Uchimbaji madini tishio linalohatarisha uhai wa hifadhi za Manyara, Tarangire

Muktasari:
Ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi, mapato yameongezeka kutoka dola 1.7 bilioni mwaka 2012 hadi kufikia dola 2.2 bilioni mwaka 2017.
Sekta ya utalii inaongoza nchini kwa kuingiza fedha za kigeni. Katika pato la taifa mchango wa sekta ya utalii ni zaidi ya asilimia 18.
Ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi, mapato yameongezeka kutoka dola 1.7 bilioni mwaka 2012 hadi kufikia dola 2.2 bilioni mwaka 2017.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Maliasili na Utalii, ongezeko la mapato hayo, linatokana na ongezeko la watalii, kutoka 1.077,058 mwaka 2012 hadi 1.327,143 mwaka 2017.
Miongoni mwa hifadhi ambazo hutembelewa na watalii wengi nchini na hivyo kuchangia ongezeko la watalii na fedha za kigeni ni hifadhi za Taifa za Tarangire na Manyara.
Mhifadhi mkuu hifadhi ya taifa ya Tarangire, Helman Batiho anasema hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 2850 na mapato ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, yameongezeka kutoka Sh9.7 Bilioni mwaka 2012/13 hadi kufikia Sh19 bilioni mwaka 2016/17.
Anasema ongezeko hilo limetokana na ongezeko la watalii wa ndani na nje, watalii wa nje wameongezeka kutoka 112,163 mwaka 2012/13 hadi kufikia 140,405 mwaka 2016/17.
Manyara ni hifadhi ya 11 kwa ukubwa nchini kati ya hifadhi 16 zilizopo., ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 648, pia mapato yake yameongezeka.
Mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo, Noelia Myonga, anasema hifadhi hiyo ipo katika wilaya za Babati, Mbulu mkoani Manyara na Karatu na Monduli mkoani Arusha ipo hatarini.
Mwaka 2015/16 ilitembelewa na watalii 122,626 na mwaka 2016/17 ilitembelewa na watalii 134,045.
Hata hivyo, idadi ya sasa ya watalii wanaotembelea hifadhi imeanza kuwa ndogo ukilingaisha na miaka ya nyuma na huenda pia hilo linachangiwa na uharibifu.
Mwaka 2012/13 watalii waliotembelea hifadhi hiyo walikuwa ni 178,787 na mwaka 2013/14 walikuwa 150,727.
Mapato ya hifadhi hii mwaka 2016/17 yalikuwa Sh11.8 bilioni na mwaka 2017/18 hifadhi hii inatarajia kupata zaidi ya watalii 129,927 na kuingiza zaidi ya Sh11.2 bilioni.
Changamoto zinazotishia hifadhi
Wahifadhi wakuu wa hifadhi hizi, viongozi wa serikali na wawekezaji wanatoa sababu zinazofanana.
Sababu hizo ni, kuongezeka shughuli za kibinaadamu kando kando mwa hifadhi ambako wananchi wamevamia maeneo ya mapito ya wanyama, wanalima kilimo kinachosababisha tope kujaa hifadhini, wanaingiza mifugo na kuchimba madini.
Myonga anasema, kilimo kinachofanyika ni hatari kwa wanyamapori na viumbe wengine kutokana na matumizi ya dawa pamoja na maji mengi.
“Wananchi wanalima kwa kutumia madawa na maji yanaingia ziwani, hivyo ndege aina flamingo na wengine zaidi ya aina 300 wanaathirika,” anasema.
Anasema mashamba ya mpunga yameongezeka maeneo ya Mto wa Mbu na Babati inapopita mito inayoingiza maji ziwani inaleta athari, wanazuia maji kufika ziwani, tatizo ambalo limekuwapo takriban mwaka mzima.
Myonga anasema katika hifadhi yake, kuna migodi ya kuchimba madini aina ya alexandrite, emerald na cristobal ambayo ni miongoni mwa madini ghali duniani. Hiyo ni mbali na machimbo yasiyo rasmi ya dhahabu. “Uchimbaji madini haya umesababisha mashimo makubwa ndani ya hifadhi huku kukiwa na matumizi ya madawa na baruti.”
Anasema tatizo la mifugo kuingizwa hifadhini ni kubwa, mwaka 2015/17 ng’ombe 2,382, mbuzi 518, kondoo 31 na punda wanane walikamatwa hifadhini na wachungaji 114.
