Tuwalinde wajawazito, waliojifungua na magonjwa ya akili

Tuwalinde wajawazito, waliojifungua na magonjwa ya akili

Muktasari:

  • Afya ya akili kwa mjamzito ni muhimu, kwani ni kipindi ambacho anakutana na mabadiliko ya kimwili, kiakili hadi kihisia.

Afya ya akili kwa mjamzito ni muhimu, kwani ni kipindi ambacho anakutana na mabadiliko ya kimwili, kiakili hadi kihisia.

Ujauzito unaleta mabadiliko ya kiakili kwa mama mjamzito hivyo kuhitaji ukaribu wa chochote kinachotokea kwenye akili, mwili au afya yake.

Magonjwa ya akili kwa wajawazito na wanaojifungua hayatazamwi kwa ukubwa na jamii ila yanajitokeza na kuathiri matibabu.

Shida kubwa ni sonona inayojitokeza kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua. Baadhi hupata kichaa baada ya kujifungua. Hali zote hizi zinachangia magonjwa ya akili kwa wajawazito hata baada ya kujifungua.

Utafiti unaonyesha wanawake wawili kati ya 1,000 hupata sonona na magonjwa mengine ya akili kutokana na sababu tofauti, ikiwamo magonjwa ya kurithi, ulevi, msongo endelevu wa mawazo, magonjwa sugu na kushindwa kukabiliana na matukio kama kufiwa ua kukataliwa kwa mimba.

Duniani kote, afya ya mama na mtoto inapewa kipaumbele kikubwa na ipo katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG) yanayoendelea kutekelezwa hadi mwaka 2030. Kujali afya ya mama na mtoto ni maandalizi ya kujenga jamii bora isiyo na matatizo mengi yanayoweza kujitokeza kwa mama au mtoto.

Kuna kundi la wajawazito ambao huugua akili na wale ambao wamepata ujauzito huku wakiwa wagonjwa wa akili tayari. Jingine ni kundi la wanaopata changamoto za akili ndani ya siku 42 tangu wameshajifungua.

Wapo wanaopata sonona wakishajifungua. Wengine huugua magonjwa ya akili kiasi cha kulazwa kuepusha uamuzi mbaya wanaoweza kuufanya kwao wenyewe na mtoto mchanga. Kumekuwa na visa vingi kwa wanawake waliojifungua kuugua akili kunakoambatana na dalili za mtu kupoteza uhalisia, tabia za ukali, kumwona mtoto aliyejifungua ni tishio kwake na wengine kumtupa mtoto, kumfukia au kuua kabisa. Haya yote hutokea mama akipata maradhi ya akili.

Tatizo hili linahitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu kwa mama mjamzito kuangaliwa na kusaidiwa ikitokea amepata maradhi ya akili. Si hilo tu, sonona inaweza kumfika mjamzito endapo ujauzito wake umekataliwa, maisha duni, kupata ujauzito kabla ya kumaliza masomo au ujauzito ulioambatana na maambukizo ya magonjwa.

Mama mjamzito anayepata changamoto ya kiakili anahitaji uangalizi kukabiliana na hali hiyo ya kiafya. Anahitaji kusaidiwa kuhudhuria kliniki, uangalizi wa ukuaji wa mtoto tumboni na kuwa tayari kubaini hali zozote za hatari zinazoweza kujitokeza nyingi, ikiwamo migogoro ya kifamilia.

Tatizo hili limechangia kwa kiasi baadhi ya wanawake kutengwa au pengine kuachwa na waume zao. Jamii inahitaji kuelimishwa kuhusu tatizo hili ambalo matibabu yake hutolewa hospitalini. Matibabu haya huhusisha matumizi ya dawa mbinu za kisaikolojia kutibu akili na kumwezesha mama kuwajibika kwa mtoto wake na mambo mengine ya kijamii.

Kama hamasa inavyotolewa kwenye magonjwa ya kuambukiza mfano janga la corona lililoibuka hivi karibu[1]ni, maradhi ya akili kwa wajawazito, wanawake waliojifungua au wanaonyonyesha yanapaswa kupewa uzito ili kuipunguzia jamii mzigo wa wagonjwa wasiohudumiwa ipasavyo. Ingawa tatizo hili huwakumba watu wote katika jamii bila kuja hali zao, elimu ianzie kwa kundi hili, kwani lina watu wengi zaidi.

Juhudi zisipochukuliwa idadi ya vifo vya wanawake bada ya kujifungua au watoto chini ya miaka mitano vitaendelea kuongezeka wakati tungeweza kuvipunguza.

Mwandishi ni Dk Raymond Mgeni, ni daktari wa magonjwa ya akili Hospitali ya Rufaa Mbeya. Kwa maoni na ushauri anapatikana kwa namba 0676 559 211