Uharibifu wa barabara Mara waiibua Tarura

Mwendesha pikipiki akipita katika sehemu ya barabara iliyoharibika katika Kijiji cha Mariwanda  wilayani Bunda.  Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Barabara za udongo zaathiriwa zaidi.

Musoma. Asilimia 33 ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani Mara zimaharibika hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji.

Hali hiyo inaelezwa imetokana na mvua zinazoendelea kunyesha, huku barabara zilizoathiriwa zaidi ni zile za udongo.

Meneja wa Tarura Mkoa wa Mara, Wilson Mwita ameiambia Mwananchi Digital leo Februari 19, 2024 kuwa jitihada zinafanyika kuhakikisha barabara hizo zinarejea katika hali nzuri ziweze kutumika.

"Tuna mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 4,559, kilometa 2,446 ni za udongo, huku za lami ni kilomita 48 tu na zingine ni za changarawe. Zilizoathiriwa sana ni hizo za udongo," amesema.

Amesema kati ya hizo asilimia 41 ya barabara ndizo zipo katika hali nzuri, huku asilimia 26 zikiwa katika hali ya wastani.

Takwimu hizo amesema ni za hadi Januari mwaka huu.

Amesema mbali ya mvua, kulitokea changamoto za kimkataba hali iliyosababisha mikataba 27 kuvunjwa na zabuni kutangazwa upya kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Mwita amesema miradi 68 ya barabara imetangazwa na wapo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa kuanza kazi, hivyo changamoto ya ubovu wa barabara itapungua kwa kiwango kikibwa.

Amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwani bajeti imeongezeka kutoka Sh8 bilioni mwaka 2022/23 hadi kufikia Sh27 bilioni kwa mwaka 2023/24.

"Kikubwa kinachotukwamisha ni kwamba, hauwezi kufanya matengenezo wakati mvua zinanyesha labda kama kuna dharura, mfano mawasiliano yamekatika kwa hiyo tunasubiri mvua ziishe ili kazi ziweze kuendelea," amesema.

Mwita amesema licha ya Serikali kuongeza bajeti ya mkoa kwa zaidi ya mara tatu lakini mahitaji bado ni makubwa.

Amesema kwa hali halisi, mkoa unahitaji bajeti ya zaidi ya Sh61 bilioni ili kuimarisha kabisa mtandao wa barabara.

"Pamoja na Serikali kutokuwa na fedha za kutosha lakini tunaona namna ambavyo inajitahidi kuhakikisha  chagamoto zinapata ufumbuzi na kwa vile nchi ina mahitaji mengi, inabidi hicho kidogo kilichopo kigawanywe angalau kila sehemu wapate," amesema.

Baadhi ya wakazi wilayani Bunda wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara.

"Huku sisi ni wakulima na barabara yetu ni mbovu, hivyo tunapata wakati mgumu kusafirisha mazao kuenda sokoni kwa sababu barabara haipitiki kabisa tunaiomba Serikali ifanye jambo hapa," amesema Mashindi Mgara, mkazi wa Kijiji cha Mariwanda wilayani Bunda.

"Barabara zimekuwa mbovu kiasi hata sisi bodaboda tunashindwa kufanya biashara, unakodiwa kumpeleka mtu huko vijijini lakini ukiwaza hali ya barabara unaamua kuachana na tenda hiyo kwa sababu utaharibu pikipiki yako kwa jinsi barabara zilivyo mbovu," amesema Bulombo Mbajo, mkazi wa Bunda.