Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tume yabaini Polisi kutesa raia, IGP apewa maagizo

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya uchunguzi mbalimbali kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 na kutoa mapendekezo ya jumla kutokana na chunguzi zilizofanyika. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ametakiwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kutekeleza mapendekezo kadhaa dhidi ya askari na maofisa wanaotuhumiwa kukiuka taratibu za utendaji kazi.

Dodoma. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imebaini ukiukwaji wa haki unaofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia wanaokamatwa na kushikiliwa katika mahabusu za jeshi hilo.

Uchunguzi wa tume umebaini vitendo vya wananchi kupigwa, kufanyiwa ukatili, mateso na kuwasababishia majeraha, ukiukwaji wa sheria katika ukamataji na baadhi ya wanaokamatwa kutopatiwa dhamana.

Kutokana na kadhia hizo, Tume hiyo inayoongozwa na Jaji mstaafu Mathew Mwaimu imemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), kuwachukulia hatua za kinidhamu maofisa na askari wa jeshi hilo waliohusika katika vitendo hivyo na kufuatilia matukio kwenye vituo vya polisi.

Hayo yamebainishwa jana Ijumaa, Julai 19, 2024 jijini Dodoma na Jaji Mwaimu wakati akitoa taarifa ya tume hiyo kwa waandishi wa habari ya mwaka 2022/23 na kuanzia Januari hadi Mei 30, 2024 iliyoangazia masuala mbalimbali mtambuka, ikiwemo migogoro ya ardhi na changamoto kwenye maeneo ya hifadhi.


Jeshi la Polisi

Akigusia uchunguzi kwa jeshi la polisi, Jaji Mwaimu amesema: “THBUB ilithibitisha kutozingatiwa kwa taratibu za kisheria za ukamataji na ushikiliwaji wa watuhumiwa katika mahabusu za Jeshi la Polisi.”

Amesema vitendo hivyo viliambatana na wananchi kupigwa, kufanyiwa ukatili na mateso na kuwasababishia majeraha. Mfano, katika lalamiko la mwananchi kutoka Manispaa ya Morogoro.

“THBUB ilijiridhisha mwananchi huyo alipigwa na kufanyiwa vitendo vya kikatili vilivyomsababishia majeraha akiwa anashikiliwa na askari wa Jeshi la Polisi, mkoani Morogoro,” amesema.

Tukio jingine, Jaji Mwaimu amesema ni lalamiko la tuhuma za askari polisi wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya kumtesa na kumfanyia ukatili mfanyabiashara, ushahidi ulithibitisha mfanyabiashara huyo aliwekwa mahabusu bila kupewa dhamana kwa zaidi ya siku 20.

Amesema mfanyabiashara huyo alifanyiwa vitendo vya ukatili vilivyosababisha majeraha mikononi kutokana na kufungwa pingu wakati akiteswa. Pia alipatikana na kidonda kikubwa sehemu za unyayo wa mguu wa kulia kutokana na kupigwa.

“Pamoja na madhila hayo, mwananchi huyo hakupatiwa matibabu kwa wakati,” amesema Jaji Mwaimu.

Tume pia imebainisha matokeo ya uchunguzi kuhusu tuhuma za askari polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma, ya kutozingatia taratibu za kisheria wakati wa ukamataji na kumshikilia mtuhumiwa na kutompatia dhamana.

“Pia, alifanyiwa vitendo vya kikatili kwa kupigwa na kuteswa,” aliongeza Jaji Mwaimu.

 Aidha, tume ilibaini baadhi ya vituo vya polisi vinatumika mahsusi kwa ajili ya kuwatesa watuhumiwa wakati wa mahojiano kabla ya kuwafikisha katika vituo vingine vya polisi.

Jaji Mwaimu amesema katika uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa na mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro dhidi ya askari polisi kumdhalilisha na kumfungulia kesi, utaratibu wa kisheria hazikuzingatiwa.

Kutokana na uchunguzi huo, tume imependekeza kwa IGP kuhakikisha askari wanapata mafunzo ya mara kwa mara ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ikiwemo mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora ili kuwajengea uweledi katika majukumu yao.

Imemshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi kuweka CCTV kamera katika vituo vya polisi, hususan kwenye kaunta (CRO) zote za vituo hivyo ili kubaini matukio yote yanayoendelea kwa mahabusu na raia wanaofika katika vituo hivyo kwa sababu mbalimbali.

“Mkuu wa Jeshi la Polisi awachukulie hatua za kinidhamu maofisa na askari wa Jeshi la Polisi waliohusika katika vitendo vya kuwapiga na kuwatesa watuhumiwa kama ilivyobainishwa,” amesema Jaji Mwaimu.

Mapendekezo kama hayo yalitolewa pia katika ripoti ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ambayo pia iliangazia masuala mbalimbali, na kutoa mapendekezo matano kwa Jeshi la Polisi.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni; Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayoliwezesha kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo.

Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania ili kutoa taswira kuwa Jeshi la Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi na kubadilisha mitalaa ya mafunzo na mtazamo wa askari wa jeshi hilo ili kutoka katika dhana ya ujeshi kwenda dhana ya kuhudumia wananchi.

Pia, ilitaka Jeshi la Polisi liboreshe mfumo wa ndani wa kushughulikia malalamiko ya wananchi na liimarishe huduma za intelijensia ya jinai na Polisi Jamii na kuanzisha programu za kulisogeza zaidi kwenye jamii.


Kauli ya Polisi

Alipoulizwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime juu ya kilichobainishwa na tume ambapo amesema: "Tumepokea na kukubali ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu kama maoni kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi. Wakati unapoambiwa shati lako ni chafu, unapaswa kulivua na kuliosha kwa sabuni na maji ili kulikatasa.

