Ujenzi Hospitali ya Wilaya Serengeti kukamilika mwaka huu

Naibu Waziri ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jaffo akijibu maswali bungeni leo. Picha na Emmanuel Herman

Muktasari:

  • Hilo limesemwa  leo  (Jumanne Julai 4) na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo aliyebainisha kwamba uandaaji wa michoro na jengo la upasuaji lenye vifaa vyote vimekamilika na kukabidhiwa kwa halmashauri husika tayari kwa matumizi.

Dodoma. Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Hilo limesemwa  leo  (Jumanne Julai 4) na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo aliyebainisha kwamba uandaaji wa michoro na jengo la upasuaji lenye vifaa vyote vimekamilika na kukabidhiwa kwa halmashauri husika tayari kwa matumizi.

"Ni azma ya Serikali kukamilisha ujenzi wa hospitali mbalimbali za wilaya nchini ili kuwasaidia wananchi wapate huduma bora za afya," amesema Jaffo.

Hospitali hiyo itakayogharimu Sh5.4 bilioni ilianza kujengwa mwaka 2009.

Ufafanuzi wa Jaffo umetokana na swali lililoulizwa na Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha aliyetaka kujua hospitali hiyo itakamilika lini ili kuanza kutoa huduma.

Serengeti ni miongoni mwa maeneo yanayopokea watalii wengi nchini hivyo kuhitaji miundombinu hiyo kwa afya ya wananchi na wageni wanaoitembelea.