TRC yapokea vichwa vitatu, mabehewa 27 ya SGR

Miongoni mwa vichwa vya treni ya umeme ambavyo vimepokelewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kikiwa kinashushwa leo Desemba 30, 2023 katika bandari ya Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania, Michibia Shiwa amesema TRC inaendelea kupokea kwa awamu vitendea kazi kwa ajili ya uendeshaji wa Reli ya Kisasa (SGR) na wanavijaribu kulingana na matakwa ya mkataba.

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC), limepokea vichwa vipya vitatu vya treni za umeme na mabehewa mapya 27 ya abiria na kufanya idadi ya vichwa vilivyopokelewa mpaka sasa kufikia vinne na mabehewa yakiwa 56.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kupokea vifaa hivyo, leo Jumamosi Desemba 23, 2023 jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi wa TRC, Michibia Shiwa, amesema wamenunua vichwa vipya 17 na mabehewa mapya 59 ya abiria kwa ajili ya uendeshaji wa SGR.

"Tunatarajia kwamba mabehewa matatu yaliyosalia yatawasili nchini Februari, 2024 huku vichwa 13 vilivyobaki vitawasili kwa awamu mbili ambapo sita vitawasili Machi 2024 na vichwa saba vitawasili Aprili 2024," amesema Shiwa.

Amesema TRC itaanza kupokea seti ya kwanza kati ya 10 za treni za kisasa (zenye vichwa vya kuchongoka) Machi 2024.

"Tunatarajia kupokea nyingine nane kati ya Mei hadi Oktoba mwaka huo, ambapo kila mwezi zitawasili seti mbili," amesema.

Amesema vichwa vilivyopokelewa, vina mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa.

Shiwa amesema mabehewa hayo ni ya madaraja mawili ambayo ni biashara na uchumi ambapo daraja la uchumi lina mabehewa 13 na kila behewa lina uwezo wa kubeba abiria 45.

"Mabehewa ya daraja la biashara ni 14, kila behewa lina uwezo wa kubeba abiria 78 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa kumuwezesha abiria kusafiri kwa amani na salama," amesema.

Amesema shirika linaendelea kupokea kwa awamu vitendea kazi kwa ajili ya uendeshaji wa reli ya SGR  ambapo zoezi la majaribio ya vitendea kazi hivyo linaendelea kwa mujibu wa mkataba ili kuhakikisha vinaendana na mifumo ya miundombinu iliyojengwa nchini kabla ya kuanza uendeshaji wa kibiashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Selemani Mrisho, amesema wana furaha kuwa sehemu ya kufanikisha kuwasili kwa mabehewa na vichwa hivyo.

"Tunaendelea na kazi yetu ya kupakua mzigo huu. Meli ilifika juzi (Desemba 28, 2024) tulianza kazi siku hiyo hiyo na mpaka leo tayari tumeshusha mabehewa 16, tuna furaha," amesema.