“Hivyo ndivyo Jeshi la Polisi litakavyofanya ili kushughulikia mapungufu yaliyobainishwa na Tume."

Kuhusu ufungaji wa kamera za CCTV, amesema kazi tayari imeanza kutekelezwa kama sehemu ya maagizo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Jeshi la Polisi kutumia mifumo ya Tehama katika operesheni zake ili kuhakikisha wananchi wanapokea haki zao kwa ufanisi na wakati.

"Jeshi la Polisi pia linatekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki za Binadamu, ikiwa ni pamoja na matumizi ya Tehama katika operesheni zake," amesema.


Kulingana na maelekezo ya Rais na mapendekezo ya Tume, amesema mifumo ya CCTV inaendelea kufungwa katika vituo vipya vya polisi vinavyotarajiwa kuanzishwa.

Kwa mfano, ufungaji umepangwa kwa Kituo cha Polisi Gezaulole, Kigamboni, Mtumba, ofisi mpya za Makamanda wa Polisi Singida, Katavi, Kaskazini Unguja, na Kusini Unguja, miongoni mwa maeneo mengine.

Aidha, amesema kuna ofisi 17 za Mkuu wa Polisi na Vituo vinavyotarajiwa kufunguliwa hivi karibuni, na kamera za CCTV zitakuwa miongoni mwa mifumo itakayofungwa katika vituo hivi.


"Wataalamu wa Tehama wa Jeshi la Polisi tayari wamepanga makadirio ya gharama za ufungaji wa kamera za CCTV katika vituo vya polisi na mifumo ya LAN ili kuwezesha matumizi ya Tehama katika ofisi zote," alisema.


Migogoro ya ardhi

Jaji Mwaimu amesema katika baadhi ya chunguzi zilizofanyika kuhusu masuala ya ardhi tume zimebaini uwepo wa migogoro ya muda mrefu na kusababisha matukio ya uvunjifu wa amani na pia walalamikaji au wananchi kutokuwa wamiliki halali wa maeneo ambayo ndiyo chanzo cha mgogoro.

Amesema uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika shamba la Malonje wilayani Sumbawanga, Rukwa dhidi ya taasisi ya kidini ya Efatha Tume, umebaini hiyo ni mmiliki halali wa shamba hilo lakini tangu amekabidhiwa mwaka 2008 kumekuwa na mgogoro wa mipaka kati yake na wananchi.

Mwenyekiti huyo amesema migogoro hiyo imesababisha matumizi ya silaha za moto na kujeruhi wananchi, hususani katika tukio la Novemba 6, 2023 ambapo wananchi watatu walipigwa risasi.

Tume imeshauri mamlaka mbalimbali za Serikali, Efatha na wananchi kukubaliana kutatua mgogoro wa shamba hilo kwa kupima eneo la ardhi linalobishaniwa na kushauriana na mwekezaji kuwaachia wananchi hao eneo hilo kuendelea na shughuli za kilimo na ufugaji kama njia ya kuleta amani na maenelewano.

Pia katika uchunguzi kuhusu malalamiko ya wananchi wa vijiji vya Komarera na Kewanja dhidi ya mgodi wa North Mara, tume imebaini kwamba mgodi huo ulitwaa ardhi yenye ukubwa wa ekari 652 katika kijiji hicho kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi na uthamini na utwaaji wa eneo husika lilifuata taratibu, uwazi na ushirikishwaji wa pande zote na wananchi ambao maeneo yao yalitwaliwa walilipwa fidia stahiki.

Hata hivyo, amesema tume imebaini kuwepo kwa matukio ya vifo na madhara mbalimbali yanayotokana na mapambano baina ya vijana wanaoishi karibu na mgodi, ambao huvamia mgodi huo na askari wa jeshi la polisi wanauolinda.

Tume imependekeza Wizara ya Madini washirikianne na ofisi ya Rais (Tamisemi) pamoja na uongozi wa mgodi wa North Mara kutenga maeneo ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo kuondoa uvamizi kwenye mgodi huo.


Maeneo ya hifadhi

Kuhusu tuhuma dhidi ya askari wa hifadhi ya Taifa ya Rubondo mkoani Geita, tume imebaini kuwepo kwa vitendo vya ukatili na mateso vilisababishwa na askari wa hifadhi na kuwa mahusiano baina ya watendaji, wahifadhi na wananchi si mazuri.

Tume imependekeza katika maeneo ya hifadhi mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii zishirikiane na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzipitia sheria zinazohusu hifadhi ili kuondoa kasoro zilipo.

Aidha amezitaka kuchukua hatua dhidi ya askari wa hifadhi ambao wanatuhumiwa kufanya vitendo vya ukatili na mateso dhidi ya wananchi.


Wasemacho wadau

Kufuatia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga ameipongeza tume kwa kutoa taarifa ambayo imesheheni kila upande kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, taasisi, wakuu wa mikoa na Jeshi la Polisi.

Amesema taarifa hiyo inatoa mwanga kwa asasi za kiraia kupata mwanga wa matendo ambayo yanakiuka haki za binadamu hasa yanapotolewa na Serikali yenyewe, tofauti na ripoti zinazotolewa na asasi za kiraia pekee.

Dk Henga amesema wananchi wanapenda kusikia taarifa kama hizi na hatua zilizochukuliwa na kushauri ziwe zinatoka kila mwezi badala ya kukaa kwa muda mrefu ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema kwa wahusika.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa ameipongeza tume kwa kutoa taarifa hiyo na kuitaka iwe inafuatilia matukio kukemea na kutoa taarifa za matukio.

“Tunaamini hata hili suala la utekaji Tume pia italifanyia kazi,” amesema Olengurumwa.