UDSM yazindua makumbusho ya chuo hicho ikitajwa kuchochea maarifa, tafiti
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimezindua makumbusho ya chuo hicho huku ikitajwa kwenda kuchochea maarifa, elimu, tafiti na tafakari kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Pia imetajwa kuwa alama ya heshima kwa urithi wa kitaaluma, kitamaduni na kihistoria.
Hayo yameelezwa leo Agosti 22, 2025 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dastan Kitandula wakati wa uzinduzi wa makumbusho hiyo inayotajwa kuwa ya kwanza kuanzishwa na taasisi ya elimu ya juu nchini.
Kitandula amesema makumbusho hayo yatatoa nafasi kwa wanataaluma, wanafunzi, na watafiti kuchunguza, kujifunza, na kufanya utafiti wa kina katika mazingira yanayohifadhi historia na urithi wa maarifa mbalimbali.
Kutokana na umuhimu huo amesema serikali ipo tayari kutoa usaidizi unaohitajika katika kuboresha miundombinu, kupanua wigo wa maudhui ya makumbusho hayo.
Pia kuanzisha programu shirikishi zitakazowawezesha wananchi na taasisi nyingine kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi historia na urithi wa taifa .
Ameongeza kuwa uanzishwaji wa makumbusho hiyo ni utekelezaji waSera Utamaduni ya mwaka 1997, pamoja na Mkataba wa UNESCO wa mwaka 1970 uliotiwa saini na Tanzania, ambao unahimiza uhifadhi na uendelezaji wa urithi wa kitamaduni.
Pia Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997 ambayo inasisitiza umuhimu wa kuhifadhi urithi wa kitamaduni kama sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii, na hatua hii ya kuanzisha makumbusho ni utekelezaji wa sera hiyo kwa vitendo.
"Makumbusho hayo yanajenga daraja muhimu la mawasiliano ya kitamaduni na kitaaluma kati ya Tanzania na dunia, na ni ushahidi wa dhamira yetu ya kuhifadhi historia, kuendeleza maarifa, na kuhamasisha ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu."amesema.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye amesema makumbusho hayo si tu jengo la kihistoria, bali pia ni zana muhimu ya kielimu itakayochangia kukuza ubora wa elimu na utafiti katika hicho.
"Kuwepo kwa Makumbusho haya kumetuwezesha kuboresha programu ya Shahada ya Awali katika Masomo ya Makumbusho na Urithi wa Utamaduni, Sasa makumbusho haya yanatumika kama eneo la kazi kwa vitendo kwa wanafunzi"
"Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha elimu tunayotoa inakuwa na mwelekeo wa kiutendaji na uwajibikaji wa kitaaluma"amesema.
Nae Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Balozi Mwanaidi Maajar amesema makumbusho hayo yatakuwa kitovu cha elimu na utafiti kwa wanafunzi, wasomi, na jamii kwa ujumla kwani ndani yake zitahifadhiwa nyaraka muhimu, picha, vielelezo vya kihistoria, na masimulizi ya matukio ambayo yamejenga hadhi na utambulisho wa Chuo hicho.