Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufahamu usiku Mtukufu katika Ramadhan unaopatikana kwenye 10 la mwisho

Muktasari:

  • Usiku huo unatajwa kuwa Mtakatifu na endapo muumini atafanya ibada yoyote kwenye usiku huo, itakuwa bora kuliko ibada atakayoifanya kwa kipindi cha miezi 1,000.

Mwanza. Katika imani ya Kiislamu, 10 la  mwisho la funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan linatajwa kuwa na usiku Mtakatifu (Laylatul Qadri) unaodaiwa kuwa ibada moja kwenye usiku huo ina thawabu nyingi zinazolinganishwa na malipo ya kufanya mema kwa kipindi cha miezi 1,000.

Leo Jumapili Aprili 7, 2024 ni siku ya 27 tangu Waislamu nchini walipoanza ibada ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ikiwa ni  10 la mwisho la mfungo huo ambao huwa ama na siku 30 au 29 kulingana na mwandamo wa mwezi.

Kutokana na imani hiyo, waumini wa dini hiyo wanatakiwa kuutafuta usiku huo unaodaiwa kuwa kati ya siku ya 21, 23, 25, 27 na 29 ambao mwenye kuupata siyo tu atapata heri duniani, bali pia atasamehewa madhambi anayoyajua na asiyoyafahamu.

“Usiku huu mmoja thamani yake ni sawa na miezi 1,000…mtu akifanya jambo la kheri dogo lolote, analipwa sawa amefanya kwa miezi 1,000,” amesema Kaimu Shekh wa Mkoa wa Mwanza, Othman Masasi.

Shekh Masasi amesema miongoni mwa mambo yanayolipa uzito 10 la mwisho kwa muumini ni kufuturisha ikiwa ana uwezo huo bila kujali aliyefunga au hajafunga, akidai wema wa mja anaujua Mungu.

Amesema Mwenyezi Mungu ameweka ibada tukufu katika 10 la mwisho la Ramadhan zinazozidisha imani, kukamilisha ibada na kutimiza neema.

Ostadhi wa madrasa Buswelu jijini Mwanza, Athman Ali amesema siyo kweli kama watu wengi wanavyofahamu kuwa Laylatul Qadri ni nyota, mwezi au jua, bali ni siku ambayo Mwenyezi Mungu kaiweka duniani ambayo waja wakifanya ibada wanapewa ziada ya thawabu.

“Laylatul Qadri ni siku maalumu ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka katika ulimwengu kama ‘promotion’. Allah ameiweka kwa wanadamu kwamba akifanya ibada siku hiyo analipwa thawabu nyingi ambazo ni ziada ya ziada, si kwamba ni nyota, mwezi au jua, la!

“Hiyo siku unaweza kupata hata kama hujaona jua na wala hakuna kitu cha kuona kama jua wala nyota…Mtu mwingine anakwambia mimi nimelala nimeona linyota likubwa huo ni uwongo,” amesema.

Akifafanua sababu la kuitwa 10 la mwisho la Laylatul Qadri, amesema Laylatul Qadri ni neno la Kiislamu ambalo kwa Kiswahili maana yake ni “siku ya makadirio”.

Amesema siku hiyo ndiyo hukadiriwa kila kitu cha kuiendesha dunia, kwa mfano kama ingekuwa ni mambo ya kidunia, ingeitwa siku ya bajeti kama vile waziri wa fedha na mipango anavyoingia bungeni akasoma bajeti ya nchi ya mwaka mzima.

“Siku hii ya Laylatul Qadri huwa Allah Tabarak wa Taala anapitisha makadirio ya kuendesha dunia yake ndani ya mwaka huu, watu wangapi wafe, wazaliwe, anapangilia ridhiki za watu, anapangilia ajali za watu, maisha ya watu, mvua zitakuwaje, mavuno yatakuwaje mambo yote ya kuiendesha dunia Mwenyezi Mungu anayapangilia siku hii.”

“Ndiyo maana Mtume Muhammad (SAW) alifundisha mwenye kudiriki siku hiyo na ahakikishe anasoma dua hii…‘ewe Mwenyezi Mungu, hakika yako ni msamehevu na unapenda kusamehe basi nisamehe’.

Ostadhi Ali amesema siku hiyo ambayo hupatikana katika siku za witiri yaani 21, 23, 25, 27, 29 kwenye 10 la mwisho la mwezi wa Ramadhani, mwenye uwezo wa kufanya ibada basi atapata heri kubwa na ibada zake ni kusali, kusoma Quran, kuomba dua na kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi na heri mbalimbali zinazopatikana, ambazo mtu anaweza kufuturisha na kutoa sadaka.

“Mtu akifanya ibada katika hizi siku za Laylatul Qadri ambazo amezizungumza Mtume, basi anaandikiwa kana kwamba kapata thawabu za miezi 1,000 sawa na miaka 83, ndiyo maana Mtume akasisitiza sana watu wafanye ibada katika siku hizi,” amesema.

Ameongeza: “Wapo watu wanaoishi hiyo imani, kwa mfano wengine wamehamia misikitini kufanya ibada katika hili 10 la mwisho kwa lengo la kupata zile radhi za Mwenyezi Mungu, na ndio maana Mtume akasema mwenye kusimama kisimamo kitukufu cha mwezi wa Ramadhai kwa imani na kujitakasa na kujitajia malipo kwa Mwenyezi Mungu, basi husamehewa madhambi yake yote aliyotanguliza.”

Waumini wanavyoifahamu

Muumini wa dini ya Kiislamu, Nasra Maludili amesema pamoja na usiku huo, katika fungu hilo mtu akitoa sadaka hata kidogo malipo yake kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa, hivyo kuwasihi Waislamu pia kujikita kutubu dhambi.

“Mwenyezi Mungu amewaambia waja wake, hizi siku 10 za mwisho za mwezi wa Ramadhan, kuna siku moja ya kukesha ila ukifanya vizuri kuanzia kufuturisha na kukesha kumsabihi Allah, Mwenyezi Mungu anagawa fungu yaani kwa makadirio unapewa thawabu, anazijua Allah, sisi hatuzijui.”

“Ili mtu apate thawabu katika siku hizo azidishe kutoa sadaka, kumthamini Allah na kumuomba msamaha kwa mambo yote uliyoyajua na usiyoyajua. Muhimu kutubu sana ili unapomaliza mwezi Mtukufu unabaki mweupe, msamaha umeshatoka ila sasa usirudie kule ulipotoka (madhambi),” amesema Maludili.

Muumini mwingine wa dini hiyo, Halima Juma amesema kwa ufahamu wake, 10 hilo la mwisho, Mwislamu anatakiwa atoe sadaka kulingana na kipato chake kwa kusaidia yatima, wasiojiweza au kufuturisha.