Trafiki yatoa maagizo magari ya kubeba wanafunzi

Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa barabarani (Trafiki), Wilbroad Mutafungwa

Muktasari:

Kikosi cha Usalama wa barabarani (Trafiki), imesema itafanya ukaguzi wa magari yote ya kubeba wanafunzi na shule ambazo zitashindwa kupeleka magari maeneo yaliyoandaliwa kila mkoa hatua zitachukuliwa

Dar es Salaam. Kamanda wa Kikosi cha Usalama wa barabarani (Trafiki), Wilbroad Mutafungwa amesema si suala la hiari kwa wamiliki wa magari ya shule kupeleka magari yao kwa ajili ya ukaguzi bali ni suala linalotambulika kisheria

"Sheria inasema magari ya shule yanatakiwa kukaguliwa mara mbili kwa mwaka, mwanzoni mwa mwezi wa sita na Desemba na pale inapobidi.

Ameyasema hayo leo tarehe 5, Agosti 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam  na kusisitiza katika ukaguzi huo wamejikita kukagua ubora wa bodi ya gari matairi, mifumo ya usukani, breki, kukagua viti pamoja na mifumo mingine ambayo haifanyi kazi katika gari na kuchukua hatua madhubuti

Kamanda Mutashingwa amesema leseni ya dereva lazima iendane na gari analoliendesha kwani magari ya kubeba wanafunzi ni magari kama yalivyo magari mengine.

"Dereva anatakiwa awe na leseni yenye daraja C na leseni hiyo lazima awe ameipata katika vyuo vya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) au VETA," amesema

Amesema madereva ambao watabainika hawana leseni zenye sifa hizo basi hawataruhuisiwa tena kuendesha magari ya wanafunzi.

Pamoja na hayo amesema jeshi la usalama barabarani litaendelea kutoa mafunzo na elimu kwa madereva na wamiliki wa magari ya shule juu ya mambo muhimu ya kuzingatia ili kutimiza usafirishaji salama wa wanafunzi.

Kutoka Baraza la Taifa la Usalama wa barabarani, Mhandisi Yona Afrika amesema kazi yao ni kusimamia usalama wa barabarani, kuweka miongozo na kuangalia sheria zote kuhusu usalama wa barabarani.

Kwa upande wake, Afisa leseni mkoa wa Dar es Salaam, Mansul Ommary amesema katika ukaguzi huo unaofanywa na kikosi cha usalama wa barabarani wao kama Latra wanakagua vibali vyao pamoja na masharti mbalimbali ya leseni .

"Magari yote ya shule lazima yapakwe rangi ya njano pamoja na kuandikwa maandishi yanayoonekana, ikitambulisha kuwa ni magari ya shule," amesema Ommary