Batiho anasema, uhai wa hifadhi yake ni Mto Tarangire unaoleta maji kutoka milima ya Qoro na maeneo mengine.
Anasema shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya mto huo zinaleta athari za kukosekana maji katika hifadhi na kutishia uhai wa wanyamapori na viumbe wengine.
“Kuna wakati mto unakauka, wanyama wengi wanalazimika kutoka nje ya hifadhi, huko wanakutana na changamoto za kuzibwa mapito yao,” anasema.
Anasema pia wanapotoka ndipo yanatokea matukio ya ujangili na kwenda kuvamia mashamba ya wakulima.
Anasema katika sayansi ya wanyama iwapo wanyama wakishindwa kuzunguka hifadhi hizo mbili, kutasababisha wakose vizazi bora, watakuwa na vizazi vya aina moja na yanapotokea maradhi wanaweza kufa wengi.
“Kuzunguka wanyama licha ya kufuata malisho na maji, pia kunawasaidia kuchanganya vizazi na hivyo kujilinda na magonjwa na kuwa na afya bora,” anasema.
Anasema kwa sasa wanyama hawawezi kuzunguka vizuri kama zamani kutoka, Tarangire hadi Manyara na Ngorongoro na wengine kufika hadi Serengeti, katika mapito yao tayari kuna mashamba, makazi ya watu, mifugo na hivyo anashauri hatua zichukuliwe sasa.
Vilio vya wawekezaji na WMA
Hifadhi hizi zinapakana na Hifadhi ya Wanyamapori ya Jamii (WMA) ya Burunge na kuna wawekezaji wa sekta ya utalii ambao wote kilio chao ni kuathirika na ongezeko la shughuli za kibinaadamu.
Mwenyekiti wa Burunge WMA, Ismail Ramadhani anasema hifadhi yao iliyopo katikati ya Tarangire na Manyara inaa ukubwa wa kilomita za mraba 283 na kwamba hifadhi hizo zikifa ni wazi WMA pia itakufa kwani mzunguko wa wanyama katika hifadhi hizo ndio kivutio cha watalii katika eneo lao.
“Mapato yetu yanategemea wanyama wa Tarangire na Manyara, wakiisha ina maana hatutapa kitu kutoka kwa wawekezaji waliopo katika eneo letu,’’ anasema.
Ismail pia anasema mapato ya jumuiya hiyo yameongezeka kutoka Sh37.4 milioni mwaka 2006/07 hadi Sh1.2 bilioni mwaka 2016/17 na kwa mafanikio hayo mwaka jana vijiji 10 vimepata kila kimoja mgao wa Sh 63 milioni.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Alayce Koiney anasema changamoto kubwa ni ongezeko la mifugo na watu katika eneo la hifadhi huku baadhi yao wakiwa ni majangili wa wanyama kwa ajili ya kitoweo.
Jitihada za Serikali
Katika siku za karibuni, baadhi ya watendaji wa Serikali wameanza kuchukua hatua kunusuru hifadhi hizo lakini bado hazijaanza kuzaa matunda.
Hivi karibuni makatibu wakuu wa wizara saba walitembelea eneo la Ikolojia ya Tarangire na Manyara na kushuhudia tishio la kuzipoteza hifadhi hizi.
Ujumbe wa makatibu hao, uliongozwa na mwenyekiti wao, Maimuna Tarishi ambaye alivitaka vijiji vya jirani na Ziwa Manyara kufuata sheria.
Katibu mkuu wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo, anasema wizara yake inatambua umuhimu wa hifadhi hivyo ni muhimu waliofungia maji kuingia hifadhini wayafungulie kwani kilimo kinachoharibu hifadhi hakina maslahi kwa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi anasema uwepo wa machimbo hayo ni chanzo cha kuharibika hifadhi hiyo na kwamba eneo la migodi pia ni mapito ya wanyama lakini kwa sasa limekuwa na mashimo makubwa yanayozuia wanyama kupita.
Mhifadhi Ikolojia wa Tanapa, Yustina Kiwango anasema licha ya kuharibiwa mazingira ya hifadhi ya Manyara pia wachimbaji wanatumia milipuko kama baruti ambayo imekuwa ikitisha watalii.
“Hapa jirani kuna hoteli ya kitalii lakini kunapigwa baruti ambayo imekuwa ikiwasababishia hofu watalii na kudhani eneo hili hakuna usalama,”anasema.