama pande zote mbili zina masilahi kati ya mtoa rushwa na mpokeaji, kwa sababu wanajificha inakuwa ngumu kupata ushahidi,” alisema.


Uchunguzi wa Mwananchi

Wakizungumza na Mwananchi katika uchunguzi huo, baadhi ya madereva walisema wanawatumikia wamiliki wa magari na polisi katika kazi yao.

Walieleza huwasilisha kwa wenye magari hesabu ya kati ya Sh80,000 hadi Sh200,000 kwa siku kutegemea ukubwa wa gari na umbali wa safari.

Mbali ya hilo, hutenga fedha kwa ajili ya mafuta na kiasi kinachosalia hugawa fungu kwa ajili ya posho yao na ya trafiki, ili kuwezesha siku kuisha vema.

Bosco Joram (si jina halisi), dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Buyuni Chanika na Ubungo Simu2000 alisema wakati huo, katika kazi yao wanawatumikia wamiliki wa magari na polisi.

“Ukiwa dereva wa daladala Dar es Salaam unawatumikia mabosi wawili; kwanza mmiliki wa gari na pili, trafiki,” alisema.

Joram alisema hutenga kati ya Sh10,000 na Sh15,000 za kuwapa trafiki, akieleza maeneo ambayo hulazimika kuwa makini ni Vingunguti na Kipawa ambako mara nyingi trafiki husimama katika Barabara ya Nyerere. Iwapo akisimamishwa huacha Sh2,000 kwa trafiki aliyemkamata.

“Suala la kutoa hela haliwezi kwisha kwa kuwa usipofanya hivyo wanakuandikia faini. Sasa kama una kosa la kuandikiwa faini Sh30,000 halafu uone ubahili wa kutoa Sh2,000! Hiyo hapana," alisema.

Saleh Kassim, dereva wa daladala kati ya Chanika-Gongo la Mboto alisema trafiki hukubali Sh2,000 kwa kosa lisilozidi faini ya Sh30,000, lakini ukiwa na zaidi ya moja wanakutaka kupeleka gari kituoni.

"Ukikamatwa ndiyo umetoka kuamka au umetoka gereji, unamwambia sina kitu nikirudi nitakucheki. Ukirudi unamalizana naye, ukijidai umesahau anakukamata," alisema akiainisha maeneo ambayo trafiki husimama kuwa ni Videte (Chanika), Magenge, Mapensheni na Shule ya Msingi Pugu.

Kwa wastani alisema hutumia Sh10,000 kwa ajili ya trafiki, kauli iliyoungwa mkono na John Gabriel, anayefanya kazi kati ya Stesheni na Mbande.

Kondakta aliyejitambulisha kwa jina moja la Samson, anayefanya kazi katika daladala la Kigogo –Kivukoni akijibu swali ni kwa vipi askari atajua kwamba alishalipa fedha alisema: “Wanajua magari yote ya njia wanayopangiwa, hivyo kama kituoni wapo watatu, ujue kabisa wanaambiana yule mimi tayari nishachukua, hivyo hawakukamati.”

Nassor Imran, dereva wa daladala kati ya Tegeta Nyuki na Mwenge alisema mapato kwa siku ni kati ya Sh130,000 na Sh180,000 ikitegemea idadi ya abiria na unafuu wa msongamano barabarani.

Alisema Sh100,000 huzipeleka kwa mmiliki wa gari kila siku bila kujali limefanya kazi au la, huku akitenga Sh14,000 kwa ajili ya trafiki barabarani.

Baadhi ya madereva na makondakta wanaofanya safari kati ya Mbezi na Mlandizi walisema ukiacha maeneo mengine kwenye Barabara ya Morogoro, vituo maalumu vya kuacha hela kwa trafiki ni Kibamba kwa Mangi na Magari Saba.

Walieleza kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa sita mchana katika vituo hivyo daladala husimama na kuacha Sh2,000 kwa trafiki wanaokuwapo hapo.

"Huo ndiyo utaratibu, hauwezi kuukwepa kama ni konda au dereva wa daladala, ukishatoa Sh2,000  basi unafanya kazi kwa amani siku nzima, labda itokee tu umefanya kosa," alisema dereva wa daladala, James Peter.

Katika uchunguzi wa Mwananchi kituo cha Kibamba kwa Mangi asubuhi ya Ijumaa Julai 19, 2024 kati ya saa 2:00 na saa 3:00 asubuhi alishuhudia trafiki watatu wakichukua fedha kutoka kwa madereva na makondakta wa daladala zilizotokea Mlandizi kwenda Mbezi.

Baada ya kushusha abiria, kondakta aliyekunja fedha kwenye tiketi, alikwenda upande wa dereva na kumkabidhi trafiki ambaye wakati huo alikuwa akizungumza na dereva.

Kituo cha Magari Saba, siku hiyo ya Ijumaa, Julai 19, 2024 saa 4:00 asubuhi walikuwapo trafiki wawili, mmoja akiwa amevaa koti la bluu na suruali ya kaki.

Dereva wa daladala alipomuona kabla hajasimama alimweleza kondakta kuna ‘kimeo.’

"Huyu (akimaanisha askari aliyevaa koti la bluu) huwa hakubali kupokea Sh2,000 kama wengine,” alieleza dereva huyo katika mazungumzo na kondakta.

Baadaye alisimamisha daladala lingine akapokea Sh5,000.

Dereva aliyejitambulisha kwa jina moja la Rashid alilieleza Mwananchi kwamba trafiki huyo hulazimisha kupewa Sh5,000 hadi Sh10,000 na usipompatia siku hiyo huwezi kufanya kazi kwa raha.

"Tunatoa mara moja kwa siku, ingawa kuna askari wanalazimisha Sh5,000, lakini mara nyingi tunaacha Sh2,000 miaka minne iliyopita ilikuwa ni wajibu kuitoa na trafiki hawakuona aibu kuchukua, kidogo kipindi hiki wanachukua kisirisiri, lakini huwezi kupita asubuhi Magari Saba au Kwa Mangi bila kuacha pesa hiyo," alisema.


Kauli ya Darcoboa

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwaya Lema akizungumzia na Mwananchi wakati huo alisema kama chama hawajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa madereva.

“Hao ni madereva waliosema, inawezekana ni sahihi kwa sababu wao ndio wako kazini, lakini siwezi kukubali wala kukataa kwa sababu hakuna anayesema moja kwa moja,” alisema.