UDSM yaadhimisha miaka 60 ikitoa msaada sekta ya afya

Muktasari:
- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo kimetimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake leo Oktoba 25, 1961 ikiwe ni miezi michache kabla Tanganyika haijapata uhuru.
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo kimetimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake leo Oktoba 25, 1961 ikiwe ni miezi michache kabla Tanganyika haijapata uhuru.
Katika kuadhimisha siku hiyo chuo hicho leo kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika kituo cha afya Kimara.
Vifaa vilivyotolewa ni mashuka 100, viti vya magurudumu matatu vinne na vitakasa mikono vinavyotengenezwa na chuo hicho.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema taasisi hiyo kama sehemu ya jamii imeamua kuadhimisha siku hiyo kwa kuikumbuka jamii.
Amesema maadhimisho ya miaka 60 ya chuo hicho yatafanyika ndani ya mwaka mmoja kuanzia leo.
Profesa Anangisye amesema chuo kimetoa msaada huo kama alama ya UDSM katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na chuo hicho kikongwe.
Amesema chuo kilianzishwa kwa kitivo cha sheria pekee kikiwa na wahadhiri sita akiwemo mwafrika mmoja.
Kitivo hicho kilianza kwa wanafunzi 14 akiwemo mwanamke mmoja ila kwa sasa kuna wanafunzi 43307 katika mwaka wa masomo 2021.
Kati ya hao wanafunzi wa kike ni 19784 sawa na asilimia 45.7.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominic amesema msaada huo una tija kubwa kwenye kituo hicho.
“Mlichofanya leo kwetu ni kikubwa sana kama mnavyoona hali ya kituo hiki, mahitaji ni makubwa ukilinganisha na uwezo tulionao.
“Tunashukuru UDSM kuendelea kuibeba manispaa ya Ubungo kama mtoto wao, nawahakikishia vifaa hivi tutavitunza kuhakikisha vinabaki kwenye ubora wake
Mkurugenzi huyo pia aligusia suala la kuwapanga wamachinga na kuomba msaada wa chuo hicho katika kutekeleza mpango huo.
“Nilikuwa najiuliza hivi kwanini nahangaika na wamachinga wakati kuna wasomi ambao wanaweza kututengenezea muundo wa kitaalam wa biashara.
“Tuna kazi kubwa ya kupanga wamachinga, tunaomba tutumie watalaam wa UDSM kuangalia namna bora ya kuwapanga hawa machinga,” amesema Beatrice.